MOTO wa wadau wa tasnia ya habari kuitaka serikali iyafungulie
magazeti ya Mwananchi na Mtanzania yaliyofungiwa kwa madai ya uchochezi,
umezidi kukolezwa na sasa wanataka Idara ya Habari (Maelezo) ifutwe kwa
madai imepitwa na wakati.
Magazeti hayo ya kila siku yalifungiwa Septemba 27 mwaka huu, kwa
kutumia sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976 inayolalamikiwa,
ambapo Mwananchi ilipewa adhabu ya siku 14 huku Mtanzania ikiwekwa
kifungo cha siku 90.
Akizungumza za na gazeti hili jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Mtakatifu Augustino (SAUT), Dk. Joseph Matumaini, alisema kuwa serikali
inapaswa kuomba radhi kwa kitendo hicho na kuyafungulia magazeti hayo
haraka.
Alisema kuwa uamuzi uliofanyika ulitumia sababu zisizo na faida kwa umma wa Watanzania.
Matumaini ambaye pia ni padri wa Kanisa Katoliki aliongeza kuwa Idara
ya Habari (Maelezo) imepitwa na wakati, hivyo inapaswa ifutwe.
Aliongeza kuwa hata mkurugenzi wa Maelezo naye anapaswa kujiuzulu kwa
sababu hakujielekeza katika masuala ya maadili ya uandishi wa habari,
sheria za uandishi na sera za habari.
Padri Matumaini alisema Maelezo si chombo cha mtu binafsi ingawa
kinatumiwa vibaya na serikali. Serikali imeshindwa kuongoza wananchi
inaamua kutishia demokrasia na uhuru wa habari.
“Wanahabari wote tuungane chini ya Baraza la Habari Tanzania kama
Mkurugenzi huyo, Assah Mwambene, hatajiuzulu na serikali isipoomba
radhi, basi sisi tuunde chombo chetu huru, Maelezo ibaki na magazeti na
televisheni ya serikali.
Alihoji kuwa kama kweli magazeti hayo yaliandika habari za kusababisha
upotevu wa amani, mbona tangu yasomwe hakujatokea uvunjivu wowowe wa
amani.
“Maelezo wajue kuwa kazi mojawapo ya vyombo vya habari ni kusema
ukweli kuhusu ajenda fulani, ajenda juu ya jambo fulani nchini si lazima
iipendeze serikali,” alisema.
MCT yalaani
Baraza la Habari Tanzania (MCT) limelaani vikali hatua ya serikali
kuyafungia magazeti ya kila siku ya Mwananchi na Mtanzania kwa tuhuma za
kuchapisha habari za uchochezi na kuhatarisha amani ya nchi.
Taarifa ya MCT iliyosainiwa na Katibu wake Mtendaji Kajubi Mkajanga
ilisema kuwa uamuzi uliochukuliwa na serikali ni wa kusikitisha na
kinyume na demokrasia na umerudisha nyuma hatua nyingi zilizopigwa na
nchi kujenga taifa la kidemokrasia linaloheshimu uhuru wa kujieleza na
wa vyombo vya habari.
“Uhuru wa kujieleza ni haki ya msingi ya binadamu na nchi inayojivunia
kuwa imejengwa kwenye misingi ya demokrasia na kuheshimu haki za
binadamu kama Tanzania haina budi kuhakikisha kuwa haki hiyo inalindwa
kwa nguvu zote.
“Vyombo vya habari vinampa mwananchi uwezo wa kuitumia haki hiyo ya
kujieleza na kupata habari ambayo imeathirika kwa kufungiwa kwa magazeti
hayo,” alisema.
Alisema kuwa japo taifa limepiga hatua kubwa katika kuisimamia haki
hiyo ya msingi ya kujieleza na kupata habari, juhudi hizo zinafifishwa
kwa kuwepo kwa sheria mbaya zinazofinya haki hiyo kama sheria ya
magazeti ya mwaka 1976 ambayo inampa madaraka waziri anayehusika na
maswala ya habari kuyafungia magazeti bila ya haki ya kujitetea au
kukata rufaa.
Sheria zingine zinazofifisha uhuru wa kujieleza wa vyombo vya habari
na uhuru wa kupata habari ni pamoja na sheria ya Usalama wa Taifa ya
1970 na Sheria ya Siri za Serikali 1963.
Akisema kuwa serikali ina uwezo wa kutumia njia mbadala kama inahisi
kuwa haijatendewa haki katika kuripotiwa masuala yake na vyombo vya
habari ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa na matamko kuhusu kazi zake na
kupeleka mashauri MCT.
“Baraza linahimiza vyombo vya habari na wananchi kuunga mkono juhudi
zake na wadau wengine wa habari katika kushinikiza kufutwa kwa sheria
kandamizi zinazofifisha uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari na
haki ya kupata habari.
Pia ni muhimu kwa wananchi kupigania haki hizo zipate mashiko katika Katiba mpya inayotarajiwa.
Wanaharakati
Watetezi wa Haki za Binadamu na Taasisi za Habari nchini zimelaani
ubabe wa serikali kwa kuendelea kuvifungia vyombo vya habari kwa kutumia
sheria kandamizi ya mwaka 1976.
Mratibu wa mtandao huo, Onesmo ole Ngurumwa, aliyasema hayo wakati
akitoa tamko la pamoja la mtandao unaowakilishwa na zaidi ya mashirika
50 ya haki za binadamu.
Pia katika muunganiko huo kulikuwepo Umoja wa Vyombo vya Habari
(MOAT), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan), na
Baraza la Habari (MCT) vyombo ambavyo vilipinga kitendo cha kufungiwa
magazeti hayo.
Alisema hatua ya kuyafungia magazeti hayo, inaonyesha dhahiri nia ya
serikali ya kutaka kuwatisha wananchi, kuleta hofu kwenye jamii na
kuwanyamazisha wapigania haki za binadamu, vyombo vya habari, na
watetezi wa haki za binadamu nchini.
“Hatua hii ya serikali inafanya idadi ya magazeti yaliyofungiwa
kufikia matatu, Julai mwaka jana serikali ililifungia gazeti la
MwanaHALISI kwa muda usiojulikana,” alisema.
Hata hivyo, mtandao huo, kwa kushirikiana na asasi za kiraia na
taasisi za habari, ulisema kuwa wanapaswa kuongeza nguvu katika kesi ya
Kikatiba iliyofunguliwa na Kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd dhidi
ya serikali kutaka kufutwa kwa sheria ya magazeti ya mwaka 1976.
“Sheria inamgeuza waziri kufanya kazi za uhariri, kushutumu, kushtaki,
kuhukumu na kutekeleza hukumu. Hii ni kinyume cha utawala wa sheria na
kanuni za haki asili.
“Sheria hizi kwa miaka mingi zimekuwa zikipigiwa kelele kwa kuwa ni
sheria kandamizi; zinapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano na sheria
za kimataifa,” alisema.
Aidha mtandao huo, pamoja na wadau wengine wamewaomba wananchi wenye
mapenzi mema kushirikiana kuitaka serikali kufuta au kuzifanyia
marekebisho sheria zote kandamizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.
Zitto akomaa
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), jana alitoa
taarifa rasmi kwa Katibu wa Bunge kwa mujibu wa kanuni za Bunge kwamba
katika mkutano ujao atawasilisha muswada binafsi wa sheria kufanya
marekebisho ya sheria ya magazeti kwa lengo la kuifuta kabisa sheria
hiyo.
Alisema kuwa madhumuni ya muswada huo ni kufuta sheria ya magazeti ya
mwaka 1976 kwa sababu inakinzana na Katiba ya nchi kuhusu haki za raia
kupata habari na kwamba iliorodheshwa na tume ya marehemu Jaji Francis
Nyalali kuwa ni sheria kandamizi.
Zitto alisema kuwa muswada wenyewe atauwasilisha siku ya Ijumaa ili
uchapwe kwenye gazeti la serikali uweze kuingia kwenye shughuli za Bunge
zitakazoanza Oktoba 15, 2013, kwa ngazi ya kamati.
Uamuzi huo wa Zitto uliungwa mkono na mbunge mwenzake wa Ubungo, John
Mnyika (CHADEMA), ambaye alisema kuwa licha ya kutangaza awali kuchukua
hatua kama hiyo, amemwachia Zitto ambaye kiprotokali ni Naibu Katibu
mkuu wa chama.
Wachungaji
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na haki za jamii kwa madhehebu ya
dini nchini, Mchungaji William Mwamalanga, amesema kuwa serikali
haikupaswa kuyafungia magazeti hayo bali adhabu hiyo ilipaswa kuelekezwa
kwa watendaji wa serikali wanaovujisha siri hizo.
Mbali na hilo kamati hiyo imemtaka Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, kuyafungulia magazeti hayo kwa kuwa
kitendo hicho kimeonyesha jinsi serikali inavyotumia vibaya sheria ya
magazeti ya mwaka 1976 ambayo imekuwa ikilalamikiwa.
Akizungumza na Tanzania Daima jana baada ya kutoa tamko lao,
Mwamalanga alisema kuwa kabla ya serikali kuchukua uamuzi huo ilipaswa
kuyaonya magazeti hayo badala ya kuchukua hatua kali ya kuyafungia.
“Kwa kweli kamati yetu haijalikubali suala hilo; tunapenda kumuomba
waziri mwenye dhamana kuyafungulia magazeti hayo kwani hatua
waliyochukua hawakuzingatia mazingira ya ndani yalivyo,” alisema.
Naye Mkuu wa Chuo cha Habari Iringa, Dominick Haule, alisema kilichofanyika ni hujuma na kwamba jambo hilo lilipangwa.
Alisema mtumishi wa serikali aliyefanya hivyo anatakiwa kutambua kuwa
amejinufaisha lakini pia ni hasara kwa serikali kwa kuwa taarifa hizo
zinafika takriban mataifa yote.
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, alisema taaluma ya habari ni nyeti na haiwezi kumfurahisha kila mtu.
Aliongeza kuwa ni bahati mbaya kwa wahariri na waandishi wao wanapimwa kwa walichoandika na si walichokiacha.
Filikunjombe aliongeza kuwa kama serikali ingeona walichoacha ingeweza kuvipigia magoti vyumba vya habari.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment