
AZAM FC inazidi kuusogelea ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kufanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro na hivyo kuiacha Yanga inayoshika nafasi ya pili, kwa pointi nne.
Ushindi huo ambao umepatikana kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, jana, unamaanisha kuwa hata kama Yanga ikishinda mechi ijayo itakuwa bado ipo nyuma kwa pointi moja dhidi ya Azam ambayo kama ikitwaa ubingwa itakuwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo tangu ilipoanzishwa miaka michache iliyopita.
Mpaka kipindi cha kwanza kinakamilika, Oljoro ilikuwa ikionyesha kiwango kizuri huku mabeki wake wakiwa wagumu kupitika.
Alikuwa ni John Bocco ndiye aliyeipatia Azam bao pekee kwenye dakika ya 71, akiunganisha pasi ya Mudathir Yahaya ambaye alimpokonya mpira Babu Ally.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kally Ongala, alisema: “Mechi ilikuwa ngumu kwa kuwa Oljoro wapo kwenye nafasi za chini, hivyo walihitaji ushindi lakini tunashukuru tumeshinda.”
No comments:
Post a Comment