BARAZA Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) limeitaka
Serikali kurejesha bungeni kwa hati ya dharura Muswada wa Marekebisho ya
Tozo ya Sh 1,000 kwa laini za simu kwa mwezi.
UVCCM imesema ikiwa tozo hiyo itatekelezwa, itanyima Watanzania zaidi
ya milioni nane haki ya msingi ya mawasiliano na huduma za kupokea na
kutuma fedha kwa mtandao, jambo ambalo pamoja na kwamba lililenga
kuongeza mapato, ni dhahiri litayashusha.
Sambamba na hilo, Baraza limempa Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chiza siku 21 kutoa kwa umma hatua anazochukua ili
kuokoa wakulima wa korosho nchini dhidi ya unyonyaji, unaofanywa na
walanguzi wa zao hilo.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda aliwaambia waandishi wa habari
jana katika ofisi za Makao Makuu ya CCM mjini hapa kuwa maazimio hayo
yalifikiwa na Baraza Kuu la Umoja huo katika kikao chake cha siku moja
jana, chini ya Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Sadifa Juma Hamis.
Kwa mujibu wa Mapunda, katika kikao hicho walijadili migogoro ya
wafugaji na hifadhi, taarifa ya utekelezaji wa tozo ya Sh 1,000 kwa
laini za simu na masuala ya wakulima wa korosho.
Kuhusu tozo ya Sh 1,000, Mapunda alisema: “Baraza limejadili kwa kina
na kubaini athari zinazoweza kutokea kutokana na tozo hiyo kwamba ni
pamoja na ugumu wa ukusanyaji Sh bilioni 178 kwa mwezi katika bajeti ya
mwaka 2013/14 ambao utaratibu wake unazorotesha na kurudisha nyuma
juhudi za kisekta kuwezesha mawasiliano kwa wote.
“Lakini idadi kubwa ya wateja milioni nane ambao ni wa kipato cha
chini watakosa huduma. Kushindwa kufikia watu wengi kwa huduma zaidi ya
milioni nane kati ya idadi ya watumiaji milioni 26, ni dhahiri
wakiondolewa kwenye mfumo wa mawasiliano, mapato yatashuka kwa watoa
huduma na Serikali,” alisema Mapunda.
Kutokana hilo, alisema Baraza Kuu la UVCCM linaitaka Serikali
kuzingatia mazungumzo ya Julai 23 ya Rais Jakaya Kikwete na watoa huduma
za mawasiliano ya simu nchini baada ya Rais kukubali kuwapo ugumu wa
utekelezaji wa hilo hasa namna ya ukusanyaji wa fedha na ukosefu wa
mawasiliano kwa watu wenye kipato cha chini.
Kuhusu wakulima wa korosho, Mapunda alisema Baraza lilijadili
changamoto za wakulima wa korosho nchini ikirejea uamuzi wa Kamati Kuu
ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mei mjini hapa kuhusu matatizo ikiwamo
kuyumba kwa bei ya korosho, malipo kuchelewa, tozo nyingi na udhaifu wa
baadhi ya vyama vya ushirika.
“Baraza Kuu limeamua kwa pamoja kuwa hali hiyo haivumiliki na
wananchi wana haki ya kulalamikia matatizo hayo, pia limesikitishwa na
kasi ndogo ya utekelezaji wa agizo la Kamati Kuu ya CCM la Mei
lililoitaka Serikali iwaite wadau wote na kuchukua hatua mapema,”
alisema Mapunda.
Alisema kutokana na hilo, Baraza Kuu linamtaka Waziri Chiza kufanya
uamuzi wa dharura wa kushughulikia matatizo hayo katika kipindi cha siku
21 na kutoa kwa umma hatua alizochukua na atakazoendelea kuchukua
kuokoa wakulima wa korosho na unyonyaji hasa wa bei kuyumba.
Mapunda alisema Baraza Kuu lilijadili migogoro ya wafugaji na
hifadhi, hasa katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara inayopakana na
hifadhi ya Serengeti na mkoa wa Lindi, ambako wilaya zake za Kilwa na
Liwale zinapakana na Hifadhi ya Selous kuwa kumekuwa na unyanyasaji
mkubwa.
Alisema wafugaji na askari wa wanyamapori na wa kampuni ya uwekezaji
ya Gurumeti, wamekuwa wakinyanyaswa na kutozwa kiwango cha Sh 50,000
hadi Sh 300,000 kwa ng’ombe mmoja bila stakabadhi na walitaka watendaji
wa Serikali wasikae kimya wakati wananchi wananyanyaswa.
CHANZO NI HABARI LEO
No comments:
Post a Comment