WAKUU wa shule za sekondari 3,001 wamehitimu mafunzo maalumu ya
kujengewa uwezo sehemu za kazi yaliyotolewa na Wakala wa Maendeleo ya
Uongozi wa Elimu (ADEM).
Walipatiwa mafunzo hayo kupitia vituo vinne kikiwemo cha ADEM Bagamoyo
yalipofungwa kitaifa na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Consolata Mgimba aliyekuwa akimwakilisha
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome.
Mgimba akihutubia wahitimu zaidi ya 700 wa kituo cha ADEM Bagamoyo
wakati wa kufunga mafunzo hayo kitaifa, aliwataka waende kufanya kazi
kwa wito na vitendo.
“Mafunzo haya ni chachu ya nyinyi kwenda kufanya kazi kwa kiwango cha
juu, kwani serikali inathamini michango na majukumu yenu ndio maana
tumewapatia mafunzo haya,” alisema Mgimba.
Alisema mafunzo hayo ni utekelezaji wa awamu ya pili ya MMES
(2010-2015) ikiwa na lengo la kuzifanya shule za sekondari zitimize
malengo yake na malengo ya kitaifa ya kuongeza ufaulu na ubora wa elimu
itolewayo.
Mtendaji Mkuu wa Chuo cha ADEM Bagamoyo, Dk. Siston Masanja,
alipongeza mafunzo hayo huku akiwataka wahitimu kwenda kuwa mfano kwa
wasaidizi wao kwenye vituo vyao vya kazi.Mafunzo hayo yalianza Septemba 23 na kumalizika juzi.
No comments:
Post a Comment