
CHANZO: CHAMPIONI JUMATANO
ADUI watano ambao watampa shida kubwa Kocha wa Yanga, Marcio Maximo kutoka Brazil, wametajwa na wengine wamo ndani ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Wachambuzi watatu maarufu wa soka nchini, Edibily Lunyamila, Bakari Malima na Saleh Ally, wameeleza kuwa, adui hao kwa Maximo ni viwanja vibovu, waamuzi wabovu, hujuma, uzalendo mikoani na presha ya Simba.
Wakijibu maswali kuhusiana na ujio wa Maximo katika klabu, wote walieleza kuhusiana na masuala ambayo yatampa wakati mgumu Mbrazili huyo na anapaswa kupambana vilivyo kuwashinda adui hai.
“Viwanja ni changamoto kubwa, haitakuwa rahisi kwake kama ilivyokuwa kwa Taifa Stars ambayo ilikuwa ikifanya mazoezini na kucheza mechi zake kwenye Uwanja wa Taifa.
“Waamuzi watakuwa adui mwingine wa Maximo, unajua viwango vyao vilivyo na hili liko ndani ya TFF na chama cha waamuzi hao. Walifanyie kazi kwa kuwa halitamkuta Maximo tu, hata makocha
wengine na wamekuwa wakilalamika.
“Nafikiri kuna vitu vingine ana taarifa navyo, lakini ni lazima uongozi wa Yanga ukae na kumueleza kuhusiana na hali halisi, hasa kama atakwenda mikoani,” alisema Lunyamila, ambaye pia ni winga hatari wa zamani wa Yanga, Simba, Mtibwa Sugar na Taifa Stars.
Kuhusiana na hilo, Malima, beki wa zamani wa Pan African, Yanga, Simba na Taifa Stars, alisema:
“Kweli kuna watu wapo tayari kuihujumu Yanga bila kujali wao ni Yanga, hii itakuwa ni moja ya vitu ambavyo vinaweza kumtokea, ingawa uongozi unatakiwa kukaa karibu na kudhibiti hili, si wote wanaupenda uongozi wa klabu.
“Pili mikoani, kuna suala la uzalendo. Wakati sisi tunacheza tumekutana nalo hili na mtu anaweza kuwapiga chenga mabeki na kipa, akafunga halafu mwamuzi akasema ameotea. Haya mambo yanatokea.
“Kingine uongozi uwe makini kumuweka vizuri kisaikolojia kwamba mashabiki sasa watakuwa wakimzomea vibaya na si kumuunga mkono kama ilivyokuwa timu ya taifa. Vizuri akajua mapema kusudi siku moja asije akamvaa shabiki au mwamuzi.”
Kwa upande wa Saleh Ally, ambaye ni mmoja wa wachambuzi wakongwe zaidi wa soka nchini, alisisitiza kuwa, presha kubwa kutoka Simba ni kati ya hao maadui watano.
“Kweli pia waamuzi, viwanja kitu ambacho Maximo ameshaanza kukiona na hujuma ni mambo ambayo yanaziandama klabu na wakati mwingine wanahujumiana wao kwa wao. Mwisho muathirika anakuwa kocha,” alisema Saleh Ally (soma uchambuzi wake uk 9).
Tayari Maximo ameanza kuinoa Yanga kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara. Msimu uliopita, Yanga ilimaliza ikiwa katika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Azam FC ambao walichukua kombe hilo kwa mara ya kwanza.
No comments:
Post a Comment