TAARIFA zaidi za kusikitisha kuhusu
mauaji ya kinyama, yaliyofanyika katika familia ya Mtangazaji wa Kituo
cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro zimeendelea kutolewa, ambapo
imebainika mama mzazi wa mtangazaji huyo, Anastazia Saro (58), aliuawa
kwa kupigwa risasi tano.
Msemaji wa familia hiyo, Idd Lema
alisema hayo jana wakati wa ibada ya kumuaga Anastazia, iliyofanyika
katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa
Kibwegere, Dar es Salaam.
Awali, taarifa zilizokuwepo, zilidai
Anastazia alipigwa risasi mbili kifuani, lakini Lema alisema baada ya
uchunguzi wa mwili huo uliofanywa na Polisi, ilibainika kuwa alipigwa
risasi tano na si mbili.
Akizungumza wakati wa ibada ya kumuaga
Anastazia, ambayo mwanawe wa pekee Ufoo hakuweza kuhudhuria, Mwinjilisti
wa Kanisa hilo, Margaret Shekoloa alisema Anastazia atakumbukwa kwa
mambo mengi, aliyoyafanya katika Kanisa hilo katika nafasi mbalimbali
alizokuwa nazo ukiacha ya muumini.
Alisema siku moja kabla ya kifo chake,
Anastazia alikwenda kanisani na kupanda maua katika bustani ya kanisa na
kupamba madhabahu.
“Alipomaliza kupamba madhabau pamoja na
kupanda maua katika bustani, aliniaga na kuniambia mchungaji tutaonana
katika ibada ya kesho bila kujua kuwa siku hiyo hataiona,” alisema
Mwinjilisti Shekoloa.
Alisema matukio ya ukatili, kwa sasa
yamezidi kuongezeka nchini na chanzo chake ni watu kutokuwa karibu na
Mungu wao. Alisema matukio hayo, yanayowagusa watu wengi wasio na hatia,
pia yamekuwa yakichangia uvunjifu wa amani.
“Anastazia alikuwa na malengo makubwa na
Kanisa hili, aliwaunganisha wanawake wote kwa kuwapa mafunzo ya
ujasiriamali,” alisema Shekoloa.
Alisema hata pale alipohitajika na
kanisa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana, aliitikia
mwito bila tatizo lolote.
Ibada ya kuaga mwili huo ilimalizika saa
11.30 jioni na mwili huo kusafirishwa kwenda kijiji cha Shali, Machame
mkoani Kilimanjaro.
Source: HabariLeo
No comments:
Post a Comment