OPERESHENI Kimbunga imeondoa kijiji haramu cha Nyamugali
kilichokuwa chini ya wahamiaji haramu kutoka nchi ya Burundi katika
Wilaya ya Kasulu, Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Dan Makanga alisema hayo jana wakati akisoma
taarifa ya maendeleo ya Wilaya mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Alisema ndani ya kijiji hicho haramu pia walikuwemo wahamiaji haramu waliokuwa na dola yao hapa nchini.
Makanga alisema lugha iliyokuwa ikitumika ndani ya kijiji hicho ni
Kirundi na Kifaransa na hata shule zilikuwa zikifundishwa kwa lugha hizo
kwa kufuata mitaala ya Burundi.
Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Wilaya, alisema mbali ya kufanya hayo yote wakiwa nchini
hapa, wahamiaji hao pia walikuwa wakipeperusha bendera ya nchi yao
katika maeneo mbalimbali ya kijiji.
“Haiwezekani watu ni wahamiaji haramu halafu hata pesa wanatumia ya
kwao ndani ya nchi nyingine… kupitia operesheni hii kimbunga imesafisha
hayo yote na wahamiaji hao wamekimbia makazi yao kwani walikuwa
wamejenga na kuishi watakavyo,” alisema Makanga.
Inakadiriwa takribani wahamiaji haramu 600 katika kijiji hicho wamekimbia baada kufanyika operesheni kimbunga.
Alisema zoezi hilo linakwenda vizuri na wamefanikiwa kukamata silaha
mbalimbali japo kuna changamoto kwa baadhi ya watu kutotoa ushirikiano
kwa vikosi vya ulinzi na usalama vinavyosimamia operesheni hiyo.
Waziri Mkuu Pinda alisema lengo la serikali kupitisha Operesheni
Kimbunga ni kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu na kuifanya
Tanzania kuwa mahali pa usalama.
Pinda alivipongeza vikosi vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri
wanayofanya ya kuondoa wahamiaji haramu nchini, na kwamba changamoto
zilizojitokeza wakati wa zoezi hilo zinafanyiwa kazi, hasa malalamiko ya
baadhi ya watu kuwa walionewa.
Operesheni hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete
alilolitoa Julai 29 mwaka huu akiwa katika ziara ya kikazi mkoani
Kagera.
No comments:
Post a Comment