WAKAZI wa zamani wa Magomeni Kota wameionya Manispaa ya
Kinondoni, kuhakikisha inawalipa fedha zao za pango kama mkataba ulivyo,
vinginevyo watazua vurugu kubwa.
Onyo hilo linafuatia kuwapo kwa sintofahau kuhusu malipo hayo, huku
mmoja wa watendaji wa manispaa hiyo (jina limehifadhiwa) akikiri kuwa
hakuna uwezekano wa kufanyika malipo hayo.
Ofisa huyo alisema viongozi wa manispaa waliosaini mkataba wa malipo
hayo, wakazi hao waliwadanganya, kwa kuwa jambo hilo haliwezi
kutekelezwa kwa kuwa ni kuvunja sheria.
Alisema kuwa viongozi wa juu wa manispaa hiyo wana hofu kufanya malipo
hayo ya sh 695,520,000 ikiwa ni pango la kodi kwa wakazi hao
linaloanzia Januari hadi Desemba mwaka huu kutokana na uwezekano wa
kuingia katika kashfa, kwa kuwa sheria haikuzingatiwa tangu awali.
“Hapa ninapokuambia viongozi wote wana hofu ya kutoa fedha hizo,
ingawa mkataba unaonesha kusainiwa na baadhi ya viongozi wa manispaa
lakini wanajua wazi ukaguzi wa
Mdhibiti na Makaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) ukifanywa kuna utata utajitokeza iwapo fedha hizo
zitatumika,” alisema.
Alisema kuwa hofu hiyo ndiyo iliyosababisha baraza la madiwani na
baadhi ya viongozi wa juu kuzuia malipo hayo kufanyika ingawa
wanashindwa kuwaeleza ukweli wakazi hao.
Alisema kuwa ni kitendo cha ajabu wanasiasa wa manispaa hiyo
walivyowadanganya wananchi hao kwa kuwa hakuna fedha ya walipa kodi
inayotolewa pasipo kufanyiwa kazi.
Akizungumzia juu ya malipo hayo, kiongozi wa kamati ya wakazi hao,
Abbas Mkweta, alisema kuwa hadi sasa hawajapata taarifa rasmi za lini
manispaa hiyo italipa malipo hayo.
Mkweta alisema kuwa wanategemea kati ya siku hizi mbili wapewe fedha
hizo kwa kuwa uhakiki umefanyika kwa kiasi kikubwa na zilizobaki ni
nyumba 15 tu.
“Sisi tunaamini tutalipwa fedha hizo lakini hadi sasa manispaa
haijatueleza watatulipa lini ila tunawaomba wakazi wa Magomeni wawe na
subira, najua kati ya siku hizi mbili ni lazima watupe taarifa za
uhakika,” alisema.
Aidha, mmoja wa wakazi hao ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema
kuwa wanaona kama mchezo wa kuigiza unaoendelea maana baadhi yao
wametoka mbali kufuatilia malipo hayo huku wakiwa wamekopa nauli.
Mkazi huyo alisema kuwa manispaa ni lazima ithamini mkataba huo la
sivyo wakazi hao watalazimika kutafuta mahema na kuja kufunga katika
viwanja hivyo kutokana na wamiliki wa nyumba walizopanga kuwadai kodi ya
mwaka mzima.
“Hivi ninavyokwambia wamiliki tulikopanga tumewadanganya hadi
tumechoka na sasa imefika mahali wanataka hela zao, sasa kama manispaa
inataka vurugu wajaribu kutufanyia jambo hilo la kugoma kutulipa hizo
fedha,” alisema.
Halmashauri hiyo iliingia mkataba na wakazi hao Septemba mwaka 2011
katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi ambapo ilikubali kuwalipia pango
la chumba wakazi hao kuanzia mwaka huu hadi pale nyumba za eneo hilo
zitakapokamilika.
Nyumba za Magomeni Kota zilijengwa na Jiji la Dar es Salaam miaka ya
1950 na baadaye kumilikishwa kwa halmashauri ya manispaa hiyo.
Nyumba hizo zilipangishwa kwa mkataba kwa wakazi hadi mwaka 2006.
Wakazi hao 644 waliendelea kukaa hapo hadi mwaka 2009 ambapo walitakiwa
kuondolewa na wakakimbilia mahakamani.CHANZO CHA HABARI NI TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment