Habari na Tanzania Daima.
HOFU kubwa imetanda ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
juu ya upatikanaji wa katiba mpya, hasa baada ya Rais Jakaya Kikwete
kusaini muswada ambao sasa ni Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya
Katiba.
Mkutano kati ya Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vyenye
uwakilishi bungeni uliofanyika Ikulu Oktoba 15, 2013 umeongeza mpasuko
ulioanza kujitokeza baina ya makada wa CCM na wapinzani.
Katika mkutano huo, rais na viongozi wa upinzani waliafikiana vyama
vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha
Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba viwasilishe
mapendekezo yao haraka serikalini ili ifatutwe namna ya kuyashirikisha
katika marekebisho ya sheria hiyo.
Walikubaliana kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika
mchakato wa katiba mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa
mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele
mchakato huo kwa masilahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa.
Awali kabla ya mkutano huo, makada wa CCM wakiwamo mawaziri kadhaa
waliweka wazi kuwa milango ya Ikulu imeshafungwa kwa wapinzani
kuzungumzia suala hilo, lakini Rais Kikwete alipotangaza kukutana nao
iliwaweka njia panda.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa baadhi ya makada wa CCM
wamekuwa wakimshutumu Rais Kikwete kwa kuwabembeleza wapinzani huku
akikiumiza chama chake.
Hoja wanayoijenga ni kuwa Rais Kikwete anataka kujijengea kitu cha
kukumbukwa, hasa katika suala la katiba mpya bila kujali athari
zinazokipata chama chake.
Makada hao wanaweka bayana kuwa hali hiyo itakiacha chama katika
wakati mgumu wa kukabiliana na wapinzani wanaoonekana kuimarika kadiri
siku zinavyoyoyoma.
Baadhi ya wabunge wa CCM wanamuona Kikwete kama msaliti kwa wabunge
wake waliopitisha muswada huo, ambao sasa ni Sheria ya Marekebisho ya
Mabadiliko ya Katiba, ukiwa na upungufu ulioainishwa na wapinzani.
Mmoja wa watu waliohudhuria mazungumzo ya Ikulu anasema rais aliridhia
marekebisho hayo na alibainisha kuwa yajikite katika masuala kadhaa,
likiwamo suala la Tume ya Warioba kuwapo kwenye Bunge Maalumu la Katiba,
marekebisho katika suala la uteuzi wa wajumbe 166 ili idadi iongezeke
na hoja ya Zanzibar kushirikishwa kabla ya muswada wa sheria ya kura za
maoni kuanza.
Tayari Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph
Warioba, alishatoa tamko kuwashangaa wabunge wa CCM kwa kupotosha
kifungu kilichokuwa kinasema Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavunjwa na
rais mara tu baada ya kuwasilisha rasimu kwenye Bunge Maalumu la Katiba,
msimamo ambao unaungwa mkono na Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala
(CCM).
Mbunge huyo katika andiko lake alilolisambaza katika vyombo vya
habari, anakiri kuwa moja ya upungufu alioubaini katika muswada ule
ambao sasa ni sheria, ni kuiua Tume ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya
mchakato kufikia mwisho.
“Kiukweli, lina mantiki ndani yake. Tukiwa kwenye Bunge la Katiba
hakutakuwa na serikali, sasa ni nani atakayejibu na kuweka sawa hoja za
wabunge? Hili kwa kweli wabunge tuliopitisha muswada ule hatukuliona
vizuri,” alisema Kigwangala.
Wakati Kigwangala akiona upungufu huo, Naibu Spika Job Ndugai,
aliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa haoni udharura wa suala hilo
kurejeshwa bungeni.
Ndugai amebeza suala la urejeshwaji wa sheria hiyo bungeni, akihoji kuwa suala hilo halina udharura.
“Ni ishu gani hasa ambayo wapinzani walienda kumwona rais ambayo
inahitaji udharura huo? Je, kanuni za Bunge zinaruhusu suala hilo?”
alihoji Ndugai.
Akizungumza na gazeti hili wiki hii, Katibu wa Halmashauri Kuu ya
Chama Cha Mapinduzi, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema Bunge ni
muhimili tofauti. Wabunge kama wataona kuna kitu cha kubadilisha
watabadilisha, lakini wakiona hakuna cha kubadilisha itabaki ilivyo.
Kauli hiyo imeungwa mkono jana na Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias
Chikawe, ambaye alinukuliwa na gazeti moja nchini (si Tanzania Daima),
akisema: “Serikali haikusudii kufanya marekebisho yoyote kwenye Sheria
ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba iliyosainiwa na Rais Kikwete hivi
karibuni.”
Mmoja wa wabunge wa CCM aliyehojiwa na gazeti hili na kutoa msimamo
wake baada ya rais kusaini muswada kuwa sheria ni aliyekuwa Mwenyekiti
wa UVCCM, Hamad Yusuf
Massauni, ambaye sasa ni Mbunge wa Kikwajuni.
“Mimi ningekuwa rais nisingepoteza muda kuongea na wapinzani, na hata
kama sheria hii itarejeshwa bungeni, sioni sehemu yoyote ya kufanyia
marekebisho, iwe ya kuondoa koma wala kuweka nukta,” alisema.
Kabla ya muswada huo kusainiwa kuwa sheria, Nape alinukuliwa na gazeti
hili akisema: “Hofu yangu ni kuwa rais asiposaini muswada huo, ataingia
katika mgogoro kikatiba, itabidi arejeshe muswada bungeni aeleze
kwanini hajasaini, na ukirejeshwa bungeni wabunge wa CCM wakakataa
kufanya mabadiliko, rais angelazimika kuvunja Bunge.”
Aliongeza kuwa: “Mimi ninaona afadhali rais asaini muswada huu ili
kama kuna upungufu uwekwe mezani kama ilivyokuwa mwanzo, ila nakubali
kabisa mzee Warioba ana hoja katika suala la kutovunjwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kabla ya kutetea rasimu mbele ya Bunge Maalumu la
Katiba.”
Alisema wabunge wa CCM ni asilimia 74 ya wabunge wote, hivyo
wakishikilia hoja ya kutobadilisha jambo lolote katika muswada huo baada
ya kurejeshewa na rais, matokeo yake ni kuvunjwa kwa Bunge na nchi
kuingia kwenye uchaguzi kabla ya 2015.
Nape alisema CCM haiko tayari kuingia kwenye uchaguzi kabla ya 2015,
hivyo akawataka wanaopinga na kuunga mkono hoja hizo watumie busara na
hekima kufikia maridhiano yatakayolijenga taifa.
Alisema kuwa muswada wa mabadiliko ya sheria wa mwanzo nao ulipitishwa
ukiwa na kasoro mwaka 2011, lakini Chama cha Demokrasia na Maendeleo
walienda kwa rais wakajadiliana wakakubaliwa, na kwamba viongozi wa CCM
walilazimika kwenda Dodoma kuwaeleza wabunge msimamo wa Rais Kikwete na
kuwashawishi waukubali.
“Tulipoona kuna hoja tulilazimika kwenda Dodoma kuwaomba wabunge wetu
wakubali hoja za CHADEMA ili marekebisho yafanyike, ingawa suala hilo
lilifanyika kwa taabu sana, sasa zamu hii wabunge wa CCM wanaweza
wasikubali hoja za wapinzani, na likiendelea vile rais atalazimika
kuvunja Bunge, hili suala limetuweka pabaya sana CCM, sijui hatima
yetu,” alisema.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa iwapo serikali itaridhia
marekebisho yaliyotajwa na wapinzani, mvutano mkubwa utazuka bungeni
kati ya washindi na washindwa.
Jambo hilo linadaiwa halitakubaliwa na wabunge wa CCM ambao mara kwa
mara wamekuwa wakishutumiwa kupitisha mambo kwa kuangalia zaidi masilahi
ya chama kuliko taifa.
Kumekuwa na mipango ya CCM kumuandaa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, kuwa Spika wa Bunge la Katiba.
Inadaiwa Chenge ndiye atakayebeba jukumu la kudhibiti baadhi ya hoja
zinazopingwa na CCM zilizotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini
ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba.
Miongoni mwa mambo yaliyomo ndani ya rasimu ya katiba ni serikali tatu.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA LA JUMAPILI 20-10-2013
No comments:
Post a Comment