Niwape
hi kwa furaha sana wapendwa wasomaji wa safu hii, ingawa zaidi
ningependa ziwafikie wanafunzi popote pale gazeti hili linaposomwa. Hawa
jamaa ni wadau wangu wakubwa sana, hasa katika kubadilishana mawazo
inapobidi.
Juzi nilikuwa naperuziperuzi kwenye mtandao, mara nikakutana na picha
za aibu zilizopigwa na msichana ambaye ametambulishwa kama ni
mwanafunzi, haikuelezwa kama ni denti wa sekondari au vyuo, lakini kwa
uzoefu, inaonekana kabinti ni ka sekondari!
Nilipoziona, zikanikumbusha miaka kadhaa nyuma, kama minne au mitano
hivi, wakati picha za msichana mmoja, aliyekuwa amevalia fulana
zinazotumiwa na shule moja ya sekondari iliyopo Mbezi, jijini Dar es
Salaam, zilipovuja na kufika gazetini. Binti huyo, alipigwa picha akiwa
katika mikao mbalimbali akiwa mtupu!
Simulizi zilivuja kwamba kabla
ya picha hizo kufika magazetini, ambako zilichapishwa, msichana huyo
alishajaribu mara nyingi kuzuia zisisambae lakini bila mafanikio. Unajua
ilikuwaje?
Mtu wa kwanza kuzidaka, alimfuata na kumuonyesha picha zake na
kumtisha kuwa angezipeleka magazetini au kwa wazazi wake kama asingempa
uroda. Kwa hofu, denti akalazimika kutii matakwa yale. Basi ikawa
mchezo, picha zikaendelea kuhama kutoka kwa huyu hadi huyu na binti
akajikuta akigeuka mtumwa wa ngono ili kulinda heshima yake, hadi
alipokuja kugundua kuwa angetumika hadi mwisho wa dunia, akaamua
kukataa, akisema liwalo na liwe, ndipo zilipofika gazetini na kutoka!
Kuna jambo moja la dhahiri kupitia kwa yule dada, kwamba alijuta na
alifahamu kwamba alifanya makosa kupiga picha zile, ambazo kwa vyovyote
alifanya hivyo akiwa na akili timamu kwani zote alionekana akiichekea
kamera. Kama asingejuta, asingekubali kuwaziba watu midomo kwa njia ya
kuutoa mwili wake kwa watu asiowafahamu.
Nimeanza na mchapo huo kama kuwaweka sawa ili muweze kunielewa
ninachotaka kuwaambia na ambacho nyinyi wanafunzi, hasa wa kike, mtambue
na kuchukua hatua ikibidi.
Utandawazi katika dunia ya sasa imeufanya
ulimwengu kuwa mdogo unaofanana na kiganja. Simu za mikononi ni kila
kitu, unazungumza na mwenzako aliye popote, unaingia mtandao wowote wa
internet, unatuma au kupokea picha, sauti na kila unachokijua. Kwa maana
hiyo, mtu mmoja anaweza kupiga picha akiwa Mbinga, kisha dakika moja
baadaye akaonekana katika mtandao wa Facebook, Twitter, Instragram au
popote na kujikuta picha hiyo ikionekana dunia nzima.
Wimbi la wadada kujipiga picha za utupu limeibuka upya na baadhi ya
wanafunzi wamejikuta wakiingia mkenge. Ni hivi, wale akina dada,
wakiwemo wasanii nyota wasiojitambua, wanapiga picha na kuziweka
mitandaoni kwa ajili ya kujiuza. Yes, wanajiuza, tunajua!
Lakini napata taabu kidogo na wewe mwanafunzi kwa kufanya vitendo hivi. Unapiga picha hizo ili iweje anko? Unajiuza, kwa nini?
Kati ya watu ambao nafsi zitawashtaki baada ya kuwa zimewasuta sana,
ni wanafunzi wanaojaribu kuingia katika ujinga huu. Ni punguani tu
anaweza kukubali utupu wake uonekane dunia nzima. Madenti ni lazima wawe
tofauti, waonyeshe kwa nini wao wanachukuliwa kuwa ni wasomi.
Kujipiga picha hizo na kuzitupia kwenye mitandao, ni kuonyesha kuwa
kiwango cha kufikiri ni sawa na cha wale machangudoa wa Uwanja wa Fisi,
Manzese Dar , ambao hawana mbadala wa kufanya zaidi ya
kuuza miili yao.
Madenti wengi wanapigana picha za utupu na wengine hadi video. Huenda
hufanya hivyo kwa kujifurahisha, lakini unapovua nguo na kumruhusu mtu
akufotoe, ni zaidi ya kujifurahisha. Ninaogopa kama picha zako zitavuja
na kumfikia mtu mwenye VVU, ambaye atakuahidi kutozipeleka magazetini
kama utampa uroda. Huoni kama unajiua mwenyewe?
Tafakari, chukua hatua!
Je, una maoni yoyote, mkasa uliowahi kukukuta ukiwa shuleni ambao ungependa ujulikane kwa wasomaji? karibu ushiriki nasi kwa kutuandikia kupitia barua pepe ojukuus@yahoo.com
Tafakari, chukua hatua!
Je, una maoni yoyote, mkasa uliowahi kukukuta ukiwa shuleni ambao ungependa ujulikane kwa wasomaji? karibu ushiriki nasi kwa kutuandikia kupitia barua pepe ojukuus@yahoo.com
No comments:
Post a Comment