SHIRIKA
la Umeme Tanzania (Tanesco), limeanzisha operesheni maalumu ya
kukusanya madeni yanayofikia Sh bilioni 233, ambapo wateja watakaokaidi
zikiwamo taasisi za umma na binafsi, zitakatiwa umeme.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi
Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni
129 ni za taasisi za Serikali ikiwamo Zanzibar inayodaiwa Sh bilioni 70
na Sh bilioni 104 watu, taasisi binafsi na viwanda.
“Kwa sasa shirika limeanzisha kampeni maalumu ya kukusanya madeni
itakayojumuisha kutoa notisi ya kutaka wateja kulipa ndani ya muda huo
na kuwakatia wote ambao hawajalipa.
“Tunawataka wateja wote walipe madeni yao mapema iwezekanavyo ili kuepuka usumbufu,” alisema.
Kukatika umeme Mramba pia alikiri kutokea kwa hali ya kukatika umeme
katika baadhi ya maeneo ya nchi hasa Kanda ya Ziwa na baadhi ya maeneo
ya Dar es Salaam hasa Ubungo na katikati ya Jiji hivi karibuni.
Akielezea hali hiyo, alisema ilisababishwa na hitilafu za mtambo
zilizotokea katika vituo vya Sokoine na Ubungo, Dar es Salaam pamoja na
kuanguka kwa nguzo kubwa mbili za vyuma wilayani Kahama.
Alifafanua, kuwa Ubungo kulitokea wizi wa nyaya za shaba za ambazo inaaminika wezi hao huziuza kama chuma chakavu.
Kwa upande wa Kahama, kulitokea wizi wa vyuma ambavyo wezi huvitumia
kutengeneza mikokoteni ya kukokotwa na ng’ombe na majembe ya kulimia ya
plau.
“Tumepata hasara kubwa ya Sh bilioni 1.2 Kahama na Sh milioni 200 Ubungo.
“Tumepata hasara kubwa ya Sh bilioni 1.2 Kahama na Sh milioni 200 Ubungo.
Tunatoa rai kwa Watanzania kujali miundombinu ambayo ni rasilimali ya
Taifa na kuepuka vitendo vinavyoleta usumbufu kwa Watanzania wenzao,
kusababisha hasara na kurudisha nyuma hatua kubwa za maendeleo
zilizokwishapigwa,” alisema.
Umeme wa mafuta Kuhusu hali ya uzalishaji umeme, Mramba alisema ni ya
kuridhisha na hakuna upungufu wa umeme pamoja na mahitaji ya huduma
hiyo kuendelea kuongezeka.
Hata hivyo, alibainisha kuwa bado Tanesco inaendelea kutumia mitambo
ya mafuta ya kuzalisha umeme wa dharura ambao ni ghali, ili kukidhi
ongezeko la mahitaji linaloendelea. Mahitaji ya umeme kwa sasa kwa
mujibu wa Mramba ni megawati 898 tofauti na ilivyokuwa mwaka jana,
ambapo mahitaji yalikuwa megawati 851.
“Hii imelazimu kuzalisha umeme zaidi ili kukidhi mahitaji haya ya
ziada. Ni muhimu kufahamu kuwa kiasi kikubwa cha uzalishaji kinatokana
na mitambo ya mafuta,” alisema.
Alielezea uwiano wa mchango wa mitambo hiyo katika kukidhi mahitaji,
kwamba mitambo ya mafuta, ambayo ndiyo ghali zaidi, inatoa asilimia 45
ya umeme unaozalishwa.
Mitambo ya gesi ambayo ni ghali pia lakini si kama ya mafuta, inatoa
asilimia 42 ya umeme huo, huku mitambo ya maji ambayo ndiyo inayotoa
umeme kwa gharama nafuu zaidi, ikichangia asilimia 13 tu ya mahitaji ya
umeme nchini.
Rekodi ya wateja Katika hatua nyingine, Tanesco imevunja rekodi ya
kuunganishia umeme wateja 143,000 mwaka jana, idadi ambayo haijawahi
kufikiwa tangu kuanzishwa kwa shirikia hilo.
Hata hivyo, Mramba alisema bado kuna maombi mengi hayajafanyiwa kazi,
lakini akaahidi kuwa wateja wote walioomba kuunganishiwa umeme mwaka
jana, watahudumiwa kwa kasi na ifikapo Februari wataanza kupata huduma
hiyo.
“Tutaendelea kuwaunganishia umeme kwa kasi kama tulivyoahidi ili
ifikapo mwishoni mwa Februari tuwe tumewaunganishia. Vifaa vinaendelea
kuwasili na kazi zinaendelea vizuri,” alisema Mramba. Ili kuendeleza
kasi hiyo, alisema Tanesco itabadilisha utaratibu wa ununuzi wa vifaa
ili kuondokana na matatizo ya mara kwa mara ya uhaba.
“Hii itajumuisha ununuzi wa vifaa kwa wingi mikoani ili kupunguza
mlundikano wa majukumu yanayofanyika makao makuu,” alisema. Hujuma
mitandaoni Mramba pia alielezea masikitiko yake kutokana na kuibuka kwa
baadhi ya watu wanaohujumu shirika hilo katika mitandao ya mawasiliano
nchini.
Kwa mujibu wa Mramba kuna akaunti za mtandao wa twitter
zilizoanzishwa na baadhi ya watu zinazodaiwa kuanzishwa na Tanesco.
“Twitter hizi zimekuwa zikitumika kuchafua shirika na kukejeli wateja.
Majina yake ni Tanesco@TANESCO-, TanescoEscobar@tanescobar na TANESCO LTD-@tanesco-,” alisema.
Alisema
wameiharifu Mamlaka ya MawasilianoTanzania (TCRA) na Jeshi la Polisi,
ili wachukue hatua stahiki kwa mitandao ya kijamii inayotumika
kulichafua shirika hili kwa kufungua akaunti kwa kutumia jina la
Tanesco.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment