MAHAKAMA ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, imemhukumu Mroni Mtwena
mkazi wa Mihingo wilayani hapa, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela
baada ya kupatikana na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa
mahakama hiyo kuwa Safina Simfukwe na Mwendesha Mashitaka Mkaguzi
Msaidizi wa Polisi, Masudi Mohamedi kuwa mnamo Septemba 9 mwaka juzi,
majira ya saa 11 alfajiri huko katika Kijiji cha Mihingo, Wilaya ya
Bunda, mshitakiwa aliiba sh 500,000 na simu aina ya Nokia, yenye thamani
ya sh 40,000, mali ya Wegero Mesere.
Mwendesha mashitaka huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa wakati
anatenda kosa hilo alitumia panga kwa kumkata mlalamikaji kwenye mkono
wake wa kulia.
Alidai kuwa mlalamikaji alimtambua na kupiga yowe na wananchi
walimkamata na kumfikisha polisi ambapo aliandaliwa mashitaka na
kupelekwa mahakamani.
Akitoa hukumu hiyo, hakimu Simfukwe alisema kuwa mahakama hiyo
imeridhika pasipo kuacha shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa
mashitaka, hivyo kumtia hatiani kutumikia kifungo cha miaka 30 na
kuchapwa viboko 24 ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment