Habari na na Julieth Mkireri, Pwani - Tanzania Daima.
WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamevamia na kupora fedha
katika kituo cha mafuta cha Derina, kilichopo maeneo ya Picha ya Ndege,
wilayani Kibaha, mkoani Pwani, kinachomilikiwa na mfanyabiashara David
Mosha.
Majambazi hao wanaokadiriwa kufikia kumi, walikivamia kituo hicho
baada ya kuwateka walinzi wa kituo hicho na kupora mali mbalimbali
ambazo hadi sasa thamani yake haijajulikana.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Urlich Matei, amethibitisha kutokea
kwa tukio hilo ambapo alisema lilitokea usiku wa kuamkia Agosti 20,
majira ya saa saba usiku.
Kamanda Matei alisema majambazi hao ambao walikuwa na silaha za moto,
walikwenda katika kituo hicho cha mafuta wakiwa na magari mawili, moja
aina ya Prado na jingine aina ya Saloon, lenye rangi nyeupe.
Aidha, alifafanua kuwa majambazi hayo yalipofika yaliegesha magari
hayo karibu kabisa na pampu za kuwekea mafuta na baada ya hapo
waliteremka na kuwaweka chini ya ulinzi walinzi waliokuwa zamu siku
hiyo.
“Kitu ambacho walikifanya majambazi hao, walijifanya kama vile
wanataka kuweka mafuta kumbe nia yao ilikuwa kupora mali, kwani
waliposhuka wakateremka na kumkamata mfanyakazi ambaye alikuwa zamu siku
hiyo,” alisema.
Kamanda Matei alisema kwamba baada ya kumkamata mfanyakazi aliyekuwa
zamu ajulikanaye kwa jina la Samson Rufunga (33), pia wakaenda kumkamata
na mlinzi wa kituo hicho aliyejulikana kwa jina la Mohamed Shaban
(47).
Matei aliongeza kuwa baada ya kuwafunga kamba za miguuni na
mikononi waliwachukua wote wawili na kuwapeleka katika chumba kimoja
kilichpo katika kituo hicho na kisha kuwafungia ndani.
Akifafanua zaidi kamanda huyo alibainisha kuwa majambazi hayo mbali na
kuwateka wafanyakazi wa kituo hicho pia walimkamata Frank Nyamahaga
(28), mkazi wa Tabata ambaye walimpora sh 100,000.
Mbali na kumpora fedha hizo pia walimchukulia funguo zake za gari
aina ya Scania, ambalo lilikuwa limeegeshwa katika kituo hicho cha
mafuta pamoja na kumpora simu zake mbili za mkononi aina ya Nokia zenye
thamani ya sh 120,000.
Mwingine aliyeporwa vitu ni Isaac Silinu (25), utingo wa Scania hiyo,
mkazi wa Ipogoro, Iringa ambaye naye aliporwa simu wakati Shabani
Ramadhani (42) mkazi wa Mwembetogwa, Iringa naye aliporwa simu.
Watu wengine walioporwa katika kituo hicho ni Issa Mohamed (25)
mfanyabiashara, mkazi wa Frelimo Iringa, ambaye aliporwa simu na sh
68,000.
Aidha, dereva wa pikipiki, Juma Selemani (30) mkazi wa
Mwanalugali ambaye alikwenda kituoni hapo kwa ajili ya kujaza mafuta,
naye aliporwa pikipiki yake aina ya SANLG na sh 4,600.
No comments:
Post a Comment