WATUHUMIWA saba wa mauaji ya mfanyabiashara wa madini ya
tanzanite, Erasto Msuya (43) wakiwemo wafanyabiashara maarufu wa madini
hayo, Joseph Damas “Chusa” na Sharif Mohamed Athuman wote wakazi wa Jiji
la Arusha jana wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Moshi.
Watuhumiwa hao wote kwa pamoja walifikishwa mahakamni hapo wakiwa
katika gari maalumu la kubeba watuhumiwa majira ya saa 5:30 asubuhi
wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi wenye silaha, wakiwemo wa kikosi
maalumu cha kutuliza ghasia (FFU).
Wakiwa katika chumba cha mahakama kilichowezesha watu wachache kuingia
ndani, mwendesha mashitaka wa serikali, wakili Stella Majaliwa baada ya
kutaja makosa yanayowakabili washitakiwa aliomba kuahirishwa kwa kesi
hiyo kutokana na kutokamilika kwa upelelezi.
Wakili Stella aliieleza mahakama hiyo kuwa washitakiwa hao
walifikishwa mahakamani hapo kutokana na kesi ya mauaji ya kukusudia
kinyume na kanuni namba 16, kifungu cha 196 ya sheria za makosa ya
jinai.
Kutokana na ombi hilo, hakimu mkazi wa mahakama ya hakimu mkazi Simon Kobelo aliridhia na kupanga tarehe nyingine.
Kesi hiyo sasa itatajwa tena Oktoba 15 mwaka huu wakati washitakiwa wote wamerudishwa mahabusu.
Mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Agosti 21, mwaka huu.
Wahitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Shaibu Mpungi, Musa Mangu, Jalila Zuberi, Sadiki Jabiri na Joseph Mwakipasile.
Mfanyabiashara Erasto Msuya aliuawa Agosti 7, mwaka huu majira ya 6:30
mchana kwa kupigwa risasi 13 kifuani, kando ya barabara kuu ya Arusha –
Moshi katika eneo la Mjohoroni, Wilaya ya Hai, karibu na Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
No comments:
Post a Comment