MKAZI wa Tengerea, wilayani Mkuranga, Pwani, Hassan Mohammed
(42) maarufu kwa jina la Nailoni, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za
kumuua binti yake kwa kumkata kwa panga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema tukio hilo
lilitokea usiku wa kuamkia Septemba 20 mwaka huu katika Kijiji cha
Tengerea, ambako Mohammed alimuua bintiye, Amina Hassan (17) kwa
kumkata panga shingoni na kichwani.
Kamanda Matei alieleza uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa huyo ana
maradhi ya akili. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya
ya Mkuranga kwa uchunguzi.
Katika tukio lingine, Hamisi Maliki, mkazi wa Hoyoyo ameuawa na
wananchi baada ya kutuhumiwa kuvunja duka la Edward Mikael, katika
Kijiji cha Mivule Wilaya ya Mkuranga.
Katika tukio la tatu, mtu mmoja amefariki dunia na mwingine
kujeruhiwa baada ya gari T 748 ADX Scania kupasuka tairi la nyuma kulia
na kupinduka katika Kijiji cha Msolwa Wilaya ya Bagamoyo.
Kamanda Matei alimtaja aliyefariki dunia kuwa ni Marid Mtamwa, mkazi
wa Njombe na majeruhi ni Erick Mvula, utingo wa gari hilo ambaye
amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi.
No comments:
Post a Comment