RAIS Jakaya Kikwete leo anakutana Ikulu na viongozi wa vyama vya
CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kwa ajili ya mazungumzo ya kuboresha
kasoro zilizojitokeza kwenye muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria
ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.
Hatua hiyo inatokana na msimamo wa wabunge wa vyama hivyo kususia
mjadala wa muswada huo uliopitishwa hivi karibuni na wabunge wachache wa
CCM na Augustine Mrema wa TLP, wakidai umechakachuliwa, huku Zanzibar
ikiwa haijashirikishwa.
Kufuatia kusigana huko, viongozi wa vyama hivyo; Freeman Mbowe
(CHADEMA), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi),
walikutana na makundi mbalimbali ya wadau na kutangaza kufanya mikutano
na maandamano nchi nzima kupinga rais asisaini muswada huo.
Uamuzi wa wapinzani hao uliwaibua mawaziri kadhaa, Stephen Wassira
(Ofisi ya Rais-Mahusiano na Uratibu), William Lukuvi (Sera, Uratibu na
Bunge), Mathias Chikawe (Katiba na Sheria) na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Frederick Werema wakiwabeza.
Mawaziri hao walidai wapinzani wanapoteza muda wa mchakato ili rais
awaite Ikulu tena kwa mazungumzo waweze kunywa chai na juisi, jambo
walilosisitiza kuwa haliwezekani, kwani milango hiyo imefungwa.
Hata Waziri Chikawe alifikia hatua ya kumtisha Rais Kikwete, akisema
kuwa asipousaini muswada huo atakuwa ametangaza mgogoro na Bunge, kwani
lilifanya kazi yake kwa kufuata Katiba.
Rais Kikwete alitilia maanani hoja za pande zote na kuamua kuwaita
wapinzani mezani kuzungumza nao, akisema kuwa kama dhamira yao ni kutaka
kupata Katiba mpya, anawashauri waachane na mipango ya maandamano na
kufanya ghasia, bali watumie njia halali, kwamba serikali iko tayari
kuwasikiliza.
Hoja zinazovutaniwa
Mbali na mambo mengine, wapinzani wanadai kuwa muswada huo
ulichomekwa baadhi ya vipengele ambavyo vingeisaidia CCM kutawala
mchakato mzima wa katiba.
Katika hoja ya mapendekezo ya kumpa rais mamlaka ya kuteua wajumbe wa
Bunge Maalumu, wapinzani hao wanasema hayakubaliki, kwamba yanarudisha
dhana kwamba wajumbe hawa watakuwa watu wa rais ambaye pia ni Mwenyekiti
wa CCM.
“Sheria iweke wazi kwamba wajumbe hawa ‘watateuliwa’ na taasisi
zilizotajwa. Hii itaondoa utata juu ya uwakilishi wao na juu ya mamlaka
yao ya uteuzi.
“Sheria itaje kwamba idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu watakaotokana
na kila taasisi iliyoorodheshwa katika kifungu cha 22(1)(c) itakuwa
354,” walisema wapinzani.
Katika suala la Zanzibar, wapinzani hao wanasema wananchi wa huko
hawakushirikishwa wakati wa uandaaji wa muswada huo, hivyo kutaka mambo
kadhaa yafanyike ili kuondoa mgongano.
Kwamba, ili kutimiza matakwa haya ya sheria na kwa kuzingatia
mapendekezo ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume, Bunge linahitaji
kuangalia upya suala la uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalumu.
Kwa mujibu wa kifungu cha 22(2) cha Sheria, idadi ya wajumbe wa
Zanzibar katika Bunge Maalumu watakaotokana na makundi yaliyoainishwa
katika kifungu cha 22(1)(c) “... haitapungua theluthi moja ya wajumbe
hao.”
Hii ina maana kwamba, kwa uchache kabisa, wajumbe hao wa Zanzibar hawatapungua 55.
Rasimu ya Katiba itakayojadiliwa na Bunge Maalumu inahusu Katiba ya
Jamhuri ya Muungano peke yake. Rasimu hiyo imependekeza kwamba masuala
yote yasiyo ya Muungano, ya washirika wa Muungano, yaani Tanzania Bara
na Zanzibar, yashughulikiwe na Katiba za washirika hao.
Rais Kikwete katika kutambua hoja za wapinzani aliomba hekima
ziwaongoze viongozi wa pande zote ili waweze kutumia utaratibu
walioutumia mwaka 2012.
“Kulipotokea mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na
kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na
kifanyike vipi. Baada ya kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na
kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo,” alisema rais.
Aliongeza kuwa kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo
huu na kutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa hawatengenezi katiba ya chama fulani
bali katiba ya nchi, katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama
ambao ndio wengi kuliko wote.
Kuhusu ushiriki wa Zanzibar, alisema kuwa alielezwa ni kwa kiasi gani
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilivyoshirikishwa na kutoa maoni yake
yaliyojumuishwa katika muswada.
“Kama ni hivyo, nashauri kuwa suala hili lirudishwe bungeni ili
wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo watu
wataendelea kulaumiana isivyostahili,” alisema.
Suala la Tume ya Mabadiliko ya Katiba nalo litakuwa sehemu ya mjadala
huo, licha ya Rais Kikwete naye kuona umuhimu wake akitaka ihusike
kwenye hatua ya Bunge Maalumu.
“Nimeulizia ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na
mapendekezo ya serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala.
Limetokana na pendekezo la mbunge katika Bunge wakati wa
kupitia vifungu na kuungwa mkono na wabunge wengi.
“Nami naiona hoja ya wajumbe wa tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge
Maalumu, hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya tume,” alisema.
CREDIT TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment