Watu 20 wa familia moja akiwamo Ofisa Mtendaji wa
kata katika kitongoji cha Igogo A kata ya Nyampurukano wilayani
Sengerema, wamelazwa katika Hospitali Teule ya wilaya hiyo baada ya kula
chakula kinachohofiwa kuwa na sumu.
Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja.
Watu hao wanadaiwa kula chakula hicho cha usiku Oktoba 23, mwaka huu.
Imeelezwa kwamba mara baada ya kula chakula hicho, walianza kusikia maumivu makali ya tumbo na kulazimika kukimbizwa hospitalini kwa uchunguzi na matibabu.
Aidha, baba wa familia hiyo amelazwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) kutokana na hali yake kuwa mbaya zaidi.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Mary Jose, alithibitisha kulazwa hospitalini hapo kwa watu hao tangu Alhamisi iliyopita kwa hofu ya kula chakula chenye sumu.
Hata hivyo, Dk. Jose alisema aina ya sumu iyohofiwa kuliwa na watu hao, bado haijafahamika.
''Ni kweli wagonjwa hao wapo lakini haijafahamika chanzo halisi cha matatizo yao na uchunguzi ulikuwa bado unafanywa kubaini hasa chanzo chake," alisema Dk. Jose.
Hata hivyo, alisema baadhi ya watu hao wameanza kupata nafuu lakini wengine hali zao bado mbaya.
Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Sofia Manyilizu, alisema serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola na madaktari, walikuwa wanajaribu kuchunguza chanzo cha tukio hilo.
''Mimi kama mlinzi wa amani wa kata ya Nyampurukano lilipotokea tukio, nilifika na kuchukua maelezo ya awali pamoja na orodha, ambapo jumla ya watu 20 wakiwamo na watoto, wameathiriwa na tukio hilo," alisema.
Miongoni mwa waliothiriwa na chakula hicho ni wazazi, watoto, wajukuu na vitukuu ambapo baba wa familia hiyo, Stanslaus Kisinza, hali yake bado ni mbaya.
Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, ambaye yuko mkoani Shinyanga kikazi, alitoa pole kwa familia hiyo na kusisitiza kuwa tukio hilo ni lazima lifanyiwe uchunguzi wa kina.
"Taarifa za tukio hili nimezipata leo (jana), baada ya kuwasili mkoani hapa (Shinyanga) kikazi nikitokea Dar Salaam na kwa hakika limenishtua sana," alisema.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment