ZAIDI ya wafanyabiashara 600 wa Soko la Manzese wamemtaka
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kuingilia kati mgogoro baina yao na
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Manzese, Joseph Mkude wa kutaka
kulibinafsisha soko hilo kinyemela.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Katibu wa
soko hilo, Mustapha Milongege alisema watendaji hao wamekuwa wakifanya
hujuma za makusudi za kutowasilisha makusanyo yao kwa usahihi ili
wafanyabiashara waonekane hawalipi ushuru.
Alisema mwenyekiti huyo akishirikiana na Diwani wa Kata ya Manzese,
Eliamu Manumbu, wako kwenye hatua za mwisho za kulibinafsisha soko kwa
kigogo mmoja wa serikali anayemtumia mfanyabiashara maarufu jijini Dar
es Salaam.
“Kwa mfano hata hili banda la mamantilie lililojengwa kwa niaba ya
aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi nalo pia wanataka
kuliuza kwa mfanyabiashara. Aliwaahidi kuwa atawapatia ofisi katika
jengo la kisasa atakalojenga,” alisema Milongege.
Alisema hata kama ni suala la maendeleo, bado viongozi wanapaswa
kushirikiana na wafanyabiashara hao katika kila hatua ili wafahamu kuwa
watanufaika vipi.
Milongege alisema kuna taarifa kuwa kuna uwezekano utekelezaji wa kuwaondoa wafanyabiashara hao ukaanza hivi karibuni.
Alisema kwa kuwa soko hilo ni sehemu inayofanya waendeshe maisha yao,
wanatoa angalizo kwa yeyote atakayejaribu kuwaondoa kwa nguvu basi
atambue kuwa hawatakubali.
Akitolea ufafanuzi madai hayo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Mkude
alisema taarifa hizo hazina ukweli kwa sababu hakuna kikao chochote
wajumbe wa serikali ya mtaa walichokaa na kufikia uamuzi huo.
“Labda kama wanaotaka kufanya hivyo ni manispaa wenyewe, lakini
naamini kitu kama hicho hakipo, hivi ushahidi wao unatokana na nini na
kikao au walisikia tu mitaani? Vitu kama hivi haviwezekani kufanyika
kienyeji, hizi ni mali za serikali,” alisema Mkude.
Diwani Manumbu alisema hakuna mpango kama huo, na kwamba mwenye
madaraka ya kufanya hivyo ni manispaa hivyo madai yao hayana ukweli
wowote.
No comments:
Post a Comment