WAKATI uongozi wa gazeti la Mwananchi ukifichua kile kilichojiri
hadi kufungiwa na serikali kwa muda wa wiki mbili, Jukwaa la Wahariri
Nchini (TEF), limekutana na kulaani hatua hiyo ya serikali kutumia
Sheria kandamizi ya Magazeti ya Mwaka 1976 kufungia magazeti.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi
Communications Ltd (MCL), Tido Mhando, kwa vyombo vya habari jana, Julai
17, mwaka huu, Mwananchi lilidaiwa kuchapisha habari iliyohusu
mishahara mipya ya watumishi wa serikali ambayo ilidaiwa kuwa ni siri,
haikutakiwa kutangazwa kwenye vyombo vya habari.
Mhando alisema hata hivyo habari hiyo haikuchapishwa kwenye Mwananchi
Julai 17 kama taarifa ya Maelezo ilivyodai bali Julai 27 mwaka huu.
Alisema kuwa Agosti 17 mwaka huu, Mwananchi lilichapisha habari yenye
kichwa cha habari ‘Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali wa polisi’
ikisindikizwa na picha ya mbwa wa polisi, ambayo Maelezo waliitafsiri
kuwa ni kuchochea chuki na uadui kwa waumini wa dini hiyo na serikali.
Alifafanua kuwa habari iliyohusu mishahara, gazeti hilo lilitoa
taarifa hiyo baada ya kupata taarifa kutoka serikalini kuhusu mishahara
mipya ya serikali.
“Hii ilikuwa ni wiki mbili baada ya serikali kuchapisha matangazo ya
mishahara ya sekta binafsi kupitia magazeti kadhaa, kutangaza ongezeko
la mshahara bungeni,” alisema.
Mhando aliongeza kuwa gazeti hilo lilichapisha habari hiyo kwa nia
nzuri, kuonyesha kuwa ahadi zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa
serikali, ikiwa ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete, kuwa mishahara ya
wafanyakazi wote nchini itaongezwa, zilikuwa zimetimizwa.
Akizungumzia habari ya pili, Mhando alisema kuwa tofauti na taarifa
iliyotolewa na Maelezo, hakuna sehemu yoyote katika habari ile iliyosema
Jeshi la Polisi lilipeleka mbwa misikitini.
Pia alisema Msajili wa Magazeti aliuandikia uongozi wa gazeti la
Mwananchi barua mbili kwa nyakati tofauti kuutaka utoe maelezo na kwamba
uongozi wa MCL ulizijibu na kutoa ufafanuzi wa kina lakini hazikujibiwa
hadi Septemba 28, Maelezo ilipotangaza kulifungia gazeti hilo.
“Kwa ujumla MCL imesikitishwa na uamuzi wa Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo kuchukua hatua kali kiasi hicho licha ya kampuni
hii kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu ilipotakiwa kufanya hivyo, kwa
kutoa ufafanuzi wa kweli juu ya habari hizo kwa wakati muafaka,”
alisema.
Wahariri wang’aka
Wakati MCL wakieleza hayo, Jukwaa la Wahariri (TEF) lilikutana jana
na kujadili uamuzi wa serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania yaliyofungiwa kwa madai ya uchochezi.
Kwa mujibu wa Katibu wa TEF, Neville Meena, baada ya mjadala wa kina,
wajumbe wameazimia kuupinga uamuzi wa serikali dhidi ya magazeti hayo
kwa sababu adhabu hiyo imetolewa kwa kutumia sheria kandamizi ya
magazeti ya mwaka 1976, ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wadau kwa miaka
mingi sasa.
“Hii ni moja ya sheria ambazo Tume ya Jaji Francis Nyalali
ilipendekeza zifutwe, kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kukiuka misingi ya
haki za binadamu, utawala bora na kwenda kinyume cha Katiba ya nchi
pamoja na maazimio ya kimataifa ya haki za binadamu,” alisema.
Meena alisema kuwa TEF inaungana na taasisi nyingine kupinga adhabu
hiyo kwa magazeti ya Mwananchi, Mtanzania na wakati huohuo wakikumbushia
kifungo cha gazeti la MwanaHALISI, kwa sababu sheria iliyotumika
haifai.
“Utaratibu uliotumiwa na serikali kwa kujigeuza kuwa mlalamikaji,
mwendesha mashtaka na mtoa adhabu, kamwe haukubaliki katika jamii yoyote
iliyostaarabika, kwa sababu ni kinyume cha utaratibu wa kutoa haki ya
asili (natural justice).
“Hili si jambo la kuendelea kufumbiwa macho na jamii ambayo inafuata misingi ya kidemokrasia na utawala bora.
“Hivyo, tunalaani kwa nguvu hatua hizi zilizochukuliwa, kwa kukiuka
misingi hii yote, hasa ukizingatia kuwa ni serikali hii ambayo imesaini
makubaliano ya kimataifa kuhusu uwazi katika uendeshaji wa serikali,”
alisema.
Kuhusu hatua za kuchukua, TEF ilisema kuwa inafahamu kuwa kuna kesi ya
kuipinga Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, ambayo ilifunguliwa mwaka
2009. Kwamba, ni jambo la bahati mbaya na kusikitisha sana kuwa hadi
hivi sasa miaka minne baadaye bado kesi hiyo haijaanza kusikilizwa, kwa
sababu haijapangiwa majaji.
“Jukwaa la Wahariri linapenda kutoa wito kwa mhimili wa Mahakama
kurekebisha kasoro hii kwa kupanga majaji kwa ajili ya kuisikiliza.
Kufanya hivi kutahakikisha si tu haki kutendeka, bali pia haki kuonekana
inatendeka,” alisema Meena na kuongeza kuwa wanatoa wito kwa serikali
kuyafungulia magazeti hayo.
No comments:
Post a Comment