VIBARUA zaidi ya 30 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA), juzi waligoma kufanya kazi wakidai wapewe ajira ya kudumu kama
alivyopendekeza Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana,
mmoja wa vibarua hao ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, alisema
waliamua kugoma ili kuukumbusha uongozi kuliangalia kwa uzito suala
lao.
Alisema baadhi yao wamefanya kazi kwa muda mrefu bila kupewa ajira,
hivyo wanaamini wakati umefika sasa wa kutekelezwa agizo la Waziri
Mwakyembe bila ya ubaguzi.
Mbali na hilo, alisema pia malipo ya sh 5,000 kwa siku hayatoshi kwa
sababu kazi wanazozifanya za kupakuwa makontena kutoka kwenye meli na
kuyapanga ni ngumu ukilinganisha na kazi kama vile kufagia.
“Tumegoma, shifti nzima ya usiku tuligoma juzi kuamkia jana, kiukweli
hatupendi kufanya hivi, lakini ujue wakati mwingine inatubidi. Japo
Waziri Mwakyembe anatambua umuhimu wetu, lakini wapo wanaochangia
kukwamisha jitihada zake,” alisema.
Akitolea ufafanuzi kitendo hicho, Msemaji wa TPA, Jannet Ruzangi,
alisema ni kweli tukio hilo lilikuwepo na liliwahusisha vibarua
wanaoingia kazini usiku.
“Hata hivyo tulikaa na kujadiliana nao, na kukubaliana kuwa waendelee
na kazi hadi Ijumaa watakapokutana na uongozi wa juu wa TPA kwa pamoja
ili kuzungumzia suala lao,” alisema Jannet.
Wiki iliyopita Dk. Mwakyembe alifanya kikao cha pamoja na wafanyakazi
wa TPA na kuagiza upandishwaji vyeo kwa wafanyakazi na kupatiwa ajira
kwa wale waliofanya kazi kwa muda mrefu huku wakiwa na vigezo.
No comments:
Post a Comment