ZAIDI ya wanafunzi 50 waliochaguliwa kujiunga katika vyuo
vikuu mbalimbali nchini kwa mwaka huu, jana waliandamana kwenda Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa lengo la kukutana na Waziri Shukuru
Kawambwa, baada ya kukosa mikopo.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumatano, wanafunzi hao walisema zaidi
ya wanafunzi 200 wenye sifa za kupewa mikopo ya elimu na Bodi ya
Mikopo (HELBS), wamenyimwa bila maelezo.
Walisema kuwa tangu mwisho wa wiki wamekuwa wakihangaika kujua sababu
za kutopewa mikopo kutoka katika bodi hiyo bila mafanikio.
Mwanafunzi Ayoub Suleiman aliyechaguliwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM), alisema kuwa wameamua kumfuata Waziri Kawambwa ili wajue ni
kwa nini hawajapewa mikopo hiyo.
Alisema majibu ya wanafunzi walioomba mikopo hiyo yalitoka Septemba
27 mwaka huu, miongoni mwao hawakuwepo kwa maelezo kuwa bajeti
imekwisha.
“Waliotupa majibu haya ni wafanyakazi wa mapokezi na walinzi pale
bodi ya mikopo, sio wahusika wenyewe kwa kuwa kila tulipoomba kukutana
na mkurugenzi, hatukupata nafasi hiyo,” alisema Suleiman.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Godwin Uledi, alisema kuwa juzi
waliwashuhudia baadhi ya wazazi wakiwa na suti na magari ya kifahari
wakifika kwenye ofisi za bodi hiyo na watoto wao, na kuingia moja kwa
moja kuonana na watendaji, walipotoka walikuwa wakitabasamu, hali
iliyoonyesha kuwa wamefanikiwa.
Alisema, wanataka wapewe sababu kwa nini hawajapewa mikopo ilhali wenzao wenye vigezo kama vyao wamepata?
“Taasisi ya vyuo vikuu nchini ‘TCU’ ilitoa mwongozo kuwa wanafunzi
wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu wakiomba vitivo vya elimu,
uhandisi, udaktari, kilimo na sayansi watapata kipaumbele katika
mikopo, hivyo nasi tulifuata mwongozo huo ili tupewe mikopo lakini
hatujafanikiwa.
“Isingekuwa tunahitaji mikopo hii tungeomba katika maeneo mengine
ambayo tulikuwa tukikidhi vigezo. Tumeomba katika vitivo hivi ili
tupate mikopo,” alisema.
Kwa upande wake mwanafunzi aliyechaguliwa katika Chuo Kikuu cha Mt.
Augustine, Revocatus Baltazary, alisema kuwa wamefungua chuo tokea
Septemba 18, lakini ameshindwa kuripoti kutokana na wazazi wake kuwa na
kipato cha chini.
“Sasa sina hata kianzio cha kwendea huko, kwa kuwa wazazi wangu hawana uwezo nitakwendaje?,” alihoji.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Ntambi Bunyazu, alisema kuwa wizara
imewasiliana na bodi ya mikopo, kwamba wanafunzi hao warudi kule
wakapewe maelezo zaidi kwa kuwa kila mmoja ana tatizo lake.
Hadi Tanzania Daima Jumatano inaondoka katika maeneo hayo, wanafunzi
hao waliambiwa waorodheshe tena majina ili wizara iyapeleke HELBS,
baada ya wiki moja watakuwa wamepata majibu.
Jitihada za kumtafuta Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na
Mawasiliano wa HELBS, Cosmas Mwaisobya, kwa ajili ya ufafanuzi wa suala
hilo, ziligonga mwamba baada ya simu yake ya kiganjani kuita kwa muda
mrefu bila majibu.
HABARI NA TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment