Zitto Kabwe.
SASA ni dhahiri kwamba Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kinameguka na kubaki vipande, kutokana na uamuzi uliochukuliwa jana na
Kamati Kuu yake kuwavua rasmi madaraka vigogo wake watatu. Mkutano wa
siku mbili wa Kamati Kuu ya chama hicho uliofanyika Dar es Salaam
hatimaye jana ulimalizika kwa kuchukua hatua dhidi ya Naibu Katibu Mkuu,
Zitto Kabwe, Mjumbe wa Kamati Kuu,
Dk Kitilla Mkumbo na aliyekuwa
Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Baada ya hatua hiyo ambayo ni ngumu kuaminika ndani na nje ya chama
hicho kikuu cha upinzani, zilipatikana taarifa zingine za Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Said Arfi kujiuzulu wadhifa huo.
Kwa
hatua hiyo, viongozi hao wamevuliwa nyadhifa zao zote za uongozi ndani
ya chama kutokana na tuhuma za kuunda mtandao wa kukivuruga chama hicho
na kuiagiza Kamati ya Chama ya Wabunge kuchukua hatua za haraka
kuhakikisha Zitto anavuliwa madaraka yake yote ya Naibu Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Hayo yalibainishwa jana na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu alipokuwa akitoa uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Alisema
uamuzi mwingine ni pamoja na viongozi hao kuandikiwa hati zenye tuhuma
dhidi yao haraka na watakiwe kujieleza kwa nini wasifukuzwe chama kwa
vitendo vyao, ikiwa ni pamoja na kupewa fursa ya kujitetea kama
inavyoelekezwa kwenye Katiba ya chama.
Lissu alisema Kamati pia imetaka baada ya utekelezaji wa azimio,
ikutane kwa kufanya uamuzi juu ya hatma ya watuhumiwa na hatua zingine
zitakazofuata.
Mtandao wa ushindi Akizungumza kilichojiri katika
mkutano huo hata kufikia uamuzi huo, alisema ilibaini kuwapo mkakati wa
kukiharibu chama kupitia waraka uitwao “Mkakati wa Mabadiliko 2013”
ulioandaliwa na kikundi kinachojiita “Mtandao wa Ushindi”.
Alisema kikundi hicho vinara wake wakuu ni wanne ambao ni Zitto
anayejulikana kama ‘MM’ au Mhusika Mkuu, Dk Mkumbo anayejulikana kama
M1, Mwigamba anayejulikana kama M3 na mtu mwingine ambaye jina lake
halijajulikana anayejulikana kama M2.
Alisema M2 anatajwa kwenye
waraka huo kuwa yuko ukingoni kuondolewa katika mageuzi ya kiutendaji
yanayoendelea katika Sekretarieti ya Chama Makao Makuu. “Kwa mujibu wa
waraka wenyewe, mkakati huu umeandaliwa pamoja na M2 na M3 na kupitiwa
na kurekebishwa na M1 ili upelekwe kwa MM kwa maoni ya mwisho na kuanza
utekelezaji,” alisema.
Lissu alisema mbele ya Kamati Kuu, Dk Mkumbo
alikiri kuwa MM ni Zitto, M1 ni yeye na M3 ni Mwigamba na kukataa
kumfahamu M2 na kukiri yote yaliyoandikwa katika Mkakati wa Mabadiliko
2013 ni ya kwao.
Alisema lakini Zitto alikana kuuona waraka huo na kumhusu kwa kuwa
ametaja tu jambo ambalo Kamati Kuu ilikataa kutokana na kuwa Juni 30
waraka huo ndio ulihaririwa mara ya mwisho na kupelekwa kwa Zitto kwa
ushauri na utekelezaji.
Lissu alisema mkakati huo ni wa kuipasuapasua
Chadema na kuiangamiza kabisa kwenye uso wa siasa za nchi na si wa
kufanya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya chama kwa njia ya kidemokrasia
na kikatiba.
“Huu ni mpango wa kukiteka nyara chama na kukiua, ndiyo maana
wamesema kwenye waraka kuwa mkakati huo unahitaji kutekelezwa kwa siri
kubwa, ili mkuu aliyepo aendelee kubweteka na ndiyo maana hata lugha
iliyotumika ni ya kipekee,” alisema.
Alisema walipanga vikao vifanyike mara chache tena vya faragha
ikiwezekana hata nje ya nchi, huku M1 akiwasiliana na wanayemtaka na
kusiwe na mawasiliano ya ujumbe mfupi bali kuonana ana kwa ana au
kuzungumza kwa simu.
Alisema mtandao huo umekwenda kinyume na Katiba
kwa kuonesha wazi kwa mtu wanayemtaka kwa kuwa Zitto ni Mwislamu,
itakuwa fursa kuungwa mkono na wanachama Waislamu ambao wamekuwa na
kigugumizi wakidhani hawatakiwi ndani ya chama.
Huku akibainisha kuvunja Katiba katika ibara mbalimbali ikiwamo
kutokuwa wawazi katika mkakati wao, kutoa tuhuma dhidi ya kiongozi bila
kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye
kanuni.
“Kutokana na hali hiyo, wamevumiliwa sana, lakini hakuna
taasisi au chama duniani inayoweza kunyamazia mikakati kama hiyo dhidi
yake na viongozi na kubaki salama, lakini sasa uvumilivu una kikomo na
hiki ndicho kikomo,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa wakati wa kikao
hicho, Zitto na Dk Mkumbo waliiomba Kamati Kuu kujiuzulu nyadhifa zao,
lakini kwa kuzingatia uzito wa makosa waliyofanya Kamati ilikataa, kwani
kufanya hivyo ingekuwa kuruhusu wajiondoe kwenye uongozi wakiwa na
heshima wasizostahili.
Mbowe anena Akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari,
Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe alisema hawatakubali chama
kibaki kwa sababu fulani na kwa uamuzi huo, kitabaki salama na kuendelea
kuimarisha na kuwa mashuhuri kuliko sasa.
Alisema chama ni muhimu kuliko mtu yeyote na kikifanyiwa mchezo
itachukua miaka zaidi ya 20 kupata chama kama ilivyo Chadema na
hawajapata mtu wa kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu.
Alisema chama hicho hakina ukomo wa uongozi na yeye ataendelea kuwa Mwenyekiti ikiwa bado wanachama wanamkubali na wakitaka kumwondoa atatoka kwani hayuko katika chama kutafuta fedha, kwani anazo ila yupo kwa ajili ya uzalendo wa nchi tu.
Alisema chama hicho hakina ukomo wa uongozi na yeye ataendelea kuwa Mwenyekiti ikiwa bado wanachama wanamkubali na wakitaka kumwondoa atatoka kwani hayuko katika chama kutafuta fedha, kwani anazo ila yupo kwa ajili ya uzalendo wa nchi tu.
Alitoa onyo kwa anayetaka kuibomoa Chadema kwamba atabomoka yeye huku
akiweka bayana kuwa chama hakihusiki wala hakiutambui waraka ulioko
mitandaoni. Arfi ajiuzulu Katika kuongeza chumvi kwenye kidonda, Makamu
Mwenyekiti wa Chadema Bara, Said Arfi naye ametangaza kujiuzulu wadhifa
huo kuanzia jana, kwa alichosema ni kuchoshwa na unafiki ndani ya chama
hicho.
Taarifa yake kwa vyombo vya habari jana iliyonakiliwa kwa Mbowe,
Zitto na Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa, Mbunge huyo wa Mpanda Mjini
alisema muhimu kwake ni maslahi ya wapiga kura, wakazi na wananchi wa
Mpanda Mjini na wilaya ya Mpanda kwa jumla na hayuko tayari kuchaguliwa
marafiki.
“Kwa kipindi kirefu zimekuwapo shutuma dhidi yangu na kutiliwa shaka
uhusiano wangu na Pinda (Mizengo) Waziri Mkuu, pamoja na kunijadili
katika vikao kadhaa Mpanda na Dar es Salaam, bado kuna shaka kwa nini
alipita bila kupingwa; huo ulikuwa uamuzi wa wana Mpanda.
“Hamsemi kwa nini majimbo mengine 16 nchini yalipita bila kupingwa
mlikuwa wapi na nani alaumiwe, huu ni unafiki wa kupindukia,” alisema
Arfi.
Aliwaambia viongozi wenzake, kuwa wamechukizwa kwa nini alihoji kauli
ya muasisi wa chama hicho, Edwin Mtei, “kutuchagulia viongozi, naomba
ifahamike wazi kuwa huu ni mtazamo wangu na utabaki hivyo siku zote, kwa
chama cha demokrasia kutoruhusu uongozi wa kiimla kwa kukidhi matakwa
ya waasisi ambao huvigeuza vyama mali binafsi.”
Alisisitiza kuwa kwake kusimamia ukweli daima litabaki kuwa lengo lake katika maisha yake siku zote hata kama utamgharimu maisha.
Alisisitiza kuwa kwake kusimamia ukweli daima litabaki kuwa lengo lake katika maisha yake siku zote hata kama utamgharimu maisha.
HABARI NA HABARI LEO
No comments:
Post a Comment