Habari na Tanzania Daima.
HOFU ya kutokea vurugu za kidini imeanza kuyakumba baadhi ya
maeneo ya Jiji la Dar es Salaam baada ya sakata la kupigwa risasi Katibu
wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Juzi idadi kubwa ya askari polisi walikuwa wakirandaranda nje ya
misikiti baada ya kuwapo taarifa za waumini wa Kiislamu kufanya
maandamano ya kutaka ukweli wa sakata la kiongozi huyo uanikwe.
Hata hivyo maandamano hayo hayakufanyika na ikatangazwa kuwa leo
katika viwanja vya Nurul Yakin wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam
kutafanyika mkutano mkubwa.
Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Rajabu Katimba,
alisema wanapinga kupigwa risasi kiongozi wao, kusomewa mashtaka akiwa
hospitalini na kupelekwa gerezani kabla hajapata ahueni.
Anasema katika mkutano huo watalizungumzia suala hilo kwa mapana na watapata msimamo wa pamoja juu ya kulishughulikia.
Tanzania Daima Jumapili liliwasiliana na Sheikh Mkuu wa Tanzania,
Mufti Shaaban Issa Simba, juu ya mkutano huo ambapo alisema yeye si
msemaji wa Shura ya Maimamu.
Alisema Jumuiya na Taasisi za Kiislamu zipo kisheria, hivyo zina
mipaka yake na zinafanya mambo kulingana na taratibu zilizojiwekea.
Alisema yeye ana mamlaka ya kuzungumzia masuala yanayohusu Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Wakati sakata hilo likizidi kuwa tete, familia ya Sheikh Ponda imesema
inakusanya ushahidi wa tukio la kupigwa risasi kwa kiongozi huyo na
itauweka hadharani ukikamilika.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, msemaji wa familia ya Sheikh
Ponda, Is-haq Rashid, alisema licha ya ndugu yake kuwa gerezani, familia
inaendelea kukusanya ushahidi wa kilichotokea Morogoro na
watakapokamilisha watauweka hadharani.
Alisema miongoni mwa ushahidi wanaoukusanya ni taarifa za daktari aliyemtibu Sheikh Ponda kwa mara ya kwanza mkoani Morogoro.
“Tumechoshwa na udhalilishaji aliofanyiwa ndugu yetu, sasa tumeamua
kuweka hadharani ushahidi wa maovu yaliyofanywa na polisi,” alisema.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa sakata la Ponda hivi sasa
linaipa wakati mgumu serikali na Jeshi la Polisi ambalo awali
lilikanusha kumpiga risasi kiongozi huyo.
Inadaiwa serikali inahofia sakata hilo litakuza tofauti za kidini
zilizoanza kujitokeza hivi sasa miongoni mwa jamii lakini pia kulipaka
matope Jeshi la Polisi.
Inaelezwa kukamatwa kwa askari anayedaiwa kufyatua risasi katika
msafara aliokuwemo Sheikh Ponda kunalenga kutuliza hali ya mambo
iliyoonekana kuiendea vibaya serikali na vyombo vyake.
Tanzania Daima Jumapili limeelezwa licha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Morogoro, Faustine Shilogile, kukana jeshi hilo kuhusika katika tukio
hilo, serikali imeamua kulivalia njuga ili kutuliza hasira za waumini wa
kiongozi huyo wa kidini.
Kauli ya kamanda huyo ilizidisha hasira miongoni mwa wanaomuunga mkono
Sheikh Ponda, huku wakitaka Shilogile ajiuzulu kwa kusema uongo.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa tayari msako wa kumtafuta
daktari aliyemtibu kwa mara ya kwanza kiongozi huyo wa kidini umeanza.
Daktari huyo inadaiwa ndiye aliyeweka wazi kuwa jeraha la Sheikh Ponda
limetokana na risasi, ingawa hadi sasa hospitali na jina la daktari
huyo havijawekwa wazi.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Kamanda Shilogile alisema
wanafanya jitihada za kumjua daktari na hospitali aliyopatiwa matibabu
kwa mara ya kwanza Sheikh Ponda.
“Polisi hatuna taarifa sahihi ya wapi alikotibiwa kiongozi huyo,
tunafanya jitihada za kujua ni wapi alikotibiwa, habari kuwa alitibiwa
hospitali fulani hapa Morogoro hazina ukweli,” alisema.
Tanzania Daima Jumapili lilitaka kujua kwanini polisi wanamshikilia
askari anayedaiwa kufyatua risasi hewani katika harakati za kumkamata
Sheikh Ponda wakati walisema hawahusiki.
Kamanda Shilogile alikataa kulitolea ufafanuzi jambo hilo kwa madai
kuwa kuanzia sasa suala la Ponda litakuwa likizungumzwa na Makao Makuu
ya Jeshi la Polisi waliounda tume ya kulichunguza.
No comments:
Post a Comment