Na Irene Mwamfupe Ndauka.
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:Nilichukua kama saa moja kutoka kazini hadi kufika nyumbani. Nje
nilikuta mfuko wa rambo mweusi, ndani yake ulionekana kuwa na kitu kwani
ulikuwa umetuna sana. Niliinama kuipekenyua ili nijue ndani kulikuwa na nini,
nilishangaa kuona ni vipande vya nyama za kuchoma tena vilikuwa na moto.
“Kha! Atakuwa nani ameweka?” nilijiuliza mwenyewe, nikauacha palepale, mimi nikapanda ngazi za kuingia ndani. Mlango ulikuwa wazi hali iliyoashiria kwamba, wenzangu walisharudi. Nilisukuma mlango, nikaingia. Nilikutana na harufu ya pafyumu, nikahisi walikuwa wakijiandaa kutoka.
("Kitabu cha Niliyoyaona Mochwari Sitasahau kinapatikana sehemu zote za Tanzania kwa wauza Magazeti ni Tsh 3000/=tu")
“Jamani za leo?” nilisalimia kwa sauti ya juu licha ya kwamba,
mlango wao ulikuwa umefungwa, hakuna aliyeniitikia, hilo sikulijali sana kwani
niliamini kwa kuwa walikuwa ndani, isingekuwa rahisi wasikie salamu yangu.
Niliingia sebuleni kwangu, kisha nikaenda chumbani, kuna kitu
kilinishangaza, nikasimama kwa mshtuko. Nilikuta sehemu nilipoweka kiberiti
asubuhi siyo, nilikiacha juu ya meza, nikakikuta juu ya kitanda. Niliacha kioo
na kitana juu ya kitanda, lakini nikavikuta kwenye stuli, niliguna!
Nilikishika kioo cha kukiangalia kwa umakini kama kina mabadiliko
yoyote, lakini sikuona, nikashika kitana. Nilipokigaua sana pia sikuona kitu
cha tofauti, nikaamua kuchania, nikahisi kuguswa na kitu kama nywele ndefu kama
za mtu aliyefuga. Nilikiweka kitana juu usawa wa dirishani, nikaona
nywelenywele nene, nyeusi, mwili wote ukasisimka.
Ninavyojua mimi, mwanamke mwenye nywele nyingi akichania kitana,
ndiyo huacha nywele, sasa mimi nilikuwa na nywele fupi sana zisingeweza kuacha
nywele ndefu kwenye kitana.
“Mh! Hapa kuna kinachoendelea,” nilisema moyoni huku nikikaa.
Nilishtuka zaidi kuona soksi zikiwa kwenye msumari nyuma ya mlango wakati
niliacha chini.
“Huyu ni nani?” niliuliza kwa sauti ya ukali.
Ghafla nikasikia kicheko kutoka chumbani kwa wale wenzangu.
Nilikaa kwenye kochi, nikaanza kuangalia sehemu mbalimbali za mle
ndani ambazo niliamini naweza kuona mabadiliko mengine mbali na yale ambayo
nilishayaona, lakini sikubahatika.
Nilitoka, nikaenda sebuleni ambako nako nilianza kuangalia kila
kona ya sebule. Nilishangaa kuona glasi ya maji ya kunywa ambayo niliitumia
asubuhi kisha nikaacha maji yamejaa, ikiwa haina hata tone la maji mbaya zaidi,
iliwekwa juu ya kabati ambapo mimi niliiweka kwenye meza ya katikati ya sebule.
“Mh! Hii kali sasa,” nilijikuta nikisema kwa sauti, mara nikasikia
kicheko tena kutokea upande wa pili kule kwa wenzangu. Sasa nikaanza kama
kuhisi kitu kuhusu watu hao. Ni kwanini kila nilipoongea kwa sauti ndipo na wao
waliangua kicheko?
Niliamua kujaribu tena, nikasema kwa sauti:
“Nitakuja kuua mtu, kweli tena.” Nikasikia kicheko tena, safari
hii kilidumu kwa muda.
Moyoni nikasema naanza kufanyia kazi uhusiano wa maneno yangu na
vicheko vya wale majirani. Nilitoka kurudi chumbani, wakati napita kwenye
korido, nilisimama jirani na mlango wao. Walikuwa wakiongea, lakini
niliposimama mimi, kukawa kimya ghafla kama hakuna watu.
Nilipozama chumbani, nyuma wakaanza kuongea tena. Sikufunga mlango
ili niweze kusikia wanachokiongea, lakini jamani kwa kusema ule ukweli wa
Mungu, sikujua walikuwa wakitumia lugha gani katika kuwasiliana hata pale
nilipojitahidi kutega masikio kwa umakini wa hali ya juu sana.
Kuna wakati utadhani wanatumia sana neno dotikom, lakini ukisema
usikilize zaidi unasikia wakisema sana kotoko au kiburate, wakati mwingine
sauti ya kike ilisema kaunto, ya kiume ikarudia hivyohivyo, kaunto.
Nia yangu kubwa ilikuwa kuwaona kwa sura na kufahamu kama ni ngozi
nyeusi au nyeupe. Hilo peke yake lingenipa mwanga ni watu wa aina gani naishi
nao pale ndani ya nyumba.
Nilisikia mlango wa chumbani kwao ukifunguliwa na mimi nikatoka
haraka sana, cha ajabu sikuona mtu akitoka lakini mlangoni kulikuwa na
kandambili pea moja tu wakati zilikuwa pea mbili.
Hilo lilimaanisha kwamba, mmoja wao alitoka kwenda chooni,
nilichofanya ni kuamua kusimama katikati ya mlango wangu ili huyo aliyekwenda
chooni akirudi nimuone. Ni kweli mmoja wao alikwenda chooni kwani nilisikia
mlio wa maji.
Nilijiahidi kusimama mlangoni kwangu kumsubiria. Kwa ramani ya
nyumba ile ilivyo, asingeweza kutoka chooni bila mimi kumwona hata kama
angekuwa anataka kutoka kwenda nje au uani.
Mlio wa maji ulikosa kusikika, nikawa natumbulia macho kule huku
moyoni nikisema:
“Leo ndiyo leo, asemaye kesho mwongo, hata afanyaje, hawezi
kunichenga hapa hata kidogo,” nilisema moyoni, ingawa wakati huo mapigo ya moyo
yalikuwa yakinienda kwa kasi.
Nilipoanza kuhisi muda unakwenda na hakuna mtu aliyetoka, nikampa
dakika tatu kwamba lazima atakuwa anavaa ndiyo maana anachelewa:
“Labda alikuwa anajisaidia haja kubwa, maana wengine huwa wanavua
nguo zote, lakini mimi nipo, siendi kokote,” nilisema moyoni nikiwa bado
nimesimama mlangoni kwangu.
Baaad ya muda, nikasikia watu wakiongea chumbani kwao, nikashtuka,
nilijikuta nikisema:
“Haa!”
Haraka sana nilitupa macho mlangoni kuangalia kandambili,
nikazikuta pea mbili, nikashangaa:
“Ina maana amenipita hapahapa au? Haiwezekani, asingeweza kunipita
hata kama ingekuwaje?” niliwaza. Nilitoka kuelekea chooni, nikakuta mlango uko
wazi, nikachungulia ndani, hakukuwa na mtu, nikanyoosha mikoni, nikarudi ndani.
Nilifikia kwenye kochi sebuleni, nikahema kwa nguvu kwani
niliamini nimo ndani ya miujiza mikubwa ya ndani ya nyumba ile.
“Hivi ni kwanini dalali alinidanganya hivi?” nilijiuliza mwenyewe
nikiamini kwamba, dalali aliyenipangisha nyumba ile alijua mchezo mzima ila
alitaka kupata fedha tu ndiyo maana alinipangisha bila kunipa tahadhari.
Nilitoka sebuleni, nikaenda chumbani, kitandani nikakuta ‘toilet
paper’ ikiwa imekatwa sehemu. Mimi niliicha pembeni ya dirisha, lakini
ikaonesha kuna mtu aliichukua na kunyofoa kidogo kisha badala ya kuirudishia
palepale, yeye aliiacha kitandani.
Mbali na ‘toilet paper’ pia kuna kikopo chenye vijiti vyenye pamba
za masikio kilikuwa kwenye stuli jirani na kitanda, lakini kwa muda huo
kilikuwa kimeanguka chini halafu vijiti vimebaki kama vitatu tu kwa maana
kwamba, aliyeingia kuchukua ‘toilet paper’ ndiyo huyohuyo aliyechota vijiti vya
pamba.
Nilianza kuhisi kuwa sikuwa
kwenye nyumba salama, lakini kwa uthibitisho upi?
Usikose sehemu ya 03 siku ya jumatano ijayo...
No comments:
Post a Comment