KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida kaburi ambalo alizikwa mtoto
Shabani Maulidi (15), ambaye anadaiwa kufariki dunia miaka mitatu
iliyopita na kuonekana akiwa hai hivi karibuni, jana lilifukuliwa na
viungo vya mwili wake kukutwa ndani.
Kazi hiyo iliyofanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi pamoja na
Mtafiti wa Ofisi ya Mkemia
Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza, Lucas
Ndungulu, ilizua taharuki kwa umati wa watu waliokuwa eneo hilo, baada
ya nyumba ya jirani lilipo kaburi hilo, Masanja Marwa, kubomoka ghafla
wakati ufukuaji huo ukiendelea, huku mwanamke mmoja ambaye hakufahamika
jina lake mara moja naye akianguka na kuzirai.
Kwa sasa mtoto huyo ambaye alionekana hai, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uangalizi wa kitaalamu.
Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Ndungulu alisema
kuwa wameamua kufukua kaburi hilo ili kupata sehemu ya viungo vya mwili
kwa ajili ya vipimo.
“Lengo la kufukua kaburi hili ni kutaka tupate kiungo chochote cha
mwili wa marehemu ili tufanye utafiti wa kitaalamu ili tujue kama ni
kweli huyu anayedaiwa kuwa ni mtoto wao ndiye,” alisema.
Alisema kuwa ufukuaji huo umemalizika na kwamba wamepata baadhi ya
viungo vya mwili wa marehemu na kuchukua baadhi ya mifupa ya mapaja yote
mawili ambayo itapelekwa katika hospitali ya rufaa kwa ajili ya
uchunguzi zaidi.
Kwa mujibu wa Ndugulu, majibu ya vipimo hivyo yatatolewa baada ya wiki
mbili kama hakutakuwa na tatizo lolote la kukatika kwa umeme.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Adamu
Sijaona, alisema kuwa pamoja na kuchukua viungo hivyo, pia watachukua
damu ya wazazi na mtoto mwenyewe.
“Tumechukua pia damu ya mama na baba wa Maulidi mwenyewe ili tukapime
vinasaba (DNA) na kama alivyosema mtafiti, majibu yatatoka baada ya wiki
mbili,” alisema.
Akizungumza baada ya kazi ya ufukuaji kumalizika, baba mzazi wa mtoto
huyo, Maulidi Shabani, alisema kuwa endapo majibu yatakuja tofauti au
vile wanavyokusudia, wapo tayari kuyapokea na kwamba ikigundulika huyo
aliyeonekana ni Maulidi, pia watampokea na kuendelea kumtunza.
“Lakini nina imani kuwa huyu aliyeonekana ni mwanangu Maulidi kabisa, kwa sababu anazo alama zote,” alisema mzazi huyo.
Mtoto Maulidi aliyefariki dunia miaka mitatu iliyopita na kufanyiwa
matanga, alionekana akiwa hai baada ya kukutana na mama yake ana kwa ana
mapema wiki hii asubuhi wakati akienda kwenye shughuli zake za
biashara.
Ilidaiwa na wazazi wake kuwa Maulidi alitoweka ghafla na kushindwa
kurudi nyumbani kwao Januari mosi 2011, wakati alipokuwa amewapeleka
mbuzi malishoni na mwili wake kuonekana baada ya siku tatu akiwa amefia
kwenye kisima cha maji.
Kwa mujibu wa baba yake, Maulidi hakurudi nyumbani siku hiyo, ambapo
waliendelea kumtafuta bila mafanikio na ndipo baada ya siku tatu
walimkuta akiwa amefia ndani ya kisima cha maji kilicho maeneo ya Kijiji
cha Nyankumbu, Kitongoji cha Mwembeni.
Tukio hili ni la tatu kutokea mkoani hapa ambapo wilayani Kasamwa,
mwanamke aliyefariki dunia miaka mitano iliyopita alionekana hai na
kutambuliwa na ndugu yake. Tukio la pili lilitokea Wilaya ya Chato,
wakati kijana aliyefariki dunia miaka miwili iliyopita alionekana akiwa
hai.
CREDIT TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment