MBUNGE wa Viti Maalumu, Suzana Lyimo (CHADEMA), amesema
usimamizi na uendeshaji mbovu wa shule katika ngazi zote ni chanzo cha
matokeo yasiyoridhisha ya elimu nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Lyimo katika mahafali ya tano ya darasa la
saba katika shule ya msingi Ndalala, Mwenyekiti wa M4C Jimbo la Ukonga,
Nixon Tugara, alisema ili kuhakikisha taifa linakuwa lenye ustawi ni
lazima usimamizi na uendeshaji wa taasisi za elimu katika ngazi zote
unafanyika kwa ufanisi.
Alisema elimu kwa Watanzania ni muhimu hasa katika mbio za kupambana na maadui ujinga, maradhi na umaskini.
“Silaha pekee ya kuwashinda maadui hawa ni elimu bora, maana elimu
kama inavyobainishwa na sera ya elimu na mafunzo ni mchakato ambao mtu
hupata maarifa na ujuzi wa kujitambua na kujiweka sawa katika kupambana
na mazingira na mabadiliko ya mara kwa mara ya kijamii, kisiasa na
kiuchumi,” alisema.
Tugara aliwaasa wahitimu hao 53 wajipange kukabiliana na mipango ya
kuhujumiwa kwa Katiba mpya na kudai kuwa hapo ndipo penye nia ya kupata
haki za kielimu zilizokosekana kwa miaka 52 ya uhuru wa Tanganyika.
Mwalimu wa shule hiyo, Mariam Omary, akisoma risala ya shule, alisema
shule hiyo inakabiliwa na ukosefu wa maji, uzio na kompyuta kwa ajili
ya somo la Tehama.
Habari na Zawadi Chogogwe.
No comments:
Post a Comment