SERIKALI kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), imewapongeza
waandaaji wa Tamasha la Pasaka, Kampuni ya Msama Promotions kutokana na
ubora wake mwaka huu na kuwataka kuendeleza mipangilio hiyo.
Akizungumza katika mkutano wa kupokea ripoti na kutathimini tamasha la
mwaka huu lililofanyika kwenye mikoa mitano hapa nchini, Mkurugenzi wa
Ukuzaji Sanaa wa Basata, Nsao Shalua, alipongeza jitihada na mipango
inayofanywa na Msama katika kuliendeleza tamasha hilo.
Shalua aliongeza kuwa michango inayotolewa na kampuni hiyo kwa
jamii kupitia matamasha hayo ni mfano wa kuigwa na kuwasihi wadau
wengine kushiriki na kuchangia katika kutunisha mfuko wa matamasha ya
Pasaka.
Naye Ofisa Sanaa Mkuu, Philemon Mwasanga, alitoa wito kwa kampuni hiyo
chini ya Mkurugenzi wake, Alex Msama, mbali ya kujenga kituo cha kulea
watu wenye uhitaji maalumu ambao ni wajane, walemavu na
yatima kitakachokuwa nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, wawe na
mkakati maalumu wa kuvumbua na kuibua wasanii wachanga katika tasnia ya
muziki wa injili hapa nchini, kwa sababu muziki wa sasa umemezwa na
teknolojia.
Mwasanga aliwataka waandaaji hao kuazimia kuanzia mwakani, kuacha
matumizi ya CD wawapo jukwaani ili kuuokoa muziki ambao unapoteza
mwelekeo wake hasa kimataifa.
Aidha, Mwasanga alitumia fursa hiyo kumsihi Msama kununua vyombo vyake
vya muziki ili kufanikisha matamasha yake ili waimbaji waonyeshe vipaji
vyao katika tasnia ya muziki.
“Ili kuendana na kasi ya muziki katika hadhi ya kimataifa, unaweza
kutakiwa nchi za wenzetu, ili ukidhi inatakiwa kujipanga kimataifa
katika utayarishaji na sio matumizi ya (mshindo nyuma) CD,” alisema.
Mwasanga alisema mtindo huo umepitwa na wakati, waimbaji wanatakiwa
wajizoeze kumiliki jukwaa kwa kuimba na kupiga moja kwa moja.
Kwa upande wake, Ofisa Matukio wa Basata, Kurwijira Maregesi, alisema
matamasha yajayo yawe ni mfano wa kuigwa kinidhamu na muonekano wa
mavazi kwa waimbaji.
Maregesi alisema waimbaji wanaume wajiepushe na uvaaji wa hereni
masikioni, kusuka nywele na kuvaa suruali chini ya makalio, kwa kuwa
muziki wa injili unamtukuza Mungu.
Ili kunogesha tamasha lijalo, Ofisa wa Basata, Vick Temu alipendekeza
kuwepo kwa ‘Projector’ zitakazofungwa uwanjani ili kuwapunguzia bughudha
watazamaji watakaoukuwa mbali na jukwaa kuu.
Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo kupitia Makamu Mwenyekiti wake,
Abihudi Mang’era, ilitoa pongezi kwa Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi
katika maeneo yote ambayo matamasha yalifanyika, licha ya fununu
za matishio ya ugaidi zilizosambazwa.
Mang’era alisema tamasha lijalo litakuwa la kimataifa zaidi, kwa
sababu litaongeza idadi ya mikoa na waimbaji wa kimataifa. Kwamba lina
malengo ya kuvuka mipaka ya Tanzania na kuingia nchi za jirani.
No comments:
Post a Comment