WATOTO wa marehemu Mohamed Stima, wamemwomba Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kuwasaidia kupata
nyumba yao ambayo wamedhulumiwa na mfanyabiashara mmoja wa Tunduma.
Akizungumza mmoja wa watoto hao, Zaituni
Mohamed (19), alisema kuwa anaiomba serikali kupitia wizara husika
kuwasaidia kuwapatia nyumba yao ambayo waliachiwa urithi na wazazi wao
walipofariki dunia.
Zaituni alisema kuwa baba yao, Mohamed Stima, wakati wa uhai wake
alikuwa amejenga nyumba yake katika maeneo ya Kitongoji cha Majengo B,
nyumba hiyo ilikuwa ikiwapa kipato, ikiwa ni pamoja na karo za shule.
Alibainisha kuwa nyumba yao ambayo ipo kwenye kiwanja Na. 64, kitalu G
waliachiwa na baba yao marehemu kama sehemu ya urithi, lakini cha
kushangaza walijitokeza watu na kuwafukuza katika nyumba hiyo, kwa madai
kuwa si mali ya baba yao, na kwakuwa ni wadogo wameshindwa la kufanya
hadi sasa.
Kwa upande wa mzee Winston Mwansumbi (62), ambaye hapo awali alikuwa
mwenyekiti wa Kitongoji cha Majengo B na msimanizi wa nyumba ya watoto
hao, alisema kuwa uongozi unajua wazi kuwa mali hiyo ilikuwa mali ya
Mohamed Stima, alipokufa aliwaachia watoto.
“Huyu mtu ambaye alikuja hapa na kuvamia eneo la watoto na kuwavunjia
nyumba yao hatumjui kijiji kizima, tunamshangaa, lakini inaonekana
anatumia fedha nyingi kuwanyanyasa watoto hao ambao kwa sasa wanaishi
maisha ya shida sana,” alisema Mwansumbi.
Aliiomba serikali kuwapatia msaada watoto hao ambao kwa sasa ni
yatima, wanaishi maisha ya shida na wamefikia hatua ya kuwa ombaomba na
wengine kushindwa kuendelea na masomo yao, jambo ambalo ni hatari, hasa
kwa watoto wa kike, kwa kuwa wanaweza kujiingiza katika vitendo viovu.
No comments:
Post a Comment