Habari na Edson Kamukara wa Tanzania Daima.
HUKU akijitapa kuwa ndiye mlinzi wa kanuni za Bunge, na
akiwalaumu wabunge, hasa wa upinzani, kwa kukiuka kanuni hizo, Naibu
Spika wa Bunge, Job Ndugai, amebainika kuwa alivunja kanuni nyingi za
Bunge siku ilipozuka zogo bungeni.
Kwanza, alivunja kanuni inayomtaka ampe fursa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuzungumza.
Pili, alivunja kanuni inayomruhusu kumchukulia hatua mbunge aliyedharau kiti cha spika.
Tatu, alivunja kanuni inayomtaka kuahirisha Bunge kabla ya kuruhusu askari kuingia bungeni unapotokea mzozo.
Kanuni ya 5 (1) inasema: “Katika kutekeleza majukumu yake yaliyotajwa
katika ibara ya 84 ya katiba, spika ataongozwa na kanuni hizi na pale
ambapo kanuni hazikutoa mwongozo basi spika atafanya kazi kwa
kuzingatia katiba, sheria nyingine za nchi kanuni nyingine zilizopo,
maamuzi ya awali ya maspika wa mabunge pamoja na mila na desturi za
mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa
Bunge la Tanzania.”
Mbowe hakupewa fursa hiyo.
Kwa utamaduni wa mabunge ya Jumuiya ya Madola ambao unatumiwa na
Bunge letu, Mbowe ni sawa na Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa shughuli
za serikali bungeni. Tofauti yao ni moja tu, kwamba waziri mkuu ana
dola, na yeye hana.
Kwa kuzingatia utamaduni huo, viongozi hawa wanaposimama wakati
wowote, kiti cha spika kitamwomba mbunge anayezungumza aketi chini
kisha mmoja kati yao ambaye atakuwa alisimama atapewa nafasi ya kutoa
hoja yake.
Kanuni ya 74 - (1) ndiyo ilipaswa kutumiwa na Ndugai kumshughulikia Mbowe kama alidharau kiti, lakini pia hakuitumia.
Inasomeka: “Spika anaweza kutaja jina la mbunge kwamba amedharau
mamlaka ya spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge ikiwa: (a) kwa maneno au vitendo, mbunge
huyo anaonyesha dharau kwa mamlaka ya spika; au (b) mbunge huyo
anafanya kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli ya Bunge
au mbunge yeyote anayeongoza shughuli hiyo.
Kama Ndugai angezingatia kanuni za kudumu zinazoliongoza Bunge ili
kudhibiti fujo kama hizo bungeni, alitakiwa kutumia kanuni ya 76 - (1)
badala ya kuwaingiza ukumbini watu wasiopaswa ili kuwadhalilisha baadhi
ya wabunge wa upinzani akiwemo kiongozi wao, Mbowe.
Kanuni hiyo inasema: “Kwa madhumuni ya kudhibiti fujo endapo ikitokea
ndani ya ukumbi wa Bunge na spika ataona kuna haja ya kutumia nguvu,
basi anaweza kuahirisha shughuli za Bunge bila ya hoja yoyote kutolewa
au kusitisha kikao kwa muda atakaoutaja ili fujo hiyo iweze kudhibitiwa
na mpambe wa Bunge.”
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanautafsiri uamuzi wa Ndugai kama
mbinu ovu iliyokuwa imeandaliwa mapema ili kuwasonga wapinzani wasiweze
kuujadili muswada wa sheria wa kurekebisha sheria ya mabadiliko ya
katiba wa mwaka 2013.
Ni wazi kuwa kasoro nyingi zilizopenyezwa katika muswada huo
zisingeweza kuafikiwa na wapinzani ili kuipa nafasi CCM kudhibiti
mchakato wa katiba mpya unaoendelea.
Katika vuta ni kuvute hiyo, wapinzani waliitaka serikali kuuondoa
muswada huo kisha kuufanyia marekebisho, ikiwa ni pamoja na
kuwashirikisha wadau wakiwemo Wazanzibari.
Serikali na kiti cha spika hawakuwa tayari kutekeleza masharti hayo,
hatua iliyoibua mvutano wa kikanuni hadi kufikia wabunge kupiga kura ya
kuamua ama mjadala uendelee au usitishwe.
Kura za wabunge waliotaka mjadala huo uendelee zilikuwa nyingi
kutokana na CCM kuwa na wabunge wengi. Lakini baada ya uamuzi huo,
Mbowe alisimama kuomba ufafanuzi wa kikanuni, akakataliwa.
Licha ya Ndugai kumdhalilisha Mbowe, hakufahamu alitaka kusema nini, hatua iliyoibua hamaki kwa wapinzani.
Mbowe alitaka kuomba kiti kiwatake viongozi wa serikali, Mwanasheria
Mkuu, Jaji Fredrick Werema na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi waweke mezani ushahidi wa
vielelezo vya taarifa walizokuwa wamezitoa.
Kwa mujibu wa Mbowe, taarifa hizo hazikuwa na uthibitisho wa
vielelezo, na kwamba vile vile zilikuwa na upotoshwaji mwingi, lakini
Ndugai hakumpa nafasi hiyo, badala yake alimtaka aketi chini.
Kiongozi huyo, hakuketi bali alisisitiza kuwa ana hoja asikilizwe,
jambo lililomfanya Ndugai kuwaita askari ili wamtoe nje bila kujali
kama wengine hawapaswi kuingia ukumbini wakati Bunge linaendelea kwa
mujibu wa kanuni.
Baada ya askari hao kuitwa na kuingia ndani, wabunge wa upinzani
ukimwondoa Augustino Mrema wa TLP (Vunjo), walimzunguka Mbowe wakipinga
asitoke nje kwa kuzingatia kuwa Ndugai alikuwa amekiuka kanuni.
No comments:
Post a Comment