JESHI la Polisi mkoani Geita limethibitisha kuonekana kwa mtoto
Shabani Maulidi, anayedaiwa kufufuka baada ya miaka mitatu ya kifo
chake, kilichosababishwa na kutumbukia kisimani mwaka 2011.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamnda wa jeshi
hilo, Leonard Paulo, alisema kuwa pamoja na kuthibitisha tukio la
kuonekana kwa mtoto huyo akiwa hai bado serikali haiamini kama ni kweli
alikufa na kufufuka.
“Mimi kama kamanda wa polisi na serikali kwa ujumla, hatuamini kama
mtoto huyu alikufa na kufufuka, japo wazazi wake wanakiri hilo. Serikali
haiamini vitu kama hivyo,” alisema.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita ambapo mtoto huyo
alilazwa kwa matibabu, alisema kuwa hali yake inaendelea vizuri na
wakati wowote ataruhusiwa.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini
ukweli juu ya tukio hilo kwa kushirikiana na wataalamu kutoka hospitali
ya wilaya, ambapo kwa sasa hatua inayoendelea ni kutafuta vipimo vya
vinasaba (DNA).
Katika tukio jingine, mtoto wa miezi miwili, Edga Sizya, amefariki
dunia papohapo baada ya kupigwa kichwani eneo la paji la uso na baba
yake mzazi, Sizya Kilulinda (35) mkazi wa Bugurula.
Kamanda huyo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 28, mwaka huu,
baada ya kutokea ugomvi kati ya baba na mama wa mtoto huyo, Kulwa Lukas
(27) kwa kile alichodai kuwa ni mke kupika ugali wa muhogo.
Alisema kuwa hatua hiyo ilizua ugomvi, ambapo baba wa marehemu
Kilulinda aliruka na kumpiga kichwa mkewe na bahati mbaya kichwa hicho
kilimpata mwanaye kwenye paji la uso akiwa amebebwa mgongoni na mama
yake.
Kufatia tukio hilo, wananchi waliamua kumpiga Kalulinda na kupoteza maisha na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi.
No comments:
Post a Comment