Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar
Tenga amemshukuru Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kwa
kusajili Katiba ya TFF toleo la 2013 kutokana na marekebisho
yaliyofanywa na Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika Julai 13 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo (Agosti 5 mwaka
huu), Rais Tenga ameishukuru Serikali, Msajili, Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, Naibu wake Amos
Makala na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa ushirikiano ambao wametoa
kwa TFF katika kufanikisha suala hilo.
Amesema baada ya kupokea
usajili huo, kinachofuata ni Katibu Mkuu wa TFF kumwandikia rasmi
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ili aanzishe mchakato wa uchaguzi wa
viongozi wa TFF.
Kuhusu kauli ya Naibu Waziri Makala kuwa
marekebisho hayo yasingeweza kusajiliwa kwa sababu hayakufuata Katiba ya
TFF, Rais Tenga amesema alikuwa ana haki ya kusema hivyo kwa sababu
hakuwepo kwenye Mkutano huo, na kuongeza:
“Makala hakuwepo kwenye
mkutano ndiyo maana alisema hivyo. Ana haki ya kuuliza, nina hakika
sasa atakuwa ameeleweshwa na ameelewa kwa sababu ni msikivu. Kuhusu
marekebisho hayo kupigiwa kura, hilo lisingewefanyika kwa sababu
hakukuwa na mjumbe aliyepinga marekebisho,” amesema.
Rais Tenga
amesema marekebisho hayo yalipitishwa kwa kauli moja (unanimous) hivyo
hakukuwa na sababu ya kuanza kunyoosha mikono kupiga kura, kwa maana
hiyo mkutano ulipitisha marekebisho kwa asilimia 100 wakati Katiba
ilikuwa ikihitaji theluthi mbili tu.
“Hakukuwa na dispute
(mabishano) kuhusu marekebisho, isipokuwa wajumbe walitumia muda mwingi
kuboresha kanuni na kutoa ushauri wa aina ya watu ambao wangeingia
kwenye kamati mbalimbali zikiwemo zile mpya za Maadili,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa vile wote walioingia kwenye Mkutano Mkuu huo Maalumu
ni watu wa mpira wa miguu wasingeweza kupinga marekebisho kwa vile
yametokana na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA).
“Labda itokee aliyeingia kwenye mkutano alikosea njia.
Mtu yeyote wa mpira wa miguu ni lazima afahamu kuwa maagizo ya FIFA ni
lazima yatekelezwe, na Katiba ya TFF inasema hivyo,” amesema Rais Tenga.
Pia Rais Tenga amewataka wapenzi wa mpira wa miguu kushawishi watu
wenye sifa na uwezo wa kuongoza kujitokeza kwa wingi wakati Kamati ya
Uchaguzi itakapotangaza mchakato na tarehe ya uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment