WAKATI mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zikitarajiwa kuendelea leo
na kesho, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetoa onyo kali kwa watu
watakaonaswa wakiwa na silaha za aina mbalimbali kwenye viwanja vya
soka kama ilivyotokea wikiendi iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa
Habari wa TFF, Boniface Wambura, alikiri watu 17 kukamatwa na bastola
katika mechi mbili wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, jambo
ambalo ni kinyume na sheria za usalama viwanjani.
“Sheria za usalama za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa),
haziruhusu mashabiki kuingia viwanjani na silaha hata kama wana umiliki
halali. Watakaorudia tabia hiyo wikiendi hii hawatoruhusiwa kuingia
uwanjani hata wakiwa na leseni na tiketi,” alisema Wambura.
Alibainisha kuwa mechi ya Yanga na Ruvu Shooting, watu 11 walikamatwa
na bastola, kabla ya tukio hilo kujirudia tena wakati Simba ilipoumana
na JKT Ruvu, ambako sita pia walikamatwa.
Wambura aliongeza kuwa watu wote waliokamatwa wikiendi iliyopita,
walikuwa na leseni za umiliki, hivyo kuruhusiwa kuziacha mikononi mwa
polisi na kwenda kuangalia mechi kisha kurejeshewa wakati wakiondoka,
nafasi ambayo haitatolewa leo.
“Hata kama mtu awe na leseni halali ya umiliki, au awe na tiketi ya
bei kubwa kiasi gani, hatoruhusiwa kuingia, hivyo mashabiki wanaomiliki
silaha tunawashauri kuzihifadhi huko wanakotoka kabla ya kufika
viwanjani,” alisisitiza Wambura huku akikataa kuwataja majina
waliokamatwa wiki iliyopita kwa kuwa hana mamlaka kisheria.
Wambura alitoa wito kwa kwa kila shabiki atakayemuona mwenzake akiwa
na silaha uwanjani, kutoa taarifa kwa mamlaka husika, likiwemo Jeshi la
Polisi ili aweze kuchukuliwa hatua kwa kukiuka sheria ya usalama
viwanjani.
Ukaguzi wa mashabiki wanaoingia viwanjani na silaha, umekuja wakati
nchi za Afrika
Mashariki zikiomboleza vifo vya watu wanaokadiriwa
kufikia 67 waliokufa katika shambulizi la kigaidi kwenye kituo cha
biashara cha Westgate, jijini Nairobi na wengine 177 kujeruhiwa.
Kauli ya Wambura imekuja huku timu nane za Ligi Kuu zikitarajiwa kujitupa viwanjani leo.
Kwenye Uwanja wa Taifa, vinara Simba watakuwa wageni wa Ruvu Shooting katika pambano linalotabiriwa kuwa na upinzani.
Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Mohamed
Theofil kutoka Morogoro kuanzia saa 10:00 jioni vitakuwa sh 5,000, sh
8,000, sh 15,000 na sh 20,000.
Mechi nyingine, maafande wa JKT Ruvu watawaalika Kagera Sugar kwenye
Uwanja wa Azam Complex, huku Coastal Union na Azam FC zikitunishiana
misuli Mkwakwani jijini Tanga.
JKT Oljoro watakuwa nyumbani Sheikh Amri Abeid jijini Arusha
kuwaalika Mbeya City, wakati kesho kutakuwa na kibarua kigumu kati ya
Yanga na Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, huku Mgambo wakiwakaribisha
Tanzania Prisons, Mkwakwani.
No comments:
Post a Comment