SERIKALI imepokea vifaatiba vya kusaidia watoto wanaozaliwa na
matatizo ya kushindwa kupumua, vyenye thamani ya sh milioni 664.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mganga
Mkuu wa Serikali, Dk. Donald Mbando, alisema msaada huo ulitolewa na
Shirika la Misaada kwa ajili ya kuokoa maisha ya mtoto (CIF), la nchini
Uingereza.
“Vifo vya watoto hao vinaweza kutokea ndani ya saa 24 pindi anapokosa
msaada wa kupumua wakati wa uhai wake anapozaliwa,” alisema.
Alisema anaamini kupatikana kwa vifaa hivyo itakuwa chachu ya kupunguza tatizo hilo nchini.
Dk. Mbando alisema vifaa hivyo walivyopokea ni vya aina tatu ambavyo
kazi zake ni kusaidia kuokoa maisha ya baadhi ya watoto wanaozaliwa na
matatizo ya kushindwa kupumua.
Alisema vifaa hivyo vitasambazwa katika mikoa 16 na wilaya zake, na kwamba lengo ni kuifikia mikoa yote nchini.
Dk. Mbando alisema mpango huo wa miaka mitatu unaendeshwa kwa
ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na Shirika la Mama na Familia
‘Jhpiego’.
Alisema ili kufanikisha malengo ya mpango huo wametoa mafunzo kwa
watoa huduma 2,500 kati wahudumu 14,000 wanaokusudiwa, ambapo mafunzo
hayo yamewasaidia watendaji hao kutoa huduma kwa usahihi zaidi.
Mkurugenzi Mkazi wa Jhpiego, Maryjane Lacoste, alisema wataendelea
kuiunga mkono serikali katika mpango huo, ikiwemo kufadhili vifaa
mbalimbali vitakavyotumika kuokoa maisha ya watoto hao.
No comments:
Post a Comment