MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba, amewataka wanasiasa kujielekeza katika kuijadili rasimu ya
Katiba iliyotolewa badala ya kuijadili tume na wajumbe wake.
Jaji Warioba alisema tume yake siku zote imekubali kukosolewa kwa
kuamini kuwa ni jambo la kawaida lakini akaongeza kwamba ni vema
wananchi na wanasiasa wakajadili rasimu ya Katiba iliyotolewa.
“Nadhani wangezungumzia rasimu wangetusaidia sana, badala ya kuzungumzia tume na watu.
“Na siamini kama kauli za viongozi hao wa kisiasa ndiyo misimamo ya vyama vyao,” alisema.
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo jana wakati akikanusha tuhuma
zilizoelekezwa kwa tume yake na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama
cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo, kwamba tume hiyo imeacha
kutekeleza majukumu yake na kuingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni.
Alisema kuwa siku zote tume yake imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa
kuzingatia sheria na kuwataka wanasiasa hao kujadili rasimu iliyotolewa
badala ya kuishambulia tume au wajumbe wake.
“Moja ya kazi za kisheria za tume ni kutoa elimu kwa umma, na ni kazi ya wakati wote,” alisema.
Bulembo alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari juzi akiwa mkoani
Tanga ambapo alisema kuwa Tume ya Warioba imeacha kutekeleza majukumu
yake na kuingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni.
Akijibu upotoshaji huo, Jaji Warioba alisema kuwa katika mikutano ya
mabaraza ya Katiba ya Wilaya, wananchi ambao walikuwa ni wajumbe wa
mabaraza hayo walikuwa na fursa ya kuuliza maswali na wajumbe wa tume
walitoa elimu kuhusu hoja na maswali yaliyoulizwa kwa mujibu wa sheria.
“Sasa Bulembo anaona kutoa elimu ni dhambi?” aliuliza Warioba ambaye
amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri Mkuu na Makamu wa
Kwanza wa Rais.
Jaji Warioba alikumbusha kuwa tume yake imekuwa ikifanya kazi katika
mazingira magumu kutokana na kauli za wanasiasa mbalimbali na kuongeza
kuwa pamoja na kauli hizo tume yake inafarijika na kauli za kutia moyo
wanazozipata kutoka kwa wananchi wa kawaida.
“Nilisema mwishoni mwa mwezi uliopita wanasiasa wamekuwa wakitoa
matamshi yaliyoifanya kazi ya tume kuwa ngumu katika mikutano ya
mabaraza ya Katiba.
“Matamshi mengine yalilenga tume na wakati mwingine yalinilenga mimi
binafsi au wajumbe wa tume badala ya kuzungumzia rasimu,” alisema.
No comments:
Post a Comment