“Subiri wakirudi jioni.”
“Wewe utakuwepo?”
Nililishangaa swali hilo, hakuwa akinidai mimi lakini anataka
niwepo?
“Unataka niwepo?”
“Ee.”
“Kwanini?”
“Naamini utanisaidia kuzipata fedha zangu.”
“Uliwahi kuja wakagoma kukupa?”
“Siyo hivyo, ila kila nikija, nikigonga mlango huwa hawafungui.”
“Basi nitakuwepo.”
“Asante kaka. Nije saa ngapi?”
“Saa moja nitakuwa nimerudi.”
Aligeuza mkokoteni na kuondoka zake huku akisema:
“Muda huo nitakuwa nimefika kaka.”
Niliondoka kwenda kazini kuomba ruksa. Lakini wakati naondoka,
mfanyakazi mwenzangu mmoja aliniuliza nakwena wapi, nikaamua kumsimulia kwa
ufupi kisa changu.
“Khaa! Sasa hapo tatizo liko wapi, mbona dawa ipo rahisi sana.”
“Rahisi! Ni ipi hiyo?”
“Sikia, twende pembeni nikakusimulie,” aliniambia yule mfanyakazi
mwenzangu huku akiangalia kulia na kushoto kama mabosi watatokea.
Tulikwenda kusimama pembeni, akaanza kuniambia:
“Sikiliza, kama unaishi nyumba ya namna hiyo, unachotakiwa, kila
siku asubuhi na jioni au usiku unapuliza bangi ndani ya nyumba, kama ni majini,
mapepo sijui nini, utaona mambo poa kabisa.”
Sikuamini maneno hayo, nikamuuliza mara mbilimbili kama ni kweli.
“Khaa! Nina mjomba angu aliwahi kuishi kwenye nyumba ya hivyo,
akaenda sehemu akaelekezwa dawa ni hiyo, akaitumia, mpaka sasa anaishi kwa raha
hakuna cha majini wala mapepo,” alisema.
Nilimsikiliza nikianza kuamini kwa mbali, lakini nilifika mahali
nikamuuliza hiyo bangi mimi nitavuta au nitaiwasha ili itoe moshi yenyewe?
“Ukishaiwasha, utaiweka mezani au popote ndani kwako, lakini
angalia isizimike ili moshi wake usambae chumba kizima au sebule nzima.”
“Hilo linawezekana,” nilimwambia nikimtumbulia macho.
Kwa sababu nilikuwa nimeshaaga, ilibidi niondoke tu na kurudi
baadaye. Nilikwenda mtaani, nilitafuta bangi nikapata maeneo ya Kariakoo,
nikaitia mfukoni.
Nilizurura sana siku hiyo, saa tisa kamili nilikuwa njiani narudi
kazini. Nilipiga hesabu za kufika kazini na kuondoka, maana muda wa kazi ni saa
tisa na nusu.
Wakati napita pale Kituo cha Polisi Msimbazi, fujo zikazuka, kuna
machinga wawili walikuwa wanapigana kwa sababu ya kugombea sehemu ya kufanyia
biashara, katika ugomvi huo mimi nilibaini mmoja wao ndiyo mwenye kosa.
Nikampa laivu kuwa yeye ndiye mwenye tatizo, alikuja juu,
akachukua boksi lenye viatu na kunirushia, likanipata kwenye bega la kulia,
sikukubali, nikaokota jiwe na kumrushia, likampata mkononi.
Polisi walifika haraka sana, wakanikamata mimi, yeye na yule
machinga niliyeona anaonewa, tukapelekwa Msimbazi polisi
Tulipofika pale, afande aliyetukamata alituamuru kuvua viatu,
mikanda, simu kuweka pembeni. Halafu mmoja alianza kutusachi mifukoni. Wakati
tendo hilo linaanza kwa wenzangu, ndipo nikakumbuka mimi mfukoni nina vipisi
viwili vya bangi.
Nilitaka kutoka mbio kituoni hapo, lakini sehemu tuliyokaa,
ningesema nitoke, nisingefika nje au hata kama ningefika ningekamatwa au kupigwa
risasi kama mhalifu, nilitetemeka, mwili uliisha nguvu.
Alipofika kwenye zamu yangu, yeye mwenyewe alishangaa kuniona
nachezesha miguu kama niliyebanwa na haja ndogo, akaniuliza:
“We vipi, unaumwa?”
Nikamjibu naumwa afande.
“Unaumwa nini?”
“Sijui, nadhani homa.”
Hakunijibu, alianza kwa kutumbukiza mkono kwenye mfuko usiokuwa na
kitu, akahamia wa nyuma ambao una waleti, akapeleka wa kulia kwangu ambao ndiyo
wenye bangi, aliposhika, akakunja sura, alipotoa akashtuka sana na kusema:
“Haa! Hii bangi siyo?”
Sikumjibu kwani niliamini ameshaijua, wenzake waliokuwa kaunta
wakaacha mambo yao na kunigeukia mimi, nao wakashangaa sana. Mmoja alikuwa
amekaa juu ya stuli, akashuka huku akiniangalia kwa kunikazia macho.
“Unakuja kituo cha polisi na bangi, wewe unatutafuta nini sisi?”
aliuliza yule aliyeshuka kwenye stuli.
Niliambiwa nafunguliwa kesi ya pili, ya kwanza kupigana na
kujeruhi ya pili kukutwa na bangi!
Nilijitetea nikisema bangi ile si kwa ajili ya kuvuta bali
nilikuwa nina shida nayo.
“Wewe usitufanye sisi watoto wadogo, tunamijua nyie raia,” alisema
yule afande aliyenisachi.
Lakini afande mmoja wa kike ambaye muda wote alikuwa akiangalia
tu, akawaambia wenzake:
“Lakini huyu kaka mbona hafanani na kuvuta bangi, muulizeni ana
shida nayo gani?”
Wale wenzake wakanigeukia na kuniuliza:
“Haya, wewe mwananchi, raia kabisa, unaweza kuwa na shida gani na
bangi mbali na kuvuta?”
Niliwasimulia kila kitu, tena nilifika mahali nikawaambia kama
kuna asiyeamini, tuongozane hadi nyumbani, Magomeni akaone maajabu ambayo hayahitaji
kuelekezwa sana ili kuamini kama yapo au la!
Palipita ukimya wa sekunde kadhaa, mmoja wao akaniuliza:
“Kama ni kweli au tufanye ni kweli, ni kwanini umemuumiza huyu?”
Nilisema kilichotokea, yule chinga niliyemsaidia naye akanitetea
kwa kusema hivyohivyo, lakini afande mmoja akasema nilijichukulia sheria
mkononi ambapo ni kosa kisheria.
Niliomba sana wanisamehe kwa yote, nikasingizia kwamba ni kwa
sababu kichwa changu hakipo sawa kwa kuishi nyumba moja na majini.
Namshukuru mmoja wao aliniambia niondoke lakini nihakikishe
situmii bangi katika kujitibu kwani serikali haiamini kama bangi ni dawa.
Nilipotoka, nilikwenda kuinunua nyingine, lakini akili iliingia
hisia kwamba, huenda yule dada wa ajabu mle ndani ndiye anayecheza michezo ili
kunikwamisha kwenda na bangi ndani ya nyumba, nikasema moyoni ngoja ninunue hii
nione kitakachotokea, nikanunua tena misokoto miwili.
Nilitembea kuelekea kituo cha daladala. Njiani nilimpigia simu
yule mfanyakazi mwenzangu aliyenijulisha kuhusu dawa ya kutibu nyumba yenye
majini, nikamwambia sitaweza kurudi kwani nilipata wakati mgumu kidogo njiani.
Alinielewa, akaniuliza kama nimepata, nikamjibu kila kitu
kimekwenda sawa, lakini sikumwambia kuhusu timbwili lililojitokeza.
Nilipanda daladala nikashuka Magomeni, niliingia ATM kutoa fedha
kidogo, kisha nikatoka. Wakati natafuta mwelekeo wa kwenda nyumbani,
nilimkumbuka dalali, nikampigia simu.
“Halo.”
“Halo habari za kazi bwana?”
“Nzuri, pole na kazi na wewe mwenzangu?”
“Nimepoa. Bwana vipi kuhusu nyumba?” nilimuuliza.
“Nyumba imefanyaje?”
“Si nilikusimulia matatizo yake, umesahau?”
“Kwani ulisema matatizo yake yakoje vile?”
Nilimwelezea kwa kirefu, nikafika mahali nikamwambie hadi
nilivyompigia simu halafu ikapokelewa na sauti ya ajabuajabu, alicheka sana.
“Wewe bwana acha kunichekesha.
“Kwanini unasema hivyo?”
“Yaani simu yangu mimi halafu apokee mtu mwenye sauti ya
ajabuajabu, kwanini sasa?”
“Mimi pia sijui.”
“We ulikosea namba.”
“Labda bwanam siwezi kukazania sana,” nilimjibu kwa kinyongo kwani
namba yake niliisevu na ninapompigia huwa nasachi jina tu, sasa nilikosea
kivipi?
“Enhe, unasemaje bwana?” aliniuliza.
“Nimeshakwambia bwana.”
“Kwa hiyo unashauri nini?”
“Nataka pesa zangu nikapange kwingine.”
“Da! Hilo halitawezekana kirahisi bwana, maana mpaka nimpate
mpangaji mwingine atoe fedha ndipo nikulipe wewe na mpangaji atakayekuwa tayari
kutoa fedha lazima akute nyumba tupu, sasa wewe utalikubali hilo?”
“Naweza kulikubali, ila tuandikishiane.”
“Kwamba?”
“Kwamba unajikomiti nikiondoka, akiingia mpangaji mwingine tu
unanilipa pesa zangu.”
“Ngoja nitakupigia,” alisema dalali na kukata simu.
Nilipokuwa nakaribia nyumbani, nikakutana na yule msukuma
mkokoteni wa maji.
“Kaka za kazi?”
“Nzuri, vipi wewe?”
“Niko sawa, ndiyo unarudi?”
“Ndiyo.”
“Najua jamaa hawajarudi, nitakuja muda uleule tuliopanga.”
“Sawa, karibu sana.”
“Asante sana.”
Niliingiza funguo ili kufungua mlango, lakini nikagundua kwa ndani
kulikuwa na funguo nyingine maana nilichungulia.
Nilipousukuma, ulifunguka. Hii ina maana wale watu wa ajabu
walikuwa wamesharudi, wako ndani. Niliingia ndani, nikafungua mlango wa
sebuleni, nikaingia humo.
Nilifikia kwenye kochi kubwa, nikajilaza. Sikuangalia kama kweli
wenzangu walikuwa wamesharudi, ila nilisikia sauti ya muziki wa redio, nikajua
wapo.
Mara nikasikia mlango wao mmoja ukifunguliwa, nikasikia mtu
akitoka. Kwa mara ya kwanza nilisikia akisema:
“Kama utamkamata anavuta bangi apelekwe polisi, ndiyo dawa yao
watu wa aina hii.”
Nilishtuka, nikakaa. Nikawaza kama ninachosikia ni cha kweli au?
Huyo aliyekuwa akisema hayo ni mwanamke na ilionekana alitoka
kuelekea uani. Nikatoka ghafla, nikaona kisigino cha mguu mmoja kikimalizia
kuingia chooni.
Nilirudi chumbani huku najiuliza kama hawa watu walisema vile kwa
sababu wamejua mimi nimenunua bangu au? Na ni kwanini wazingumze Kiswahili kwa
mara ya kwanza siku hiyo?
Baada ya dakika mbili, nilimsikia akirejea chumbani kwake huku
akisema:
“Mimi mtu anayevuta bangi siku yoyote na mahali popote pale,
nikimwona nampeleka polisi ajue mimi ni nani. Haiwezekani watu wawe wanavuta
bangi hovyo tu.
Moyoni nikasema hata iweje, hii bangi leo lazima niichome humu
ndani. Mkienda polisi msipoenda mtajua wenyewe.
“Mimi siwezi kuishi katika mazingira magumu namna hii wakati pesa
ni yangu. Kwanini ustaarabu usiwepo?” nilisema moyoni nikipeleka mkono mfukoni
ili kutoa ile bangi niliyonunua mara ya pili.
Niliipata, nikaitoa. Niliiweka kwenye meza kisha nikaendelea
kulala nikiusaka usingizi kwa nguvu zangu zote maana nilijisikia kuchoka sana.
Hapo nilikuwa sijaenda chumbani kwangu.
Sikumbuki ni muda gani nilipitiwa na usingizi, ila nakumbuka
wakati nalala ilikuwa saa kumi na moja. Nilipokuja kushtuka ilikuwa saa kumi na
mbili na nusu. Ina maana nililala kwa saa moja na nusu.
Jicho langu moja kwa moja lilitua kwenye bangi pale mezani,
sikuiona.
Nilihamaki kwa kusema ha! Nani amechukua bangi yangu? Sikujibiwa
na mtu, ukimya ulitawala huku akili ikiniambia wale wapangaji wenzangu watakuwa
wanahusika moja kwa moja.
Baada ya muda nilitoka mle sebuleni, nikaenda chumbani. Nilifungua
mlango na kusimama kwanza kabla ya kuzama ndani. Niliangaza kila kona,
nikabaini kitu.
Niligundua kwamba, kuna mtu alikaa kitandani maana nilipoondoka
asubuhi nilikuwa nimekitandika, muda huo kwa pembeni upande wa mbele
kulikuwa na alama za makalio.
Alama hiyo ilinipa picha kuwa, aliyekaa alikuwa na makalio makubwa
sana! Nilipoangalia chini kwenye kapeti nikabini kitu kingine kwamba, aliyekaa
alikuwa na mafuta kwenye miguu kwani iliweka alama kuzunguka miguu yake.
Aidha, nilibaini jambo jingine kwamba, aliyekaa kitandani pia alikuwa
akisimama na kutembeatembea kwani alama ya miguu yenye mafuta ilionekana sehemu
mbalimbali za chumbani kwangu.
Mara nikasikia hodi ikigongwa mlango mkubwa. Niliikumbuka ile
sauti kwamba ilikuwa ya yule msukuma mkokoteni wa maji.
“Nakuja,” nilisema kwa sauti kupitia dirishani kwani chumba changu
na sebule yangu vilikuwa upande wa mlango mkubwa wa kuingialia.
Nilitoka mpaka mlangoni, nikafungua na kumkuta yule kijana.
“Bro vipi, wapo wale watu ndiyo nimekuja hivi.”
Usikose sehemu ya Tano hapa hapa.
No comments:
Post a Comment