Rais wa TFF aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga (kulia) akimkabidhi baadhi ya nyaraka Rais Mpya, Jamal Malinzi.
Rais wa TFF aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga akiongea wakati wa
hafla ya makabidhiano. Kushoto ni Rais Mpya wa TFF, Jamal Malinzi.
TANZANIA FOOTBALL FEDERATION
HOTUBA YA RAIS WA TFF KWENYE HAFLA YA MAKABIDHIANO
TAREHE 02 NOVEMBA 2013
Ndugu mgeni rasmi ……..…………………………………………….
Ndugu…………………………………. Mwakilishi wa Wizara
Ndugu…………………………………. Mwakilishi wa BMT
Ndugu…………………………………. Mwakilishi wa wadhamini
Ndugu Leodegar Tenga Rais aliyemaliza muda wake
Ndugu Said El Maamry Mwenyekiti mstaafu wa iliyokuwa FAT
Ndugu Muhidin Ndolanga Mwenyekiti mstaafu wa
iliyokuwa FAT
Wajumbe wa Baraza la Wadhamini
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji
Wafanyakazi wa TFF
Wageni waalikwa
Mabibi na Mabwana
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwa hapa leo.
Awali ya yote naomba nichukue fursa hii kukupongeza Rais wetu
uliyemaliza muda wako Ndugu Leodegar Tenga na Kamati yako ya utendaji .
Mliyoufanyia mpira wa Tanzania ni makubwa, historia haitawasahau.
Mmetujengea taasisi imara isiyotetereka, taasisi inayoheshimika ndani na
nje ya mipaka ya nchi hii, nawashukuru na kuwapongeza sana.
Uchaguzi umekwisha. Mchakato ulikuwa mrefu. Wapo walioshinda na wapo
ambao kura zao hazikutosha. Wote tuna kazi moja tu kujenga mpira. Kama
tulikwaruzana kwenye kampeni tusameheane, tuwe kitu kimoja, tuinyanyue
soka yetu. Makundi hayajengi yanabomoa, tuachane nayo.
Ndugu zangu, uongozi wetu ulioingia madarakani alfajiri ya tarehe
28-11-2013 unakabiliwa na changamoto nyingi. Nitaelezea changamoto
chache zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
- 1. Mashindano yanayotukabili.
Tunakabiliwa na mashindano mbalimbali ya kimataifa. Mfano ni mechi ya
marudiano ya U/20 wanawake dhidi ya Msumbiji wiki ijayo, Mitoano ya
mashindano ya Afrika wanawake mapema mwakani, Mashindano ya Chalenji
Novemba mwaka huu, na mashindano ya kufuzu AFCON 2015. Yote haya
yanahitaji maandalizi ya haraka.
- 2. Programu ya vijana.
Ilani yangu ya uchaguzi ilielezea azma ya Tanzania kuomba uenyeji wa
fainali za vijana za Afrika U/17 mwaka 2019. Jambo hili tutalizungumzia
kwenye kikao chetu cha utendaji leo. Ili tuwe na timu nzuri ya kucheza
fainali hizo tukiwa wenyeji hatuna budi mwaka kesho kuunda timu ya Taifa
ya U/12 itakayokua pamoja kuelekea 2019. Programu yetu ya vijana
tutakayoiandaa sharti ijielekeze kwenye ratiba hii.
- 3. Udhamini wa timu za vijana na za wanawake
Hii ni changamoto kubwa sana kwa TFF. Timu zetu za Taifa kuanzia zile
za wakubwa hadi za vijana ni brands, na kama ni brands inabidi
ziingizwe sokoni, ziuzwe kwa tunaodhamiria wawe wadhamini wa hizo timu.
Kitengo cha masoko lazima kiimarishwe ili kukabiliana na changamoto
hizi. Mdhamini ni mfanyabiashara, anapotoa pesa kudhamini brand fulani
anategemea matokeo mazuri kwake kwa njia ya kukuza biashara zake. Twende
kwa wadhamini tuwashawishi waone watafaidikia nini (leverage) kwa
kudhamini timu zetu. Tusisubiri waje tuwafuate sisi.
- 4. Uwekezaji
Jitihada za haraka lazima zifanyike kuiongezea TFF uwezo wa kiuchumi.
Ni muhimu mtaalam mshauri (consultant) atafutwe atufanyie mchanganuo wa
uwekezaji katika ardhi yetu hii ya Karume ili tuwekeze kitega uchumi
kama ilivyokubaliwa kwenye mkutano mkuu. Aidha bidhaa zenye nembo yetu
zianze kuuzwa kwa utaratibu maalum ili shirikisho lipate haki yake.
Kabla sijamaliza kuzungumza, niongelee suala la fujo viwanjani. Mpira
ni dakika tisini. Katika kipindi hicho uamuzi wa mwamuzi unakuwa ni wa
mwisho. Tusifiche upungufu wa timu zetu kwa kujificha nyuma ya kivuli
cha mwamuzi. Waamuzi wakionekana wamefanya makosa yawe ya makusudi au ya
bahati mbaya vyombo vya kuwahukumu vipo, mahakama ya waamuzi sio
mashabiki. Kitendo cha mashabiki kufanya fujo kabla, wakati na baada ya
mechi ya mpira kamwe hakikubaliki mahali popote duniani. Kanuni za
FIFA, CAF na TFF ziko wazi na adhabu zinajulikana. Moja ya adhabu hizi
ni timu husika kucheza kwenye uwanja mtupu usio na mashabiki kama
ilivyowatokea Al Ahly na Zamalek huko Misri au kucheza nje ya uwanja
wako kama ilivyowatokea Senegal ambao baada ya vurugu Dakar, Senegal
waliamriwa na FIFA mechi zao za nyumbani wachezee nje ya nchi na
wakachagua kuchezea Morocco.
Ndugu zangu yaliyotokea majuzi Mbeya na Dar es salaam wote
tumeyasikia na wengine miongoni mwetu hapa ni mashuhuda. Ninasema iwe
mara ya kwanza na y a mwisho. Kwenye masuala ya kutekeleza mahitaji ya
kanuni uongozi wangu hautaionea haya klabu yoyote, iwe mpya au kongwe
kwenye ligi yetu. Ni jukumu la viongozi wa klabu kudhibiti wanachama na
wapenzi wao. Tabia ya benchi la ufundi kutoa matamshi yanayoweza kuamsha
hisia za mashabiki ni kinyume na taratibu na kanuni ziko wazi kuhusu
jambo hili. Viongozi wa klabu na mabenchi yao ya ufundi wakishindwa
kutekeleza wajibu wao tusilaumiane.
Ndugu zangu ya kufanya ni mengi katika kuiendeleza soka yetu.
Tunashukuru Mungu kuwa uwezo wa kukabiliana na changamoto hizi tunao na
tuna ari na nia ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mpira. Ombi
langu kwenu nyote ninaomba ushirikiano wa wadau wote kuanzia Serikali,
Halmashauri, mashirika ya umma na binafsi na NGO’s, nina imani
tukishikamana tutaifikia ndoto yetu ya kuing’arisha Tanzania kimpira
kwenye anga za dunia.
Ahsanteni nawashukuru sana.
TAARIFA YA MAKABIDHIANO YA OFISI YA TFF YALIYOFANYIKA KATIKA OFISI ZA TFF JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 2 NOVEMBA 2013
Mheshimiwa Rais wa TFF,
Pongezi na Shukurani
1. Naomba nianze kwa kushukuru kwa kukubali kufanyika kwa
shughuli hii ya makabidhiano ya Ofisi. Utaratibu huu haupo kikatiba wala
katika kanuni zetu, lakini ni muhimu sana kwa vile unatoa taswira ya
uongozi endelevu na ushirikiano unaostahili kuwepo baina ya uongozi mpya
na ule wa zamani.
2. Aidha napenda, kwa mara nyingine, kukupongeza kwa dhati
wewe binafsi kwa kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa Shirikisho letu pamoja
na kumpongeza Makamu wa Rais na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa
ushindi wao.
3. Tumeshuhudia mchakato wa uchaguzi uliofanyika kwa uwazi,
na ulio huru na wa haki. Ninawashuru sana na kuwapongeza Wajumbe wa
Kamati ya Uchanguzi kwa ueledi na kazi nzuri walioifanya. Kwa kiwango
hicho hicho ninawapongeza na kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi na wa Kamati za Maadili – ngazi ya awali na ya rufani – kwa
kutekeleza wajibu wao kikamilifu na vyema.
4. Nawajibika kutoa pongezi kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa
kukamilisha kazi muhimu ya kutuchagulia viongozi wetu kwa utulivu
mkubwa.
5. Utulivu wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi – kuanzia
mwanzo hadi mwisho – ni kielelezo cha ukomavu wa uongozi wa mchezo wa
mpira wa miguu nchini. Natoa shukurani za dhati kwa wanachama na wadau
wote wa mpira wa miguu nchini kwa mchango wao wa hali na mali katika
kufanikisha zoezi hili muhimu kwa mustakabali wa mpira wa miguu nchini.
Dira na Malengo ya Uongozi Uliopita
6. Dira ya uongozi uliopita ilikuwa ni kujenga mazingira
mazuri na endelevu ya maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu nchini. Hii
ilitokana na hali ya migogoro isiyoisha na malumbano ya mara kwa mara
yaliyokuwepo kabla ya kuingia madarakani.
7. Ili kufanikisha dira yetu, uongozi uliopita ulidhamiria
kujenga msingi bora wa uongozi wa mpira wa miguu nchini, hivyo kujiwekea
malengo yafuatayo:
- Kutengeneza Katiba mpya na Kanuni zitakazokidhi mahitaji ya nchi yetu ya kudumisha demokrasia na utawala bora – uwazi, uwajibikaji, na kadhalika.
- Kuhakikisha kuwa Katiba yetu na Kanuni zetu zinazingatiwa na kuheshimiwa.
- Kuweka Kanuni za Fedha na kuchukua hatua za kujenga uaminifu katika usimamizi wa ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya fedha. Tuliazimia kuona hesabu za Shirikisho zinakaguliwa na wakaguzi wenye sifa za kimataifa, na taarifa ya ukaguzi kuwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu kila mwaka, bila ya kukosa.
- Kuwa na mfumo wa mashindano utakaongeza ushindani na kuchochea uwekezaji. Azma ilikuwa ni kuongeza idadi ya mashindano ili kutoa fursa kwa vipaji kuonekana na kuendelezwa.
- Kuweka jitihada katika mafunzo ya wataalamu wa mpira wa miguu nchini kwa kuongeza idadi na kozi/semina za mafunzo ya uongozi, uamuzi, ualimu na udaktari wa michezo.
- Kujenga mfumo mpya wa uongozi wa timu za taifa. Lengo lilikuwa ni kuhakikisha kuwa timu za taifa zinakuwa na uongozi wake chini ya Mwalimu/Walimu wa timu ya taifa na kuzitofautisha na Idara ya Ufundi, pamoja na kuhakikisha timu zetu za taifa zinashiriki michezo mingi iwezekanavyo ya mashindano na ya kirafiki.
- Kujenga uhusiano mzuri na wadau na washirika wetu, hususan wadau wetu wakuu ambao ni Serikali na vyombo zake; Mashirikisho ya mpira tuliyojumuika nayo - FIFA, CAF, na CECAFA; Wadhimini na Wafadhili wetu – kampuni, mashirikia ya umma na watu binafsi - wanaochangia maendeleo ya mpira wa miguu nchini kwa hali na mali.
- Kuwa karibu na jamii na kuisaidia jamii. Nia ni kutumia umaarufu wa mchezo wa mpira wa miguu nchini kuhamasisha maendeleo ya jamii, hasa katika masuala ya afya ya jamii – kampeni ya malaria, ukimwi, kupambana na madawa ya kulevya na kadhalika. Rais anayeondoka madarakani ni Balozi wa Malaria nchini na Rais wetu mpya ni mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Malaria, chini ya Uenyekiti wa Waziri wetu wa Afya, Mheshimiwa Hussein Mwinyi.
8. Utekelezaji wa Dira tuliyojiwekea na malengo yetu
ulifanyika kwa ushirikiano wa karibu na wanachama na wadau wetu.
Yaliyofanyika yanajulikana. Itoshe kusema kuwa kazi hiyo ilifanyika kwa
jitihada kubwa na uadilifu mkubwa na kwamba malengo tuliyojiwekea
yalifikiwa.
9. Katika hotuba niliyoitoa katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu
uliopita – Jumamosi, tarehe 26 Oktoba 2013, niliainisha kwa kina nini
kilifanyika katika kipindi cha uongozi uliopita pamoja na mafanikio ya
kazi iliyofanyika. Napenda kuimbatanisha hotuba hiyo kama sehemu ya
taarifa hii ya makabidhiano.
10. Matarajio yetu ni kuwa, baada ya jitihada za kuweka msingi
wa uongozi na wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini, nguvu itaelekezwa
katika kukuza kiwango cha mpira wa miguu nchini mwetu. Tulichokifanya ni
kutayarisha Mpango wa Muda Mrefu wa Maendeleo ya Mpira Miguu Nchini – 2013 hadi 2016 (Long Term Technical Development Plan – 2013 to 2016), ambayo umeambatanishwa kama sehemu ya taarifa hii ya makabidhiano.
11. Hivyo basi, uongozi mpya una kazi ya kusimamia na
kufanikisha utekelezaji wa Mpango huo. Pia, ni matarajio yetu kuwa
uongozi mpya utayadumisha mambo ya msingi tuliyojiwekea na kuufanyia
kazi upungufu uliopo.
Shukurani kwa Wanachama na Wadau wa TFF
12. Pamoja na kuwa nimeshatoa shukurani mara kadhaa, napenda
kwa mara nyingine tena kuwashukuru wote waliotusaidia kufika hapa
tulipo. Nawashukuru sana wanachama wetu, wadau wetu wote – Serikali yetu
na vyombo vyake vyote, wadhamini na wafadhili, waandishi na vyombo vya
habari, wapenzi wa mpira na wananchi kwa ujumla kwa mchango wao wa hali
na mali. Bila yao tusingefika hapa tulipofika.
13. Shukurani maalum zimwendee Mheshimiwa Rais wetu, Dk. Jakaya
Mrisho Kikwete, kwa mchango wake usiopimika. Alikuwa ni sehemu
mabadiliko haya tangu mwanzo, hata kabla ya uongozi wetu kuingia
madarakani. Ametusaidia kwa kiasi kikubwa kuzijenga timu zetu za taifa
siyo tu kwa uamuzi wake wa kulipia mishahara ya walimu wa timu ya taifa,
bali pia kwa kuwahamasisha vijana wetu kwa hali na mali wafanye vizuri.
Sina hakika kuwa yupo Rais mwingine, popote pale duniani, aliye karibu
na mapenzi ya dhati kwa vijana wa timu zake za taifa zaidi ya Rais wetu.
Zaidi ya hayo, Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele katika
kuhamasisha utawala bora katika mpira wa miguu nchini na amefanya kila
aliloliweza kuona kuwa kiwango cha mchezo kinapanda na timu zetu
zinafanya vizuri. Napenda kutoa shukurani za dhati kwake kwa uongozi na
msaada wake.
Wanachama, Katiba na Kanuni, Wafanyakazi, Mali na Mikataba ya TFF
14. Wanachama
TFF ina jumla ya Wanachama 44 ambao wote ni wanachama hai kama ifuatavyo:
- Vyama vya Mikoa – 25
- Vyama Shiriki - 5
- Vilabu vya Ligi Kuu - 14
15. Katiba na Kanuni
Hivi sasa TFF ina Katiba Mpya (ya Mwaka 2013) iliyofanyiwa
marekebisho ya mwisho na Mkutano Mkuu Maalum wa TFF tarehe 13 Julai
2013.
Pamoja na Katiba TFF ina kanuni zifuatazo ambazo kwa mujibu wa Katiba ya TFF hupitishwa na kamati ya Utendaji:
- Kanuni za Fedha
- Kanuni za Mashindano kuanzia Ngazi ya Wilaya hadi Ligi Kuu
- Kanuni za Utii
- Kanuni za Nidhamu
- Kanuni za Maadili
- Kanuni za Uchaguzi za Uchaguzi za TFF na za Wanachama wa TFF
- Kanuni zinazosimamia Uendeshwaji wa Bodi ya Ligi Kuu
- Kanuni za Mashindano mengine, kama vile Copa Coca Cola, Uhai Cup, Super 8 na Taifa Cup. Ni vyema ikafahamika kuwa kila mashindano lazima yawe na Kanuni zinazosimamia uendeshwaji wake.
TFF inalazimika kuzifanyia marekebisho Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wake kufuatia marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi za TFF. Aidha,
TFF inadeni la kutayarisha Kanuni za Chombo cha Usuluhishi (Arbitration
Tribunal) kama ilivyoainishwa katika Katiba. Hivi karibuni, TFF
imepokea Kanuni za Mfano kutoka FIFA ambayo ipo haja ya kazi hii
kukamilishwa na uongozi mpya.
16. Wafanyakazi wa TFF
Hivi sasa TFF ina jumla ya wafanyakazi 29. Kati yao yupo/wapo
- Katibu Mkuu - 1
- Wakurugenzi / Maofisa Mwandamizi - 5
- Wafanyakazi wengine - 23
Katibu Mkuu na Wakurugenzi wapo katika kipindi cha nyongeza cha miezi
sita (6) cha mikataba yao, kinachoishia mwishoni mwa mwezi Desemba
2013. Wafanyakazi wengine wapo katika mikataba ya miaka minne yenye
kipindi cha majaribio cha miezi sita kuanzia mwanzoni mwa mwezi Septemba
2013. Hivyo basi, uongozi mpya una nafasi ya kufanya tathmini ya
mahitaji ya TFF kisha kufanya uamuzi juu ya ajira za Wafanyakazi waliopo
kadiri utakavyoona inafaa.
TFF ilichukua hatua ya kuingia kufanya makubaliano ya hiari na
wafanyakazi wake ili kuondokana na ajira za maisha (Permanent
Employment) na kubaki na ajira za mikataba (Contract Empoyment) kwa
wafanyakazi wake wote.
Wafanyakazi wa TFF wamekuwa wakifanya kazi ngumu na saa nyingi kuliko
kawaida. Ajira ya TFF haina saa za ziada wala siku za mapumziko.
Kutokana na dhana ya kujitolea na ukweli kwamba shughuli nyingi za TFF,
kama vile michezo na mikutano hufanyika siku za mwisho wa wiki na
sikukuu, ni dhahiri kuwa Wafanyakazi wa TFF wamekuwa wakilazimika
kufanya kazi siku hizo, na mara nyingi bila malipo ya saa za ziada.
Aidha, kutokana na kukosa uwezo, uongozi uliopita ulishindwa kupandisha
mishahara yao ipasavyo.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru kwa kuihudumia
TFF na mpira wa miguu katika mazingira magumu sana. Tunauomba uongozi
mpya uliangalie suala hili kwa umakini, kama moja ya hatua za kuongeza
ufanisi wa Sekretariati.
17. Mali za TFF
Hivi sasa TFF ina mali zifuatazo:
- Kiwanja cha Karume Stadium, chenye hati namba 27026 iliyotolewa tarehe 10 Novemba 1981. Kiwanja cha Karume kina ukubwa wa ekari 8.26. Ombi la kuingezea muda hati hiyo limeshapelekwa na linafuatiliwa.
- Ndani ya Kiwanja hicho, kuna Jengo la ofisi ya TFF, Jengo la Kituo cha Ufundi (Technical Centre) na Uwanja wa nyasi za bandia wa Karume.
- Kiwanja cha Tanga chenye ukubwa wa hekta 7.6 (ekari 19) kilichopo katika eneo zuri sana mjini Tanga. Kiwanja hiki tayari kimeshalipiwa na hivi sasa taratibu zinaendelea kukamilisha taratibu za kukiandikisha na kupata hati.
- Magari sita (6) na Trekta moja (la kusafishia uwanja wa nyasi bandia). Magari hayo ni: Bus kubwa aina ya Yutong, basi dogo aina ya Coaster, magari ya aina 4WD Ford Everest, Rav 4, Suzuki Escudo na Honda CVR. Mawili kati magari hayo - Suzuki Escudo na Honda CVR – yanatumika lakini hayapo katika hali nzuri. Ni vyema uongozi mpya ukayafanyia tathmini magari hayo na kufanya maamuzi muafaka kadiri utakavyoona inafaa.
- Fedha taslimu Shilingi 33,518,000 na US$ 1,390 zipo katika akaunti hivi sasa. Hii ni baada ya TFF kufanya malipo ya Shilingi 158,000,000 kwa ajili ya Mkutano Mkuu (uliofanyika wiki iliyopita) na malipo ya Shilingi 56,240,000 yaliyofanyika kwa ajili matayarisho ya Timu ya Taifa ya Wanawake U-20 na gharama za mchezo baina ya timu yetu ya Taifa na ile ya Msumbiji uliofanyika wiki iliyopita. Hata hivyo, leo hii US$ 415,000 (Shilingi 664,000,000) kimehamishwa kutoka kwenye Akaunti za TBL kwenda kwenye Akaunti za TFF. Fedha hizo zitakuwa tayari kwenye Akaunti ya TFF ifikapo Jumanne wiki ijayo. Malipo haya yalikuwa yafanyike karibu miezi miwili iliyopita lakini yalicheleweshwa ili kutoa nafasi kwa zoezi la ukaguzi wa fedha za udhamini wa TBL kufanyika. Zoezi limefanyika vyema na kufikia ukingoni, ndiyo maana malipo yamefanyika. Malipo mengine yanayofanana na hayo, ya US$ 420,000 (Shilingi 672,000,000) yanatarajiwa kufanyika wiki mbili kutoka sasa - katikati ya mwezi huu wa Novemba 2013.
Hivyo basi, uongozi unaoingia madarakani hautaanza kwa shida. Ni
matarajio yetu kuwa hatua ya awali itakuwa kurejesha fedha kwenye
akaunti zilikoazimwa kinachofikia US$ 166,509 - US$ 148,174 kutoka
kwenya Akaunti za FAP na US$ 18,335 kutoka kwenye Akaunti ya TRA - kwa
ajili ya kugharimia Mkutano Mkuu na matumizi ya Taifa Stars kwa ajili ya
matayarisho na safari ya kwenda Gambia.
Ili kujiridhisha kuwa fedha za udhamini zinatumika kama
ilivyokubalika katika mikataba, TFF imetoa nafasi kwa wadhamini kufanya
ukaguzi wa fedha inazozitoa wakati wowote ule. Utamaduni huu tumekuwa
nao katika kipindi chote cha utawala wa uongozi wetu, ili kutoa imani
kwa wadhamini na kuhakikisha kuwa malengo ya udhamini husika
yanafanikiwa. Huu ni utaratibu mzuri na ni matumaini yetu kuwa
utadumishwa.
Jengo la Kituo cha Ufundi ndiyo kwa limekamilika kukarabatiwa na bado
halijafunguliwa rasmi. Ukarabati huo umefanikisha kutengenezwa kwa
mfumo wa maji machafu unaojitegemea. Hivyo, kutohitaji kutengemea
mashimo ya Jengo la Ofisi za TFF. Hatuo ya mwisho ya kazi hiyo ni
kukamilisha ukaguzi wa matumizi yaliyofanyika katika ukarabati huo na
kuiwasilisha CAF mapema iwezekanavyo. Hayo ndiyo makubaliana kuhusiana
na msaada uliotolewa na CAF – unaojulikana kama CAF FAP 2.
Ukarabati wa Kituo cha Ufundi umefanywa, pamoja na sababu nyingine,
ili kutoa fursa kwa Mradi wa Ujenzi wa Karume kuendelea. Kama
nilivyoeleza katika Mkutano Mkuu, dhamira ni kuwekeza katika Mradi wa
Ujenzi wa jengo / majengo yenye hadhi kubwa kwa ajili ya kukodishwa
kuzunguka uwanja huo. Jengo lililo karabatiwa na uwanja wa mpira
vitabaki na kuendelea kutumiwa kama Kituo cha Mafunzo. Jambo la muhimu
ni kuhakikisha kuwa uwekezaji katika mradi huo hauhitaji dhamana ya
uwanja wetu na majengo yetu. Ni imani yetu kuwa njia muafaka
inapatikana, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa ‘Build, Operate and
Transfer’ (BOT).
18. Hesabu za TFF
Ripoti ya Ukaguzi wa hesabu za TFF hadi kufikia Desemba 2012
iliwasilishwa katika Mkutano Mkuu uliopita. TFF ilipata Hati Safi ya
Ukaguzi wa hesabu zake na Mkutano Mkuu ukaikubali na kuipitisha ripoti
hiyo hesabu za mwaka 2012. Aidha, taarifa ya hesabu za TFF kwa kipindi
cha kuanzia tarehe 1 Januari hadi 30 Septemba 2013 kusambazwa kwa
Wajumbe wa Mkutano Mkuu.
Ifahamike kuwa TFF imekuwa ikipata Hati Safi, kila mwaka katika
kipindi cha miaka minane iliyopita. Hatuna shaka kuwa hali hii
itaendelea.
19. Mikataba ya Udhamini
TFF inayo mikataba ifuatayo ya udhamini na Wadhamini wafuatayo:
- Vodacom – Udhamini wa Ligi Kuu
- TBL – Taifa Stars
- Coca Cola – Mashindano ya Copa Coca Cola
- SSB & Co – Mashindano ya Uhai
- Bank ABC – Super 8
- Azam Media – Haki za Matangazo ya Television kwa Ligi Kuu
Aidha, baadhi ya vilabu kama vile Yanga na Simba vinadhaminiwa na
TBL, Coastal Union inafadhiliwa na Tanga Cement na Azam FC inadhaminiwa
na Azam Cola.
Changamoto zinazoikabili TFF
20. Zipo changamoto nyingi zinazoikabili TFF lakini kubwa kwa
maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu na ambazo uongozi mpya hauna budi
kuzishughulikia ni ulazima wa:
- Kuendeleza sola la vijana na watoto kwa kutoa fursa kwa watoto/vijana wengi kupata malezi mazuri ya uchezaji wa mpira wa miguu ili kupanua wigo wa kupata wachezaji wenye vipaji. Katika jambo hili bado tuko nyuma sana. Tulididimia sana kutokana na kufutwa kwa michezo mashuleni. Ipo haja ya uongozi mpya kushirikiana na Serikali kuhamisha michezo shuleni, kama hatua ya wali ya kutatua tatizo la soka la vijana/watoto.
- Kuendeleza soka la wanawake. Matatizo ya soka la wanawake yanafanana na ya soka la vijana. Tofauti ni ndogo sana. Kama ilivyo kwa soka la vijana, hatua muhimu kufanyika kwa jitihada ya kuwahamasisha wasichana wacheze mpira wa miguu shuleni.
- Kuhakikisha ueledi unazingatiwa katika uongozi wa Vilabu na Vyama Wanachama wa TFF. Kinyume chake hatutaweza kushindana na wenzetu ambao walishapiga hatua katika taaluma ya uongozi wa michezo. Vilabu vyetu ni lazima vihakikishe kuwa vinatimiza masharti ya ‘Club Licencing’ kama yalivyotolewa na CAF, pamoja na marekebisho yake. Huu ni mtihani kwetu. Ni lazima tufaulu kutimiza masharti hayo, vinginevyo tutabaki nyuma. Ipo haja ya kuuangalia kwa mfumo wa uongozi wa Vilabu vyetu na Vyama Vyetu kwa azma ya kubuni mfumo utakaotuletea ufanisi zaidi wa kiungozi na uendeshaji kuliko ilivyo hivi sasa.
- Kuhamasisha uwekezaji katika maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu nchini. Tuna upungufu mkubwa wa vifaa na viwanja vya kuchezea. Ni vigumu kuundeleza mchezo wa mpira bila ya kuwa na viwanja vya kuchezea na vifaa. Aidha, zinahitajika raslimali watu na fedha katika kulea na kuwaendeleza wachezaji na wataalamu wetu. Licha ya hapo kiasi kikubwa cha fedha kinahitajika kwa ajili ya matumizi mengine ili timu ifanye vizuri. Kwa maneno mengine tunahitaji kufanya kila jitihada kuhamasisha watu binafsi, makampuni na Serikali iwekeze katika mpira, wadhamini zaidi wajitokeze na wapenzi wengi zaidi wachangie timu zao – kwa njia mbalimbali - ili kuongeza mapato ya vilabu na vyama husika. Vilabu vyetu na Vyama Wanachama wa TFF vinakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha za uendeshaji. Mawazo au fikra kuwa kuna fedha nyingi katika mpira wa miguu ni dhana isiyo na msingi na inayotokana na kutofahamu gharama za uendeshaji wa vilabu na vyama vyetu. Pamoja na ongezeko kubwa la mapato ya milangoni na mchango wa udhamini katika kipindi cha uongozi uliopita, bado kinachopatikana hakikidhi hata theluthi moja ya mahitaji muhimu. Haja ya kuongeza mapato ndiyo changamoto mama. Ikitatuliwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza makali ya changamoto nyingine.
- Ili kuvutia uwekezaji, udhamini na misaada kwenye mpira wa miguu, ni lazima tuhakikishe kuwa tunaendelea na jitihada za kujenga uaminifu wa utunzaji na matumizi ya fedha ndani ya TFF. Ipo haja ya kuhakikisha kuwa Kanuni za Fedha zinazingatiwa na hesabu zetu zinakaguliwa mara kwa mara. Mpango wa Tiketi za Elektroniki ni muhimu usimamiwe kwa nguvu zote kwa vile sio tu utatuongezea mapato bali pia utatoa picha ya uaminifu na ueledi.
Uhusiano na ZFA
21. TFF haina budi kufanya kila linalowezekana kudumisha
uhusino mzuri baina yake na ZFA. TFF inatambulika na FIFA kama msimamizi
wa mchezo wa mpira wa miguu nchini Tanzania. Lakini ukweli ni kuwa
mchezo wa mpira katika visiwa vya Unguja na Pemba unasimamiwa na ZFA.
Hakuna matarajio ya hali hiyo kubadilika. Kwa sababu hiyo, upo ulazima
wa kudumisha uhusiano uliopo na kuhakikisha kuwa ZFA inapata haki ya
kupewa baadhi ya miradi inayotokana na fedha za FIFA – FAP. Kwa vile
fedha hizo hatolewa kwa njia ya miradi, utaratibu tuliokubaliana ni
kuhakikisha kuwa kila mwaka baadhi ya miradi / semina zinafanyika
visiwani.
Wakaguzi wa Hesabu za TFF
22. Hesabu za TFF zinakaguliwa makampuni ya Ukaguzi wa Hesabu yafuatayo:
- TAC Associates – kwa hesabu zote za TFF
- KPMG – kwa fedha za FIFA
Bodi ya Wadhamini
23. Mkutano Mkuu wa Mwaka 2011 uliridhia kuundwa kwa Bodi ya
Wadhamini wa TFF na Mkutano Mkuu uliopita ulipitisha majina ya Wajumbe
wa Bodi ya Udhamini kama ifuatavyo:
- Said El Maamry – Mwenyekiti
- Mh. Joel Bendera – Makamu Mwenyekiti
- Dr. Ramadhani Dau – Mjumbe
- Steven Mashishanga – Mjumbe
- Mohamed Abdulaziz - Mjumbe
Mheshimiwa Rais, napenda kukubidhi taarifa hii ya makabidhiano leo
hii tarehe 2 Novemba 2013 kwa ufahamu na kumbukumbu za TFF. Tafadhali
jisikie huru kuomba ufafanuzi wa jambo lolote lililomo katika taarifa
hii au kuomba taarifa juu ya jambo ambalo kwa bahati mbaya
limesahauliwa. Sekretariati ya TFF inawajibika kutoa ufafanuzi
unaohitajika.
Tunakutakia wewe mwenyewe na uongozi wako kila la heri na mafanikio
katika kuingoza wa TFF kuelekea kule kunakotarajiwa na wapenzi wa mpira
wa miguu nchini. Wadau na wapenzi wote wa mpira wa miguu wanaoitakia
heri nchi yetu wapo nyuma yako.
Leodegar Tenga Angetile Osiah
RAIS WA TFF KATIBU MKUU WA TFF
CHANZO NI GPL
No comments:
Post a Comment