WAKATI
ninaandika makala haya, upigaji kura katika Uchaguzi mdogo wa Jimbo la
Kalenga mkoani Iringa ulikuwa unaendelea kufanyika na kwa maana hiyo
sikuwa na matokeo kuweza kujua nani ataibuka kidedea.
Lakini ninafahamu kwamba kulikuwa na ushindani mkali kati ya wagombea
wa CCM (Godfrey Mgimwa) na Chadema (Grace Tendega). Ingawa wapo
washiriki wengine, lakini kama ambavyo imejitokeza katika miaka ya hivi
karibuni, vyama hivi ndivyo vimeonekana kuwa na ushindani mkali katika
siasa za Tanzania Bara.
Vyama vyote vilifanya kampeni kubwa kuhakikisha mgombea wake anakuwa
ndiye mwakilishi wa jimbo hilo ambalo limekuwa wazi kufuatia kufariki
kwa mbunge wake, aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu William Mgimwa
mapema mwaka huu.
Kama kawaida ya siku zote, Chadema wamekuwa hawawaamini CCM,
wakiamini wanacheza rafu zinazosababisha wao kushindwa katika chaguzi
kadhaa. Kutokana na sababu hiyo, mara nyingi wamekuwa wakilalamikia
suala hilo na kuelezea mikakati yao kuhakikisha jambo hilo halijitokezi.
Safari hii, wameibuka na kauli mpya kwamba ili kulinda kura zao,
watatumia helikopta, ambayo mwanzo waliitumia katika kampeni zao, ili
kuzuia upotevu wowote wa kura. Kwamba wakiwa angani, wataweza kufuatilia
mwenendo wa magari yatakayokuwa yamebeba masanduku ya kura.
Ninapata shida kidogo kuwaelewa Chadema kuhusu jambo hili. Ingawa
sihusiki na malumbano baina ya polisi waliozuia matumizi ya chombo hicho
cha usafiri na chama hiki kikuu cha upinzani, najaribu kuangalia jinsi
gani wanasiasa wanavyoweza kucheza vizuri na akili za watu ili kujizolea
mashabiki.
Watu wenye akili wanajaribu kujiuliza ni kwa namna gani helikopta ile
inavyoweza kulinda kura wakati zoezi la kuzihesabu hufanyika ardhini,
tena ndani ya vyumba maalum? Hii, kama nilivyosema ni namna ya
kujitafutia mashabiki kwa kucheza na akili zao kwa bei rahisi.
Kila chama kinao mawakala wake katika vituo vyote vya kupigia kura.
Hawa ndiyo wasimamizi wakubwa wa kura, kwani kwa muda wote wako macho
kuhakikisha haufanyiki udanganyifu wala hila za aina yoyote. Na kwamba
baada ya zoezi la kupiga kura, wote wanapaswa kufuata taratibu zote kama
zilivyoainishwa na msimamizi wa uchaguzi.
Kwa maana nyingine, helikopta ni kama inayotumika kuharibu fikra za
watu juu ya kumpata mwakilishi wamtakaye, badala yake akili yao
wanaiweka katika kuitazama inapopaa angani.
Hata hivyo, naamini kuwa uchaguzi huo umepita kwa amani na vyama hivyo vitakuwa na la kujifunza.
No comments:
Post a Comment