MIKOA sita imeomba kuandaa Tamasha la Krismasi litakalofanyika Desemba 25 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana
na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama,
wamepokea maombi kutoka kwa wadau mbalimbali wa muziki wa Injili nchini
wakiomba lifanyike katika mikoa yao.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Mbeya, Mwanza, Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Shinyanga.
“Tunachofanya kwenye kamati yangu ni kupokea maoni kwa njia
mbalimbali ikiwemo simu za mikononi kutoka kwa wadau wetu kwamba wapi
wanataka tamasha lifanyike.
“Kwa kipindi cha wiki moja tumepokea maombi mengi kutoka kwenye mikoa
hiyo na kesho (leo), ndiyo siku ya mwisho tuliyoweka kwa ajili ya
kupokea maombi, baada ya hapo tutatangaza mkoa gani utakuwa wa kwanza,”
alisema Msama na kuongeza: “Lakini si kupendekezwa tu na wadau ndiyo
kigezo cha kupewa nafasi, lazima tuangalie na mazingira ya mkoa husika
katika mambo ya matamasha,” alisisitiza Msama.
Tamasha la Krismasi linaandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ya
jijini Dar es Salaam, ambayo pia huandaa Tamasha la Pasaka kila mwaka.
Kwa mujibu wa Msama wanataka Tamasha la Krismasi liwe bora zaidi
kuliko la Pasaka kwa kualika wasanii maarufu kutoka nje na ndani ya
Tanzania.
Alisema hilo litakuwa tamasha kubwa la nyimbo za kumsifu Mungu na
litakuwa na tofauti kubwa kulinganisha na matamasha mengine yaliyowahi
kuandaliwa na kampuni yake.
No comments:
Post a Comment