WAKAZI wa vijiji vitatu katika Halmashauri ya Bagamoyo, Pwani
wameilalamikia halmashauri hiyo kwa kumkumbatia mwekezaji na kuchukua
ardhi huku wakiambulia malipo kidogo.
Wakizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni waliotembelea vijiji
hivyo, wanakijiji hao walimtaja mwekezaji huyo kuwa ni Subash Patel,
ambaye amechukua eneo hilo kwa makubaliano ya kuwalipa sh 700,000 kwa
ekari moja.
Walidai mwekezaji huyo alichukua ardhi yenye ukubwa wa ekari 8,500 atakazotumia kujenga kiwanda cha saruji.
Mtendaji wa Kijiji cha Magulumatala, Masudi Ali, alisema malipo
yaliyotolewa na mwakilishi wa Patel ni kidogo tofauti na makubaliano ya
awali.
“Nimeshuhudia mtu akilipwa sh 12,000, ni kiasi kidogo ukilinganisha na
thamani halisi ya ardhi ilivyo hivi sasa katika maeneo mbalimbali
nchini,” alisema.
Naye Shabani Masudi, alidai mwekezaji huyo amekiuka makubaliano na
inaashiria kuwa kuna dhuluma kutokana na kiasi kidogo kilicholipwa.
“Baadhi ya kasoro tunazolalamikia ni kupunjwa malipo, kupunjwa ukubwa
wa maeneo mbalimbali yaliyofanyiwa tathmini na hata wanakijiji wengine
wameshindwa kuona majina yao,” alisema.
Alivitaja vijiji vilivyoathirika na zoezi hilo ni Mkenge, Tulawanda na Magukumatala.
Akijibu tuhuma hizo, msemaji wa mwekezaji huyo, Meneja Uhusiano na
Mawasiliano wa MMi Steel Ltd, inayotaka kuwekeza katika eneo hilo,
Abubakary Mlawa, alisema hakuna ukweli katika suala hilo bali
halmashauri ndiyo iliyofanya tathmini ya maeneo hayo na wala si
mwekezaji.
Mlawa alisema katika kikao chao na halmashauri, wanavijiji hao
walikubaliana kulipwa sh 400,000 kwa ekari na kulipia mazao
yaliyokuwepo, jambo ambalo limetekelezwa na kampuni hiyo.
“Yaani kama wanadai malipo ni madogo basi watakuwa wamedhulumiana wao
wenyewe na si sisi kama wanavyodai maana hata ukiangalia gharama za eneo
hilo kabla ya mwekezaji kuhitaji walikuwa wakiuza sh 200,000 lakini
waliposikia tunayahitaji ndipo walipotupandishia bei,” alisema.
No comments:
Post a Comment