VIJANA nchini, wametakiwa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya
jamii ili kujihakikishia usalama wa maisha bora kutokana na fursa
zilipo kwenye mifuko hiyo iliyoko hapa nchini kwa sasa.
Wito huo, umetolewa na msanii wa kizazi kipya, Mwasiti Almasi, wakati
akizungumza kwenye semina ya Fursa kwa vijana iliyofanyika kwenye
viwanja vya Tangamano jiji hapa.
Mwasiti alisema kwa sasa vijana ndio nguvu kazi ya taifa
inayotegemewa, lakini kutokana na kukosa uelewa wa kuzitumia fursa
zilizopo, vijna wengi wamekuwa tegemezi kwa familia zao na mzigo kwa
taifa.
“Mtanzania wa kawaida kama unataka mitaji ya uhakika ingia kwenye
mfuko wa NSSF, kwani mfuko huo umetusaidia sana sisi wasanii wa Kigoma
All Stars, kwani umetukomboa kiuchumi na umetupa mwangaza mkubwa wa
kimaendeleo,” alisema Mwasiti.
Naye msanii Nickson Simon ‘Nikki wa Pili’ alisema vijana wengi
wamekosa taarifa sahihi kuhusu namna ya kutumia fursa zilizopo katika
kujileta maendeleo yao na taifa kwa ujumla, hali inayowafanya waonekane
ni tegemezi.
“Tatizo ni jinsi tunavyowaandaa vijana, kwani elimu wanayopata
haiendani na mazingira ya fursa yaliyopo kwenye maeneo yao, utaona
kijana toka anapata elimu ya msingi hadi chuo, hakuna kitu cha
ujasiriamali alichojifunza wala taaarifa zozote kuhusu kujitegemea
alizozipata,” alisema Nikki wa Pili.
Aliongeza kuwa ifike wakati vijana walioko shuleni wasiishie kupata
elimu ya darasani, bali waandaliwe kwa ajili ya kuhakikisha wanapewa na
elimu nyingine ya fursa zilizopo kwenye eneo husika walipo.
Hata hivyo, mwakilishi kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Makao
Makuu, Salim Kimaro, alisema mfuko wao kwa sasa umejikita katika
kuwasaidia vijana kiuchumi kwa kuwapa mikopo ambayo wataitumia
kuendeshea biashara zao walizozibuni.
“Cha msingi ni vijana kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya
akiba na mikopo (saccos), baada ya hapo wawe wanachama wa mfuko wetu na
wawe wamechangia kwa kipindi cha miezi sita watapata fursa ya
kukopeshwa fedha,” alisema Kimaro.
No comments:
Post a Comment