Askofu
wa kanisa la Evanglist Assembels of God Tanzania (E.A.G.T) Singida
mjini, John Mafwimbo akizungumza kwenye mkutano wa Injili uliofanyika
kwenye viwanja vya shule ya msingi Ukombozi mjini Singida.Pamoja na
mambo mengi, askofu Mafwimbo amewasihi wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba, kufanya mambo waliyotumwa na Watanzania na si vinginevyo.
Mchungaji
wa kanisa la Free Pentekoste Tanzania Singida mjini, Boniface Ntandu,
akiwahubiria waumini wa madhehebu ya dini mbalimbali waliohudhuria
mkutano wa injili uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi
Ukombozi.
Na Nathaniel Limu, Singida
Makanisa ya Kipentekoste mkoani Singida, yameungana na Watanzania wengine kuwaomba wajumbe wa Bunge Maalum la kuandaa Katiba mpya,kujiepusha na mambo/vitendo ambavyo hawakutumwa na wananchi na badala yake washikamane na wavumiliane ili waweze kufanikisha kupatikana kwa katiba itakayoendeleza amani na utulivu uliopo nchini.
Makanisa hayo ambayo ni pamoja na Free Pentekoste Tanzania na Evangelist Assembles of God Tanzania (E.A.G.T.),yamedai kwamba matusi, dharau, ugomvi na kejeli za aina mbalimbali hazitachangia kupatikana kwa Katiba inayotarajiwa na Watanzania.
Wamedai vitendo hivyo, vitachangia pamoja na mambo mengine kubomoa umoja na undugu uliojengeka kwa miongo mingi na vitakaribisha vitendo viouvu kama vinavyofanywa na vikundi vya Boko haramu na Alshabab.
Akizungumza kwenye mkutano mkubwa wa injili uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Ukombozi mjini Singida, Askofu wa E.A.G.T, John Mafwimbo alisema ni wakati sasa kwa waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini kufunga kwa ajili ya kufanya maombi kuliombea Bunge Maalum la Katiba,liweze kutekeleza yale yote waliyotumwa na Watanzania.
"Tuwaombee bila kuchoka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba,waweze kututengenezea/kutuboreshea vizuri Katiba na wala wasituchanganye,ili sisi huku waumini wa madhehebu ya dini na Watanzania wengine wasiokuwa na dini tuje tufanye uamuzi sahihi wakati wa kuipigia kura Katiba hiyo",alifafanua.
Akifafanua zaidi, Mafwimbo, alisema kazi ya wajumbe nikuwajengea Watanzania mazingira mazuri ili waje kupigia kura Katiba itakayokidhi mahitaji yao ya zaidi ya miaka 50 ijayo.
Kwa hali hiyo, Askofu Mafwimbo amewashawishi wajumbe hao kuimarisha utamaduni wa kuvumiliana, kupendana na kumaliza tofauti zao wao kwa wao.
"Niwakumbushe tu wajumbe wetu, kwamba Watanzania ni waumini wazuri wa amani na utulivu. Kitendo hicho kimeendelea kuchangia nchi yetu kupaa kimaendeleo na wakati huo huo, sisi waumini tunaendelea kuabudu kwa uhuru mpana bila usumbufu wa aina yo yote",alisema na kuongeza kwa kusema; "Endapo hatutapata katiba stahiki,tutakuwa tunakaribisha vurugu kama zile zinazofanywa na makundi ya boko haramu".
No comments:
Post a Comment