KATIKA Gazeti la Risasi Jumamosi la Aprili 26, mwaka huu ukurasa wake wa nyuma kulikuwa na habari yenye kichwa;UOZO MAHOSPITALINI...OFM YAIFUNGIA KAZI PALESTINA.Katika habari hiyo, mapaparazi wa Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ walitinga Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni, Dar, Palestina iliyopo Sinza na kufanya ‘upelelezi’ kuhusu kuwepo kwa madai kwamba, huduma za sehemu hiyo ya afya si nzuri.
OFM walifanya kazi mambo yakajulikana na kuanikwa hadharani ambapo ilitegemewa kuwa, hali ya huduma ingebadilika.
Hata hivyo, juzi kati, wana-OFM watatu walitinga hospitalini hapo wakifuatilia majibu ya vipimo vya ndugu wa mmoja wao na kukutana na kisanga kipya kabisa.
Kisanga hicho ambacho kilirekodiwa hatua kwa hatua na mapaparazi wetu kilimhusu mgonjwa mmoja (jina tunalo) akiteseka na nduguye wa kike (naye jina tunalo) kupita vyumba vya madaktari kwa lengo la kupata tiba.
Mgonjwa huyo aliyekuwa kwenye kiti cha matairi cha wagonjwa (wheel chair) alionekana kuwa hoi kwa vile alikuwa hawezi kutembea wala kujieleza sawasawa.
Mawasiliano yote ya OFM na mgonjwa huyo yalifanywa kupitia ndugu yake ambaye alisema alikatisha shughuli zake za siku hiyo kwa ajili ya kumpeleka mgonjwa hospitalini hapo.
Malalamiko ya ndugu huyo yalikuwa haya:
“Mimi nashangaa hii hospitali haina chumba cha wagonjwa wa dharura (emergence), tangu nimefika napata usumbufu wa kufuata taratibu zote kama wagonjwa wa kawaida.
“Mtu anaumwa hoi kama hivi, badala wampeleke chumba cha dharura, wao wamenipa kiti chao eti tufuate taratibu. Sasa mtu akizidiwa akifa je?” alilalama ndugu huyo.
Ndugu huyo alisema kuwa, baada ya kuzurura kwa karibu saa nzima na mgonjwa wake, daktari mmoja alitokea na kuonesha kutofautiana na wauguzi ambapo aliwauliza kisa cha kumwacha mgonjwa huyo kwenye baiskeli badala ya kumpeleka kwa daktari.
“Ilibidi yule dokta, tena Mungu ambariki sana, akamwandikia nimpeleke kupima malaria, lakini kule nako ilibidi nikae kwenye foleni kwa muda mrefu.
“Lakini daktari wa maabara naye alimlaumu daktari aliyemshauri mgonjwa huyo afike hapo akisema ilipaswa mgonjwa wangu apewe chumba cha mapumziko na kupatiwa huduma akiwa hukohuko badala ya kumsumbua kwenye foleni zisizo na ulazima,” alisema ndugu huyo.
Alizidi kudai kwamba vipimo vilionesha kwamba mgonjwa hakuwa na kitu alichoumwa mwilini hivyo aliandikiwa dawa za kupunguza maumivu (panadol) na kutakiwa kwenda kuzinunua dirishani.
“Lakini pale dirisha la dawa napo nikakutana na tatizo jingine, mhusika alisoma kadi na kudai shilingi 200 kwa ajili ya malipo ya panadol.
“Nilitoa noti ya shilingi 5,000, akaikataa akisema eti hapokei, anapokea shilingi 200 kamili na kama sina nikanunue dawa hiyo nje ya hospitali,” alisema ndugu huyo huku akisikitika.
Hatua kwa hatua ya matukio hayo, OFM ilikuwa ikipiga picha kwa kamera ya kisasa kwa ajili ya ushahidi na kumbukumbu.
CHANZO NI GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment