Mwanasheria wa Okwi, Edgar Agaba, ambaye alifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, alikumbana na wakati mgumu baada ya kiongozi huyo kusisitiza mambo mawili makuu, likiwemo lile la fidia zaidi ya Sh milioni 200 kama watashindwa kuelewana.
“Kikao kile watu hawasemi ukweli, mwanasheria wa Okwi alibanwa sana kwa kuwa katika mkataba wa Yanga na Okwi unaeleza hivi; mchezaji ndiye atajitafutia kibali kwa kuwa aliihakikishia klabu ana uhakika wa kikupata.
“Lakini Okwi hakucheza mechi sita, hilo ni tatizo lake. Ajabu fedha yake akaanza kudai mwishoni na kususa kucheza, utaona kama kukiuka mkataba kila upande ulifanya. Sasa yeye ikawa zaidi kwa kuwa mwisho aliacha kucheza mechi zote zikiwemo za Simba na Azam ambazo ndiyo Yanga ilipoteza ubingwa.
“Hivyo mwenyekiti (Manji) amesema Okwi achague hilo au kupunguza mkataba, maana hakuonyesha kuwa msaada mkubwa kwa Yanga kwa muda aliokuwepo. Lakini pia anaweza kushtakiwa na kudaiwa fidia za kuikosesha Yanga ubingwa ambayo inaweza kuzidi hata milioni 200,” kilieleza chanzo cha uhakika.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Agaba alikubaliana na Manji kwamba atamfikishia masuala hayo Okwi na baada ya hapo watajadili na kumpa jibu ndani ya siku chache.
Kwa mambo yalivyo, inaonekana ngoma ni nzito kwa Okwi ambaye aliondoka nchini baada ya kususa kuichezea Yanga.
Lakini imeelezwa uongozi wa klabu hiyo uko tayari kuendelea kufanya naye kazi kama watafikia makubaliano.
CREDIT: CHAMPIONI


No comments:
Post a Comment