Kamati
ya Rufani ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imewaadhibu walalamikiwa watano kati ya saba baada ya kufanya mapitio
(revision) kwa uamuzi wa Kamati ya Maadili kutokana na maombi ya
Sekretarieti, huku Richard Julius Rukambura akifungiwa miaka 20
kujihusisha na mpira wa miguu.
Sekretarieti ya
TFF iliwasilisha maombi ya mapitio kwa Kamati ya Rufani ya Maadili ili
kupata mwongozo kwa vile kulikuwapo mkanganyiko kwenye uamuzi wa Kamati
ya Maadili, hivyo kuiwia vigumu kwake kuutekeleza.
Uamuzi huo wa
mapitio umesomwa leo jioni (Oktoba 15 mwaka huu) mbele ya waandishi wa
habari na wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti
Victoria Makani.
Rukambura
amefungiwa miaka 20 baada ya kupeleka masuala ya mpira wa miguu katika
mahakama za kawaida kinyume na Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF na kifungu
cha 73(3)(b) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013. Adhabu yake
itamalizika Oktoba 15, 2033.
Kabla ya kutoa
adhabu hiyo, Kamati imejiridhisha kuwa Rukambura ni mwanafamilia wa TFF
kwa vile aliwahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Pamba ya Mwanza, na fomu
zake za kuomba uongozi TFF ziliidhinishwa na Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Shinyanga. Vilevile ni ‘Leadership Aspirant’ kwa mujibu wa
kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo la 2013.
Pia imesema kwa
Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kusajili Katiba ya TFF
inayokataza masuala ya mpira wa miguu kwenda katika mahakama za kawaida,
na kutaja vyombo vya haki vitakavyoshughulikia masuala hayo (judicial
organs), Kamati ya Maadili ilikosea kutomtia hatiani mlalamikiwa kwa
kuegemea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye Shaffih
Dauda, Kamati imebaini kuwa mwanafamilia wa TFF kwani ni Mwenyekiti wa
Bombom FC, fomu yake ya kuomba uongozi ilipitishwa na klabu ya Simba na
pia ameshakuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali ndani ya Chama cha Mpira
wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA), hivyo yeye ni ‘Leadership
Aspirant’ kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo
la 2013.
Hivyo Dauda
amepatikana na kosa la kimaadili kwa kutotekeleza maagizo rasmi ya TFF
ya kutosambaza barua iliyotoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Kamati ya
Rufani ya Maadili imempa onyo kali na faini ya sh. milioni moja
anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo akishindwa kufanya hivyo
atafungiwa mwaka mmoja. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha
6(1)(a),(c) na (h) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
Akilipa faini ataweza kuendelea na mchakato wa kugombea nafasi ya uongozi aliyoomba.
Nazarius
Kilungeja amepatikana na kosa la kimaadili kwa mujibu wa kifungu cha
73(8)(a) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, kwani akijua kuwa
ana adhabu ya kinidhamu ya kufungia miaka mitano na Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) iliyoanza 2009 alichukua fomu kuomba
uongozi TFF.
Hivyo,
amefungiwa miaka mitatu, adhabu ambayo itakwenda sambamba na ile ya
RUREFA ambapo kifungo chake sasa kitamalizika Oktoba 15, 2016.
Sekretarieti ya
TFF imepewa onyo kali kwa kupokea fomu yake ya kugombea na malipo
wakati akiwa amefungiwa. Onyo hilo pia limetolewa kwa Chama cha Makocha
wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) Mkoa wa Rukwa kwa kuidhinisha fomu
yake ya kugombea.
Naye Wilfred
Kidao Mzigama ambaye ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF amepatikana na
kosa la kimaadili kwa kuwa na nyaraka la Kamati ya Utendaji bila kibali
na kukiuka taratibu za kuwasilisha malalamiko kwa mujibu wa Ibara ya
12(2) na Ibara ya 50(1) na (5) ya Katiba ya TFF.
Amepigwa faini
ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo
akishindwa atafungiwa mwaka mmoja. Akitekeleza adhabu hiyo ataweza
kuendelea na mchakato wa kugombea uongozi kwa nafasi aliyoomba.
Vilevile Kamati
hiyo imetoa onyo kali kwa Sekretarieti ya TFF na wajumbe wa Kamati ya
Utendaji kwa kushindwa kudhibiti nyaraka muhimu za vyombo vyao.
Pia Kamati ya
Rufani ya Maadili imempata na kosa la kimaadili Kamwanga Tambwe kwa
mujibu wa kifungu cha 73(8) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013,
kwa kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wakati ana adhabu ya kinidhamu
inayomalizika 2014.
Hivyo, amepewa
adhabu ya kufungiwa miaka mitatu ambayo itakwenda sambamba na ile ya
kinidhamu na kumalizika Oktoba 15, 2016. Pia Sekretarieti ya TFF, Chama
cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU) na Chama cha Waamuzi wa Mpira
wa Miguu Tanzania (FRAT) Mkoa wa Ruvuma wamepewa onyo kali kwa kupokea
na kuidhinisha fomu zake za kugombea uongozi wakati akitumikia adhabu ya
kufungiwa.
Kamati ya
Rufani ya Maadili imewakuta kutokuwa na hatia ya makosa ya maadili kama
ilivyobaini Kamati ya Maadili walalamikiwa Riziki Juma Majala na Omar
Isack Abdulkadir, hivyo wana haki ya kugombea uongozi kwa kufuata Katiba
na Kanuni za TFF.
Kwa mujibu wa
kifungu cha 74(4) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, uamuzi wa
Kamati ya Rufani ya Maadili hauna fursa ya rufani wala marekebisho
kutoka chombo kingine chochote isipokuwa FIFA na Mahakama ya Usuluhishi
wa Michezo (CAS).
chanzo: shafiidauda.com
No comments:
Post a Comment