Kikao cha Bunge la Afrika Mashariki (EALA), jana kilivunjika kwa
mara ya pili baada ya Wabunge wa Tanzania, kutoka ndani ya ukumbi
wakipinga kanuni kuvunjwa juzi.
Baada ya wabunge wa Tanzania kutoka nje, Spika wa
Bunge hilo, Margareth Zziwa aliahirisha Bunge kwa dakika 15 ili kuweka
mambo sawa, lakini jitihada za kuwashawishi ziligonga mwamba na kuamua
kuahirisha Bunge hadi leo.
Hata hivyo, Mbunge wa Tanzania, Makongoro Nyerere
hakuungana na wenzake kugoma kwani alibakia ukumbini na kuungana na
wabunge 32 wa Burundi, Kenya, Uganda na Rwanda.
Awali, Mbunge Abdullah Ali Hassan Mwinyi alitoa
msimamo wa wabunge wa Tanzania kuwa walitoka, kupinga kitendo cha
wabunge wengine kudharau kiti cha Spika juzi na kutoka nje ili
kushinikiza hoja yao.
Mwinyi alisema ili kushinikiza kuheshimiwa kiti
cha Spika, wameamua kutoka nje ya ukumbi huo kwa kuonyesha hawaungi
mkono, tabia ya baadhi ya wabunge kushinikiza hoja zao, kujadiliwa na
Bunge hata kwa kukiuka kanuni na taratibu.
“Jana(juzi) ilikuwa ni mara ya pili wenzetu,
kudharau kiti cha Spika na kutaka kutoa hoja na kujadiliwa bila kufuata
kanuni, sasa tumeona ni vizuri na sisi kwa kupinga kuvunjwa kanuni,
tutoke ili kuonyesha tunapinga mchezo huu,” alisema Mwinyi.
Mwinyi alisema kitendo cha wabunge wenzao kutoka
nje ya ukumbi kwa kukataliwa kuvunja taratibu, kinadhalilisha kiti cha
Spika na hata wabunge wenyewe.
Mbunge mwingine wa Tanzania, Twaha Taslima alisema
kanuni zipo wazi kuwa kama mbunge ana hoja na kutaka Bunge lijadili
mambo ambayo si ya dharura ni lazima aiwasilishe saa 24 kabla kwa Spika.
“Sasa jana(juzi), Mbunge wa Kenya, Peter Mathuki
alitaka hoja yake ya kutaka utaratibu wa kufanyika bunge kwa mzunguko
ijadiliwe kitu ambacho hakikuwa sahihi,” alisema Taslima.
Muthuki, juzi aliungwa mkono na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), isipokuwa Tanzania.
Jana aliwasilisha hoja hiyo kwa kufuata utaratibu lakini haikujadiliwa baada ya wabunge wa Tanzania kutoka nje.
Katika hoja hiyo, msimamo wa wabunge wa Tanzania
na Kamati ya Uongozi ya Bunge ni kuwa vikao vyote vifanyike katika
ukumbi wa Bunge, Arusha baada ya kukamilika.
Wabunge wa Tanzania ambao jana walitoka ni Shyrose Bhanji, Profesa Nderakindo Kessy na Taslima. Wabunge wanne hawakuwapo.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo, kama wabunge
watatu wa nchi moja, wakitoka nje kupinga jambo lolote basi kikao
kinaahirishwa kwa dakika 15 na wasiporejea bunge linaahirishwa.
Akizungumzia mgogoro huo, Ofisa Habari wa EALA,
Bobi Odiko alisema kilichotokea jana si ukiukwaji wa taratibu na
kuongeza kuwa ana imani mambo yatakuwa sawa na vikao vitaendelea leo kwa
amani.
-Mwananchi
-Mwananchi
No comments:
Post a Comment