Dar es Salaam.
Siku moja baada ya Kamati Kuu ya Chadema kumvua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Taifa wa chama hicho, Zitto Kabwe, mama yake mzazi, Shida Salum ametoa ya moyoni akieleza kuwa kilichomkuta mwanaye kimefunika mabaya mengi yaliyopangwa afanyiwe.
Siku moja baada ya Kamati Kuu ya Chadema kumvua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Taifa wa chama hicho, Zitto Kabwe, mama yake mzazi, Shida Salum ametoa ya moyoni akieleza kuwa kilichomkuta mwanaye kimefunika mabaya mengi yaliyopangwa afanyiwe.
Baada ya Kamati Kuu ya Chadema kumvua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Taifa Zitto Kabwe, mama yake mzazi Shida Salum (pichani) aibuka kueleza jinsi zahama hiyo ilivyokuwa ‘ushindi’ kwa mwanae. PICHA | MAKTABA
“Kwa upande wangu naona kama ni ushindi kwa Zitto kutokana na jinsi ninavyojua hali ilivyo, mambo yalikuwa ni mengi mno na nikwambie tu, Zitto kuvuliwa uongozi kumefunika hayo yaliyokuwa yamekusudiwa kufanywa dhidi yake. Nilikuwa naomba Mungu kila siku ili afukuzwe Chadema,” alisema mama huyo wakati akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Tabata, Dar es Salaam.
Shida Salum alisema kuwa Mungu amemnusuru mwanaye na kusisitiza, “Watu walikaa na kutengeneza ripoti ya siri kuhusu Zitto na kuiweka kwenye mtandao kisha kuituma kwa wanachama wa Chadema wanaowafahamu. Mpaka wanafikia hatua hiyo maana yake ni kwamba wamejaribu njia zote za kummaliza, lakini wameshindwa.”
Alisema kutokana na hali ilivyo hivi sasa
amemnyang’anya mwanaye kwa muda simu zake zote za mkononi, kompyuta
mpakato (Laptop) pamoja na iPad ili asiwasiliane na watu, kwa maelezo
kuwa wapo wenye nia mbaya wanaomsaka kumpa pole za kinafiki. “Kwa sasa
nataka mwanangu atulize akili.”
Shida Salum, mbali na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, pia ni mwasisi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata) na Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo (Chawata).
Zitto pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dk Kitila Mkumbo juzi walivuliwa uongozi kutokana na uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu kilichokutana kwa siku mbili, kuanzia Novemba 20 mwaka huu katika Ukumbi wa Blue Pearl jijini Dar es Salaam, wakituhumiwa kukisaliti chama.
Mbali ya kuwavua uongozi Zitto, Dk Mkumbo pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Samson Mwigamba, pia Kamati Kuu imewapa siku 14 wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama.
Kwa uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge wake wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Katika ufafanuzi wake wa jana, Shida aliwataka
wanachama wa Chadema kuwa watulivu kwa maelezo kuwa Zitto hajafukuzwa
uanachama, “Siku nyingi walikuwa wanamwinda na hata hilo jambo ambalo
Chadema wanasema amefanya, hawana uhakika nalo.”
Juzi wakati akisoma uamuzi wa Kamati Kuu, mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema wamebaini kuwapo kwa mkakati mkubwa wa watu hao kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’, ambao umeandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’.
Alisema kikundi hicho vinara wake wapo wanne, Zitto anajulikana kama Mhusika Mkuu (MM), Mkumbo (M1), Mwigamba (M3) na mtu mwingine wa nne ambaye alieleza kuwa hajatambulika na anatumia jina la M2.
Atoa ya moyoni
Mama Zitto ambaye wakati akizungumza na gazeti hili alikuwa
amelala kutokana na kusumbuliwa na maradhi alisema, “Kutolewa katika
uongozi ni jambo la kawaida. Zitto hajafukuzwa chama ila anaweza
akafukuzwa maana kapewa siku 14 tu za kujieleza.”
Alisema kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibroad Slaa, kwamba chama hicho walimwondoa Aman
Kabourou (aliwahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini-Chadema) itakuwa Zitto,
inaonyesha jinsi watu walivyo na chuki na mwanaye.
“Hayo ni maneno ya chuki, maana hata Zitto naye
ana watu wake ambao wanaweza kutengeneza aina fulani ya chuki kwa
viongozi wa chama na wanaweza kupata wakati mgumu kufanya safari au
mikutano yao mikoani,” alisema.
Alisema tangu siku nyingi ndani ya Chadema
kulikuwa na mpango wa kumng’oa Zitto, akifafanua kuwa hata katika kikao
cha Kamati Kuu iliibuliwa hoja ya ruzuku za vyama, huku wajumbe
wakimshutumu Zitto kwamba kwa nafasi yake na Naibu Katibu Mkuu alitakiwa
kuitetea Chadema kuhusu ruzuku.
Katika vikao vya Kamati ya PAC, Zitto aliingia
katika malumbano na chama chake baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa
hesabu zake hazikaguliwi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), huku akitaka ruzuku kwenye vyama hivyo isimamishwe.
“Zitto alipoingia katika kikao cha Kamati Kuu
alishikilia msimamo wake kwamba kama Chadema inachukia ufisadi, nacho
lazima kihakikishe kinakaguliwa,” alisema na kuongeza;
“Wao wanaona ili waweze kusalimika katika suala
hili la ruzuku ni lazima wamfukuze Zitto. Chadema hawako sawa, hesabu
zao haziko sawa.”
Alisema kuwa tatizo lililopo ni kuwapo kwa mkakati
wa watu fulani kuiyumbisha Chadema , hivyo kila juhudi zinafanywa ili
kukitingisha chama hicho kipoteze mwelekeo.
“Siwezi kusema wamemwonea au hawajamwonea, wao
wametumia waraka wa Mwigamba ambao Zitto amekiri katika Kamati Kuu
kwamba hajawahi kuusikia wala kuuona, tofauti na Dk Kitila ambaye
amesema amewahi kuuona,” alisema na kuongeza;
“Zitto anahusishwa na kitu ambacho Chadema hawana
uhakika nacho, ukiusoma ule waraka katika aya ya mwisho umeandikwa hivi,
‘Huyu mtu tunayefikiria awe mwenyekiti hajaoa,
tumshauri aoe akikataa tutafute mtu mwingine’,
maana yake ni kwamba waraka huo ulikuwa haujamfikia Zitto, kama ungekuwa
umemfikia Zitto watu hao wasingemwomba Zitto agombee uenyekiti.”
Alipoulizwa nafasi yake ndani ya Chadema kutokana na yaliyomkuta mwanaye
alisema, “Mimi hawawezi kunitengenezea jambo. Hivi Zitto anaweza kuwa
mbaya mimi nikawa mzuri.”
Mama huyo alieleza kuwa tangu alipovamiwa na
majambazi nyumbani kwake, Aprili 19 mwaka huu hajawahi kuhudhuria kikao
chochote cha Chadema. “Wale wanaodhani Zitto kaonewa wanatakiwa kuwa
wavumilivu na wapole, wasubiri kwani kila kitu kinawezekana.”
Ushauri kwa mwanaye
Alisema kuwa mwanaye ana uamuzi wake na kwamba
hata kama Chadema itamfukuza uanachama, haitaweza kumnyang’anya vyeti
vyake vya elimu aliyoipata.
“Zitto anaweza kufanya kazi mahali popote duniani,
lakini pia ni mwalimu anaweza kuamua kufundisha. Ubunge ni mgawanyo wa
madaraka. Watu wote hatuwezi kuwa wabunge,” alisisitiza.
Alisema wakati Kikao cha Kamati Kuu kikifanyika
Zitto alikuwa nje ya nchi na kwamba yeye alimshauri kuhakikisha kuwa
anahudhuria kikao hicho.
“Alipotua tu na ndege aliniambia kuwa kuna foleni
na alitaka kukodi pikipiki ili awahi kikao, aliniambia lazima aende ili
kujua hatima yake.
Aliacha gari lake na kwenda na hata mimi
nilimsisitizia kwamba ni lazima aende katika kikao,” alisema. Alisema
kuwa Zitto alipofika katika kikao hicho aliweza kuzima hoja zote
zilizomhusu ikiwamo ya ruzuku za vyama, kwamba baadhi ya wajumbe
walipoona amebadili mwelekeo wa kikao, mjumbe mmoja (akamtaja kwa jina)
aliibua waraka uliomng’oa Zitto katika wadhifa wake.
“Unajua Kamati Kuu ilijadili zaidi kuhusu ruzuku.
Hata ule waraka uliongezwa maneno baada ya baadhi ya wanachama kumpora
Mwigamba laptop yake alipokuwa mkoani Arusha katika kikao cha Chadema,”
alisema.
Huku akiwataja wanachama wa Chadema walioongeza
maneno katika waraka huo (wakiwamo wabunge wawili) na viongozi wa ngazi
za juu wa Chadema, mama Zitto alisema kilichomkuta mwanaye ni ushindi
mkubwa, kwamba alipangiwa kufanyiwa makubwa zaidi ya yaliyomkuta.
“Hakuna amani maana ukisikia kengele inagongwa
hapa nyumbani unasema hao ndiyo wamekuja kumuua Zitto nini, hivi sasa
mpaka walinzi wanaolinda hapa wakisikia unakuja nyumbani kwa Zitto
lazima wakuandike jina na kukufuatilia,” alisema mama huyo.
Dk Kitila alonga
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Mkumbo alisema
kutokana na ushauri wa watu mbalimbali, yeye na Zitto wamepanga
kukutana na waandishi wa habari na kutoa tamko.
“Tumepanga mimi na Zitto tutatoa ufafanuzi kuhusu jambo hili, nadhani ni kesho (leo), tutawajulisha lakini,” alisema.Baada ya chama hicho kutangaza kuwaengua katika uongozi Zitto na Dk
Kitila, saa mbili baadaye Makamu Mwenyekiti Taifa wa Chadema, Said Arfi
aliandika barua ya kujiuzulu.
No comments:
Post a Comment