Klabu ya Yanga na wawakilishi wa
michuano ya shirikisho ya Afrika imewatupia virago rasmi makocha
wabrazil Marcio Maximo na msaidizi wake, Leonardo Neiva kwa kile
kinachoelezwa kutofurahishwa na mwenendo wa timu katika ligi licha ya
kuwa na wachezaji wengi mastaa wa kigeni na kutumia mamilioni katika
kusajili wachezaji mahiri wa kigeni.
Yanga hivi karibuni ilimsajili mrundi na mfungaji bora msumu uliopita, Hamis Tambwe kutoka kwa mahasimu wao (Simba) akiungana na Mliberia, Kpah Sherman, Wanyarwanda Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite na Mbrazil Andrey Coutinho kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni
Tayari uongozi wa Yanga, katika kile kinachoonekana pesa si tatizo, chini ya Mwenyekiti bilionea Yusuf Manji umemrudisha klabuni aliyekuwa kocha wa zamani, Mholanzi Van de Pluijm, atakayesaidiwa na kocha mzalendo na mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa na klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa.
Katika maelezo yake, Manji amewatakia kila la kheri wabrazil hao na kusema na mungu akipenda wataendelea kushirikiana nao katika siku za usoni.
Tayari makocha hao wawili , Pluijm na Mkwasa wameshatambulishwa kwa wachezaji wa Yanga na habari za uhakika kutoka klabu hapo zinasema baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu, Pluijm, aliyewahi kuipatia yanga mafanikio katika ligi kuu, ana anza kibarua chake rasmi leo.
Hata hivyo, kuondoka kwa Maximo, aliyewahi kuajiriwa na Serikali ya Tanzania kama kocha mkuu wa timu ya taifa, Stars Stars katika miaka ya nyuma na kurudi nchini kivingine kuongoza Yanga, kumegubikwa na sintofahamu huku kukiwa na habari kuwa bado anavutana na uongozi juu ya mafao yake kwa kuvunjiwa mkataba.
Maximo, aliiongoza Yanga katika mechi tisa ndani ya miezi mitatu (akipoteza mechi mbili katika mechi saba) baada ya kupokelewa kwa shangwe uwanja wa ndege alipowasili kuwafundisha mabingwa hao wa zamani wa Tanzania.
Inasemekana kuondolewa kwake kunatokana na kipigo cha mabao 2-0 Yanga ilichokipata baada ya kufungwa na watani wao wa jadi, Simba katika mechi isiyo ya ligi (Nani Mtani Jembe) chini ya kocha Mzambia Patrick Phiri.
Maximo anakuwa kocha wa pili kufukuzwa na Yanga baada ya matokeo mabaya ya mechi ya Nani Mtani Jembe. Kocha kutoka Uholanzi, Ernie Brandts, pia alifukuwa baada ya kupata kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Simba .
No comments:
Post a Comment