MATARAJIO ya Simba kupata angalau nafasi ya pili ili kushiriki michuano ya kimataifa mwakani yamezidi kupotea baada ya jana kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Coastal Union ya Tanga, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba ambayo kutokana na matokeo hayo imebaki katika nafasi ya nne ikiwa nyuma ya Azam, Yanga na Mbeya City, ilishindwa kutumia nafasi kadhaa ilizopata, wakati wapinzani wao hawakuwapanga wachezaji wao wengi nyota, wakiwemo Haruna Moshi ‘Boban’, Jerry Santo na Juma Nyosso.
Alikuwa ni Hamad Juma wa Coastal aliyepeleka machungu kwa Simba baada ya kufunga bao katika dakika ya 45, ambapo aliwachambua mabeki wa Simba kabla ya kupiga shuti jepesi lililojaa wavuni na kumshinda kipa Ivo Mapunda.
Simba iliamka katika kipindi cha pili na kufanya mashambulizi kadhaa lakini haikuweza kutumia vizuri nafasi hizo.
Katika mechi hiyo, kipa wa Coastal, Fikiri Selemani ambaye ana umri wa miaka 17, akitokea kikosi B cha timu hiyo, alionyesha kiwango kizuri na kusifiwa na kocha wake, Yusuf Chippo.
Akizungumzia mchezo huo, Chippo alisema timu yake ipo vizuri na aliamua kuwatumia wachezaji kadhaa wa kikosi B kwa kuwa aliweka imani kwao.
Upande wa Simba, hakuna ambaye alijitokeza kuzungumzia mchezo huo.
No comments:
Post a Comment