BENKI ya KCB imesema inatambua changamoto zinazoikabili sekta ya
elimu nchini na kuahidi kuendelea kuwekeza kwa ajili ya kuinua kiwango
cha elimu nchini.
Mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Dk. Edmund Mndolwa, alitoa kauli
hiyo jijini Dar es Salaam jana alipokabidhi madawati 700 katika shule
saba za serikali jijini Dar es Salaam.
Alisema benki yake inatambua matatizo mbalimbali yanayoikabili sekta
ya elimu nchini, hivyo wataendelea kusaidia kulingana na kile
wanachokipata.
“Leo tunahitimisha kampeni ya nunua madwati 10 upate mengine 90 ambayo
imehusisha shule za serikali jijini hapa, sita zikiwa za msingi na moja
ya sekondari, ambayo lengo lake kuu ni kuboresha mazingira ya
elimu,” alisema Mndolwa.
Mkuu wa kitengo cha masoko na mawasiliano wa benki hiyo, Christina
Manyenye, alisema thamani halisi ya madawati yote ni sh milioni 121 na
kwamba KCB ilichangia zaidi ya sh milioni 114 huku shule husika
zikichangia sh milioni saba.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbuyuni, Doreen Malecela, aliishukuru
KCB kwa kuchangia madawati hayo ambayo yataongeza ari ya kusoma shuleni
hapo.
Miongoni mwa shule zilizonufaika na kampeni hiyo iliyodumu kwa mwezi
mmoja ni Mbuyuni, Makumbusho, Sinza, Mkunguni, Msasani B, Hananasif na
Shule ya Sekondari Oysterbay.
No comments:
Post a Comment