MBALI na Askofu wa Kanisa la Full Gosple Bible Fellowship, Zacharia Kakobe kuteswa na misukule inayodaiwa kufufuliwa na baadhi ya makanisa ya kiroho nchini, Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ (pichani) naye ameibuka na kucharukia suala hilohilo.
Akizungumza na Uwazi juzi, Mzee wa Upako alisema suala la misukule linamtesa sana na kwamba anapingana na kufufuliwa kwao na baadhi ya wachungaji wa makanisa mbalimbali wanaojigamba kufufua misukule wakati si kweli na ni utapeli mtupu.
MZEE WA UPAKO ANAFUNGUKA:
“Kuna baadhi ya viongozi wa makanisa ya kioroho (bila kutaja majina) wanadanganya watu kuwa wanatoa misukule, si ukweli kabisa ni uongo. Wanatafuta namna ya kula sadaka za waumini wao kwa kuonekana wanaweza sana mambo ya kiroho,” alisema Mzee wa Upako na kuongeza:
“Hawa wachungaji wanatuchafua sana sisi tunaosimamia Neno la Mungu, wanaharibu Kanisa la Mungu kwa kudanganya waumini wao kwa sababu ya pesa tu. Hebu fikiria kuna wengine wanatoa hadi shilingi 400,000 kwa mtu ili akubali kufanywa msukule feki na baadaye aombewe kanisani tena nimesikia wanatengenezewa hati za kifo kuonesha kuwa kweli watu hao walifariki dunia wakati si kweli, wamwogope Mungu.
“Huo ni usanii ndani ya Kanisa la Mungu. Nasema naumizwa sana na wachungaji wa namna hii, nateseka sana na hili jambo. Ninayo mpaka CD za mahubiri za baadhi ya viongozi wa makanisa wanaodanganya kuwafufua misukule lakini kwa busara siwezi kuwataja ila wanajijua kwa sababu hata dhamira zao zinawashuhudia.”
TURUDI KWA KAKOBE
Akikazia zaidi, Askofu Kakobe alisema, anayedai ana uwezo wa kufufua misukule ni muongo na kwamba atakuwa anaabudu shetani.
“Mwenye uwezo wa kufufua ni Yesu Kristo pekee na alifanya hivyo kwa sababu ya utukufu wa Mungu na si vinginevyo, si binadamu wa kawaida ambaye amepewa upako wa Mungu anadanganya watu kuwa anao uwezo wa kumtoa mtu ambaye alichukuliwa msukule,” alisema Askofu Kakobe huku akisisitiza kwamba mtumishi yeyote wa Mungu anaweza kufanya muujiza huo kwa utukufu wa Mungu lakini si kwa sababu ya kuonesha yeye anaweza.
CHANZO NI GPL
No comments:
Post a Comment